Mashemasi na Mafrateri waonywa kuepuka ubinafsi




n Na Thompson Mpanji, Mbeya

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Chengula (IMC) amewaalika mashemasi na mafrateri kuacha ubinafsi  na badala yake waendelee kudumisha umoja, mshikamano na upendo kama wanavyoishi sasa  huku akionesha matamanio yake ya kupata mashemasi na mafrateri  watanzania wenye asili ya Asia.
Akizungumza katika kikao cha mwaka  cha mashemasi na mafrateri kilichofanyika katika Ukumbi wa Parokia ya Mbeya Mjini, Askofu Chengula amewapongeza kwa kuishi kama ndugu wamoja na wazaliwa  wa Jimbo Katoliki Mbeya  licha ya kutoka maeneo mbalimbali  ndani na nje ya Tanzania.
Katika kikao hicho cha mwaka  mashemasi na mafrateri  kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Nigeria, Benin na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pia nje ya Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania Bara na visiwani wamekuwa wakikutana  na Askofu kuzungumzia masuala ya  kimwili na kiroho.
“Ninawapongeza  mnavyoishi… kama  wote ni wazaliwa wa  Mbeya na muendelee kuwa na umoja, upendo na mshikamano huo huo kwani ninyi ni familia moja ya Yesu Kristo huku mkiendelea kumtanguliza Mungu ili  wote muweze kupitia madaraja yote matakatifu kadiri Mwenyezi Mungu atakavyopenda,”amesisitiza.
Aidha Askofu Chengula ameonesha matamanio yake  ya kupata mafrateri, mashemasi na hata mapadri raia  wa Tanzania  wenye asili ya Asia kutoka katika Jimbo lake, ”nimekuwa nikitamani sana  kupata mafrateri na mashemasi wahindi na wazungu lakini wawe wa Jimbo letu.”
Askofu Chengula amewaalika  kujiweka tayari  kwenda kufanya kazi za kichungaji katika majimbo mengine  nje ya Jimbo Mbeya na popote duniani kama walivyo mapadri  wa Jimbo ambao wanafanya kazi za kichungaji nje ya Jimbo.
“Muwe  na moyo wa utayari wa kwenda kufanya kazi  katika majimbo mengine kama kaka zenu(mapadri) kadiri ya uhitaji huku mkiondoa umimi mkiongozwa na Sala kuwa ndiyo mafuta ya safari yetu,” amesisitiza.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU