WARAKA MZITO WA BABA ASKOFU SEVERINE NIWEMUGIZI KWA WATANZANIA HUU HAPA..



Heri ya Krismasi!

Tunaadhimisha sherehe za kuzaliwa Bwana Yesu Kristo mwaka huu 2016 kukiwa na hisia na mitazamo mbali mbali ya watu wa makundi tofauti katika jamii yetu, juu ya hali ya maisha ya mtanzania leo. Hii ni hasa baada ya kusikia toka kwa watu mbali mbali tathmini za hali halisi ilivyo mijini na vijijini. Licha ya tetemeko la ardhi lililotikisa huku Kagera mwezi Septemba na njaa pia katika baadhi ya wilaya mkoani Kagera, baadhi ya watumishi wa umma hasa waliozoea kufanya kazi kwa mazoea na bila kuzingatia nidhamu na maadili ya utumishi wao wameishi kwa hati hati wasijue kutumbuliwa kwao kutakuwa lini na tokea wapi! Wafanya biashara nao biashara zao zimepiga miayo kwa sababu ya kutochanganya kama ilivyozoeleka huko nyuma, wengi wanasema hali ni ngumu, pesa haikamatiki! Viongozi wa makanisa nasi tumejikuta tukikimbizana na viongozi wa serikali kuulizana nao kama ubia wa sera ya PPP (Public-Private-Partnership) bado unaishi au la. Milango yao na masikio havikufunguliwa kwa urahisi. Mahospitali yetu yako taabani hasa kwa suala la watumishi, karibu yaende ICU licha ya makubaliano mazuri baina ya serikali, makanisa na wadau wengine binafsi katika huduma za afya yaliyopo kwenye makaratasi.



Nimefika kwa kinyozi wangu nikamuuliza: vipi hali? Akajibu kuwa hali ni ngumu sana, waliozoea kuleta familia kunyoa kwake mara kwa mara hawaendi tena kwani hawana pesa, karibu anafunga kazi hiyo; naye ameapa kura ikipigwa tena atafikiria mara mbili nani wa kumpa kura yake. Upo mzaha sasa kuwa sote tuko tunaisoma namba kwa jinsi nchi inavyoendeshwa kwa kasi, anayeshika usukani akiwaacha njiani hata wa ndani wake! Wengine wanapumua kama vifaru waliojeruhiwa. Na mwandishi wa habari mmoja ameniuliza nina neno gani la faraja kama mchungaji kwa wote hawa Krismasi hii? Nikamjibu kuwa wasiwe na hofu, Yesu amekuja, ni Mungu pamoja nasi. Wakiwa naye huyu basi mengine yote si kitu! Akachangamka kwa neno hilo naye.



Mwandishi wa habari mwingine akanichokoza akiuliza mimi naona changamoto gani nchini kwa sasa ambazo Kristo amekuja kupambana nazo? Nimemjibu kuwa bila shaka zipo nyingi duniani na hapa nchini kwetu. Zipo za kiuchumi, za kisiasa, za kijamii, na za kidini. Mzunguko wa pesa umekuwa mgumu, mifuko ya wengi iko tupu. Walikuwapo watu kadhaa waliozoea kuzipata kifisadi na kuzimwaga katika mzunguko. Kufungwa kwa mifereji iliyosaidia kuzipata kumeathiri wengi. Hata mama Ntilie anaonja kibano hicho! Kisiasa kuna aina fulani ya mnyauko au kupooza kwa shughuli za kisiasa, hili mnalifahamu kwa mapana sababu zake; kijamii tunashuhudia kila siku mapambano ya wafugaji na wakulima pande mbali mbali za nchi; kuna watu kuporwa ardhi; ukatili wa kijinsia; shida za maji vijijini; ugumu wa malezi ya watoto waitwao wa dijitali; watanzania wengi maskini kutokuwa na bima ya afya, nk. Kidini, ni dini na makanisa yanayoahidi kuleta utajiri, kutenda miujiza, kuponya magonjwa na kuondoa kero zote za maisha mara moja na kutoa burudani za nyimbo za Injili ndizo zinazong’ara na kufuatwa na wengi, tofauti na makanisa yale yanayokazia kuabudu kwa moyo (Mt 15:8; Lk 21:34; Yn 4:23; Efe 6:6; Kol 3:23), heri nane (Mt 5:3-12), kujitahidi kuingia mbinguni kupitia njia nyembamba (Mt 7:3), kujikana, kubeba msalaba na kumfuata Bwana (Mt 16:24; Lk 9:23). Watu wengi wanataka njia pana na isiyo na shida au msalaba! Kwa changamoto zote hizi Kristo aliyezaliwa ulimwenguni ndiye jibu! Mtu anaweza kuniuliza kwa vipi? Ukweli ni kuwa kama wanadamu wakimsikiliza kwa makini Yesu na kwa makini wakafuata ushauri wake changamoto zote zitapata majibu sahihi au suluhu ya kudumu!



Kwetu huku Ngara na kuelekea Biharamulo nimesema changamoto kubwa ni UHARIBIFU WA MAZINGIRA. Hakuna aliye na huruma na sisi: mazingira yanaharibiwa kwa kasi ya ajabu kwa kukata miti na kuchoma mkaa kwa namna ya kutisha mbele ya macho ya viongozi wetu. Kisingizio ni kuwa hakuna nishati mbadala! Vyanzo vingi vya maji vimekauka kutokana na hujuma hii ya kibinadamu; tuna ng’ombe wilayani Ngara huenda wengi kuliko sehemu yoyote Tanzania ingawa eneo la wilaya ni dogo huenda kuliko wilaya zote nchini. Hatuwezi kupona jangwa na mmomonyoko wa ardhi. Tumelia na kupiga kelele lakini hakuna anayetuhurumia. Uharibifu umehalalishwa, maana ulisikia wanaokamata ng’ombe kwenye hifadhi za Burigi wanasimamishwa kazi! Barabara ninayopita nitake nisitake kama mchungaji kwenda kwenye parokia zangu za Biharamulo inatisha kwa uharibifu. Magari makubwa yanaanguka yakijaribu kupita pembeni mwa barabara kwa kukwepa kupita juu ya lami yenye mashimo kama mapango. Barabara ya Nyakanazi-Lusahunga-Rusumo inatisha, ingawa ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hii ukizingatia bidhaa za thamani kubwa zinazopitishwa humo kwenda Burundi, Rwanda, DRC na hata Uganda! Mbaya zaidi sasa mazingira yanachafuliwa kwa marundo ya chupa zilizovunjika, zikimwagwa pembeni mwa barabara usiku na magari makubwa yasiyofahamika! Ukitaka naweza kukutumia picha za hali hii ninayoizungumzia. Usalama wetu na mali zetu Ngara daima ni tete hasa kutokana na kupakana na nchi jirani zenye migogoro ya ndani isiyoisha. Uumbaji wa Mungu unalia, nasi tunalia, lakini machozi yetu ni kama ya samaki majini, hakuna anayetusikia wala kutuhurumia. Sisi wafuasi wa Kristu tunabaki kusema tu NJOO KWETU MASIHA utuokoe na uharibifu huu na hofu zetu.



Ni matarajio yangu kuwa ujio wa Kristu utagusa mioyo ya wahusika wote, awazibue masikio wasikie kilio, awafumbue macho waone, awape moyo wa huruma wauonee huruma uumbaji wa Mungu ulioharibiwa sana; Neno lake liwachome sindano wahalifu ili kutibu dhamiri zao; viongozi nao waone aibu kwa kukaa kimya au kuona uharibifu unaotendeka kama vile ni mambo ya kawaida, au kama vile hakuna la kufanya ili kunusuru mazingira yetu. Kilichofanyika kwa misitu tokea Nyakahura ngazi Saba, Busiri hadi Lusahunga wilayani Biharamulo ni maafa kwa mazingira! Sote tunashuhudia mabadiliko ya tabia nchi na madhara yake kwa hali ya hewa na bado tunawachekea tu waharibifu wa mazingira!



Paulo Mtume kupitia Waraka kwa Tito  (2:11-14) ametuambia katika mkesha wa Noeli kuwa neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu imefunuliwa kwetu. Yesu Kristo ndiye neema hiyo. Amekuja kutufundisha kuukataa uovu na tamaa za kidunia, ili tuishi kwa kiasi, haki na usawa. Kuharibu mazingira kwa kisingizio chochote kile ni uovu usiopaswa kukubalika wala kuvumilika. Kuna wenzetu ni wakulima wazuri sana wa mpunga, lakini ni adui wa miti ati kwa sababu miti inawapokea ndege wanaokula mazao yao. Shida ni kuwa wao ni wepesi wa kuhama inapotokea maeneo kuharibika kwa sababu ya kazi za kibinadamu zinazoleta ukame. Wanahama na kwenda kwingineko na kuendelea na uharibifu ule ule! Nawasihi wabadilike na kuwa rafiki wa mazingira. Wajue kama wao wanavyohitaji kuhifadhiwa maisha yao, vivyo hivyo mazingira yanahitaji kuhifadhiwa ili nayo yamhifadhi binadamu. Uumbaji wa Mungu nao unahitaji ukombozi. Paulo mtume analieleza hili vizuri akisema “kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu; kwa maana viumbe vyote  pia vilitiishwa  chini ya ubatili…viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu” (Rum 8:19-21). Tumefunga mwaka wa Yubilei ya huruma ya Mungu tarehe 20 mwezi Novemba , lakini sasa ni fursa ya kuendelea kudhihirisha upendo na huruma kwa watu na mazingira yetu pia.



Emmanueli, Mungu pamoja nasi atubadilishe mioyo yetu itake kutenda mema daima. Yesu Kristu ni mwanga ulioingia ulimwenguni kufukuza giza. Hata jua linapotua yeye anabaki akiangaza akili na mioyo. Ndiyo maana yeye ndiye tumaini pekee ulimwengu unaweza kutegemea. Licha ya changamoto nyingi zinazoweza kumtatiza mwanadamu, akiwa na imani katika Kristo Yesu anaweza kutembea mbele akiwa na matumaini kwamba hatimaye atashinda yote magumu. Kristo amekuja ili atushike mkono na tutembee kumwelekea Mungu atoaye uzima wa milele mwisho wa safari. Ukidumu mikononi mwake Yesu una uhakika wa kufika kwa Mungu. Hii ni hata kwa asiye Mkristo. Mfano mzuri ni kiongozi mkubwa wa India Mahatma Gandhi muumini wa dini ya Kihindu aliyewahi kusema kwamba “Yesu Kristo ni mmoja wa walimu wakubwa binadamu amewahi kupata”.



Gandhi alimtambua Yesu kuwa ni mwana wa Mungu katika maana kuwa ni katika maisha yake Yesu kuna ufunguo wa ukaribu wake na Mungu, na kwamba Yesu alieleza roho na mapenzi ya Mungu kuliko mtu mwingine yeyote angeweza! Alikiri kuwa Yesu hakuhubiri dini mpya bali maisha mapya, akiwaalika watu kutubu. Gandhi alikiri kuwa Yesu alileta sheria mpya: “Amri yangu ndiyo hii, mpendane kama nilivyowapenda ninyi” (Yn 15:12). Pia alikiri kuwa Kristo alimpa funzo kubwa kwamba ukweli ndiyo jambo la msingi la kwanza kutafuta maishani: “tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru” (Yn 8:32). Lakini pia alimfunza kujitoa bila kujibakiza pasipo kutegemea kurudishiwa chochote. Haya ni mambo ambayo mtu yeyote bila kujali dini au kanisa ujifunze kwa Yesu Kristo. Kwako wewe Mkristo naamini shuhuda huyu asiye Mkristo lakini shabiki wake Kristo anakufumbua macho zaidi utambue ni nani uliye naye maishani. Hivyo imarisha kumpenda zaidi, kumthamini na kuzingatia atakayokufundisha mtoto Yesu.



Kuzaliwa kwa Kristo kuna maana gani kwangu na kwako leo? Kuzaliwa kwa Yesu kuna maana kuwa: 1)Uzazi wa Yesu umetimiza maaguzi ya manabii: kwamba ulikuwa mpango wa Mungu, hivyo uzazi wake ulikuwa wa kimungu; 2)Mrithi wa kiti cha Ufalme wa Daudi amezaliwa (Lk 1:32-33); 3)Furaha imeingia duniani (Lk 2:14,20,25-32): wachungaji walifurahi; mzee Simeoni naye alifurahi kuona wokovu umefika; 4)Mwokozi amefika atakayelipa fidia ya wokovu wa binadamu (Mk 10:45; Lk 1:21; 19:1-10); 5)Shetani atashindwa (Mwa 3:15; 1 Yoh 3:8; Ebr 2:14). Matokeo ya kushindwa shetani ni: 6) Amani inaweza kuingia mioyoni mwetu (Isa 9:6-7; Lk 2:14; Kol 2:19-20); 7)Njia ya kuingia mbinguni imewekwa wazi (Yn 3:16, kila amwaminiye hatapotea; 14:5-6, Yeye ndiye njia, ukweli na uzima). 8)Hatimaye Yesu atarudi tena katika utukufu i)kutukaribisha kwake (Yn 14); ii)kufufua wafu (1 Thes 4:13-18); iii)kubatilisha mauti (1 Kor 15:25-26); iv)kukusanya wateule wake (Mt 24:31); v)kuhukumu ulimwengu (Mt 25:31-46) na vi)kuwatuza waaminifu wake: kila mtu kulipwa kadri ya matendo yake (Mt 16:27). Nikijua maana hii ya kuzaliwa Yesu Kristo napata ujasiri wa kumpokea na kuwa tayari kumfuata, nikiomba anishike mkono katika safari ya kwenda kwa Baba. Najawa furaha, amani na nguvu ya kuishi kwa matumaini. Nakusihi nawe usipoteze fursa hii.



Amani ya Bwana iwe nawe leo na daima. Amina.



+Severine NIWEMUGIZI

Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU