‘Ukristo umekomesha utumwa na ujinga Tanzania’ Ask. Lebulu

IMEELEZWA kuwa ujio wa Wamisonari walioleta ukristo Tanzania Bara miaka 150 iliyopita, uliwezesha mapambano dhidi ya biashara ya utumwa, ujinga, umasikini na maradhi.
Hayo yameelezwa na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu, katika mahojiano maalum na Kiongozi, miezi miwili baada ya uzinduzi wa Yubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, na miaka 100 ya upadri.
Akielezea huduma za Kanisa katika kipindi cha miaka 150 ya uinjilishaji, Askofu Lebulu amesema kuwa wamisionari hawakuishia tu katika kuinjilisha, bali walijikita katika kuendeleza hadhi ya mwanadamu mzima, kiroho na kimwili.
“Ukristo unaelekeza kutambua hadhi ya ubinadamu, hivyo pamoja na kufanya shughuli za uinjilishaji, wamisionari walipinga biashara ya utumwa, ili kulinda hadhi ya ubinadamu” ameeleza.
Aidha Askofu Lebulu amebeinisha kuwa Kanisa la Tanzania limefanikiwa kuwa taasisi inayosaidia watu katika uinjilishaji kimwili na kiroho, kupitia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya, elimu na miradi ya maendeleo.
Ameeleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka 150 Kanisa limekomaa, na hii imedhihirisha uwepo na utendaji wa Kristo mfufuka Tanzania Bara na Afrika. Amesema kuwa Huruma ya Mungu ndiyo iliyowawezesha wamisionari kuwafikia watu wengi, hadi Tanzania na kuwa msaada kwa watu wenye shida.
“Tunapoadhimisha miaka 150 ya ukristo, tunashuhudia ukomavu wa kanisa, yaani uwepo wake Kristo katika ngazi mbalimbali, kuanzia kwenye familia, jumuiya ndogo ndogo, parokia hadi majimbo” amesema.
Amewaasa waamini kujitoa katika kulitegemeza kanisa ili kazi ya umisionari iendelee. Amesema kuwa Kanisa ambalo halijitegemei kifikra, kihuduma na kiuchumi ni fukara.

“Waamini ni kiini cha kufaulu kwa Kanisa, waamini ndiyo kanisa na sehemu ya msingi katika kanisa. Kulitegemeza kanisa siyo mzigo, ni jukumu letu” ameasa.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU