“Tuunge mkono juhudi za kanisa katoliki” Mbunge Sumbawanga


Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Aida Joseph Khenani (Chadema) ameitaka serikali, taasisi binafsi, vyama vya siasa na mtu mmoja mmoja kuunga mkono juhudi za kanisa katoliki mkoani Rukwa katika kuboresha misingi ya elimu na maendeleo ya kitaaluma katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Aida ameyasema hayo katika mahafali ya kuhitimu elimu ya chekechea kwa wanafunzi wa shule ya  Familia Takatifu yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa parokia ya Familia Takatifu jimboni Sumbawanga.

“Nalipongeza sana kanisa Katoliki mkoa wa Rukwa kwa kujali na kuthamini watu wenye mahitaji mbalimbali katika jamii kikiwemo kituo cha watoto yatima cha Mt. Martin De Pores Katandala ambacho ni ukombozi kwa yatima mkoani Rukwa, kusaidia kujenga shule maalumu ya msingi ya wasioona Malangali ambapo pia kwa sasa ni kituo cha kulelea ndugu zetu walemavu wa ngozi yaani Albino, kuanzisha huduma za elimu ya chekechea hata kwa watoto walemavu kupitia kituo cha chekechea cha Familia Takatifu,” amesema mbunge huyo.

“Kanisa linaona mbali na ndio maana katika masuala ya msingi kama hili la elimu, tudumishe taaluma ya watoto wetu na si kuingiza siasa katika vitu vya msingi. Nadhani serikali,taasisi zingine, makampuni na watu binafsi tuunge mkono juhudi hizi kwa nguvu zote,
‘ ameongeza.

Kwa kutambua mchango mkubwa wa kanisa katoliki katika maendeleo ya jamii nchini na kwa kujali walemavu, Mheshimiwa Aida Khenan ametoa mchango wa shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa miundombinu wa madarasa na vifaa vya kujifunzia kwa watoto wa chekechea wenye ulemavu ambao wataanza kujiandikisha katika mhula wa masomo wa mwaka 2017.

Akitoa mchango huo Aida amesema kuwa serikali inatakiwa kuandaa mpango maalumu wa kutokomeza unyanyapaa kwa walemavu kwa kuwajengea misingi bora ya elimu kuanzia chekechea hadi vyuo kama ilivyo kwa wasio na ulemavu

Akimshukuru mgeni rasmi kwa mchango huo mkuu wa shule hiyo ya ckekechea ya Familia Takatifu Sr. Rose Kindimba amesema kuwa wameamua kuanzisha huduma ya kupokea watoto wenye ulemavu mbalimbali shuleni hapo ili kuwajengea misingi kama ilivyo kwa wasio na ulemavu na kuwaomba  wazazi  kutowanyanyasa watoto wao kwa kuwanyima elimu na kuwaficha kwa kuogopa aibu suala ambalo linawanyima fursa za kujiendeleza kupata ujuzi na kujitegemea kama ilivyo kwa watu wengine.

“Tunao walemavu katika familia zetu, katika jamii zetu, taifa na hata dunia nzima ambao wanahitaji msaada wetu. Lakini tukumbuke kuwa ulemavu hauna cha tajiri wala maskini, bosi wala kibarua, hauna kabila wala rangi siyo wa wazungu tu au waafrika pekee isipokuwa Mungu amewaweka wenzetu kati yetu ili tutambue ukuu wa uumbaji wake, nasi tumeona tufanye maboresho kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kujifunzia watoto wenye ulemavu”. Amesema Sr. Rose.
Kituo hicho cha chekechea kimeanza mwaka 1999 na kimekuwa kikipokea watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitatu kwa ajili ya kuwaandaa kwa masomo ya shule ya msingi.



Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU