PAPA FRANSISKO AFANYA UTEUZI VATICAN


Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Askofu mkuu Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa; Rais wa Tume ya Kipapa ya Kanisa la Mungu yaani “Ecclesia Dei” Tume ya Biblia Kimataifa sanjari na Tume ya Taalimungu Kimataifa. Askofu mkuu Luis Francisko Ladaria Ferrer kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J. alizaliwa kunako tarehe 19 Aprili 1944 huko Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake kitawa na kikasisi katika Shirika la Wayesuit, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Julai 1973. Kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1994 amekuwa ni Jaalum kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko Mjini Roma. Kunako mwaka 1995 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mshauri katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Tarehe 9 Julai 2008, Papa Mstaafu Benedikto XVI akamteua kuwa Askofu mkuu na Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Tarehe 2 Agosti 2016 Papa Francisko akamteua kuwa Rais wa Tume ya Kipapa kuhusu Mashemasi Wanawake.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uamuzi wa kung’atuka kutoka madarakani uliowasilishwa kwake na Kardinali Gerhard Ludwig Muller, baada ya kuongoza kwa muda wa miaka mitano!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU