Wasomi watakiwa kuwa tiba ya ufisadi nchini

NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Simon Msanjila amewaasa wahitimu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCO) kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho kwa kupambana na kukemea rushwa na ufisadi.
Prof Msanjila ameyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati wa mahafali ya tisa ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo ambapo jumla ya wahitimu 1,583 wametunukiwa vyeti kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada za uzamili na uzamivu katika taaluma mbalimbali.
Amesema kwamba  wahitimu hao wanapaswa kuishi kwa kufuata maadili ya taaluma zao, kama ni mwalimu akawe ni mwalimu wa mfano mwema na mwanasheria akawe mwanasheria wa kweli.
“Tunafundishwa katika kitabu cha Mithali 4:6 kwamba, Usimuache Elimu, naye atakuhifadhi, umpende Elimu nae atakulinda,.Kwa vile elimu ni mwangaza na nuru kama ambavyo tunavyofundishwa kwamba pasipo na nuru kiza hutawala. Mkajikinge na vishawishi vinavyoweza kuwasababisha kupata maambukizi ya Ukimwi, mkazuie, kupambana na kukemea rushwa na ufisadi na mkawe mabalozi wazuri wa chuo kikuu cha Katoliki Ruaha,” ameasa.
Aidha amewataka wahitimu hao kutobweteka na kuridhika na kiwango cha elimu ambayo wameipata kwani dunia ya sasa ni ya ushindani mkubwa, wajenge dhana ya kutaka kujiendeleza zaidi kwani elimu haina mwisho.
“Na kwa kusema kweli Astashahada, Stashahada na shahada mtakazopewa ni changamoto katika kuendelea kujifunza daima, msibweteke na mafanikio ya leo, mkumbuke kwamba ndani na nje ya RUCU kuna fursa za kujiendeleza hata kufikia Shahada za Uzamili na Uzamivu katika taaluma zenu mbalimbali”.
Prof. Msanjila amesema serikali inavitaka vyuo vikuu vijikite na kujidhatiti kwenye fani na maeneo ambazo vina uhakika vitakuwa bora kuliko vingine.
Amevitaka vyuo vikuu viache tabia ya kujijenga kwa kuangalia tu fani au programu ambazo vitapata wanafunzi wengi ili vipate fedha nyingi kupitia ada.
“Uhakiki wa vyuo vyote uliofanyika siku za karibuni utatoa picha kwa kila chuo kama kinazingatia ubora wa elimu na kama kina uwezo wa kudahili wanafunzi waliopo chuoni, ninawashauri RUCU mjipime kuwa umahiri wenu upo kwenye fani zipi na mjiimarishe huko badala ya kutaka kutanuka kwa kuchukua kila kitu, msijaribu kuwa University of everything.” Amesema Prof. Msanjila na kuongeza kuwa “ Wakati RUCU ikijipima umahiri tambulishi wenu kama chuo (University Niche) mzingatie pia mtazamo wa serikali ya awamu ya tano inayolenga kujenga uchumi wa viwanda, hivyo wito wangu kwa chuo, katika program zake zitolewazo chuoni, haina budi kuwa na uelekeo huo.
Kabla ya kuanza kwa mahafali hayo, kulikuwa na ibada ya Misa Takatifu ambayo imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa na Homilia imetolewa na Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe huku akiwataka wahitimu hao kutumia talanta zao vizuri.
Askofu Maluma amesema wahitimu hao wanapaswa kuwa na ndoto na watamani kufanya vitu vionekane na watambue kwamba ujana wao ni mtaji wa kuanzia pale walipo ili walete faida kwao na kwa jamii nzima.
“Nyie si watalanta moja hapana, nyie ni wa talanta 2 na tano, fanyieni kazi yale yote mliyoyapata hapa, mtazaa matunda, mkilinda utu wenu mtaishi vizuri,” Amesma Askofu Maluma na kusisitiza kuwa “elimu, ujuzi na yote mliyopata mlipokuwa hapa RUCO iwafae kwenu wenyewe na muwe vyombo vinavyofaa kwa jamii na ulimwengu mzima.”

Akitoa neno kwenye mahafali hayo Askofu Ngalalekumtwa amewataka wahitimu hao kutumia muda wao vizuri chuoni hapo “mtambue ya kwamba elimu ina gharama kubwa na kama mmepata bahati ya kuwa hapa someni kwa bidii na siyo kufanya mambo yasiyofaa.”

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU