KAULI: WOTE TUILINDE AMANI YETU


Taifa letu linatimiza miaka 55 tangu tupate uhuru kutoka kwa mkoloni mwingereza. Mara nyingi siku kama hizi huwa siyo za mchezo ama ‘kispotispoti’ kama vijana wa sasa wanavyoita siku hizi. Mataifa mengi, likiwemo letu pendwa siku kama hii huitumia kuangalia wapi limetoka na wapi linakwenda. Kumbukumbu hizi mara nyingi huwarudisha wananchi kwenye jasho, damu, machozi na zaidi FURAHA. Na ndiyo maana siku hii huwa ni ya mapumziko. Ni siku muhimu pia kwa nchi kutuma ujumbe kwa nchi zingine, uwezo kiulinzi na usalama pia maendeleo.
Ndiyo maana hata unapotimiza umri fulani basi mara nyingi utafanya sherehe kidogo kufurahia kufikisha idadi Fulani ya miaka. Siku hii huchagizwa na mapochopocho ya hapa na pale, keki, shampeni, vyakula mbalimbali na vinywaji na kuimbiwa juu, wengine siku hizi humwagiana ndoo za maji, kikubwa KUFURAHI. Kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu kwa kufikisha umri huo na pengine akuongezee zaidi huwa ni jambo la msingi kuzidi mengine.
Si hivyo tu, bali mataifa mengine licha ya kutuma wawakilishi walau waje washuhudie shamrashamra za kusherehea uhuru, huja kwa lengo la kujifunza mambo kadhaa yakiwemo ya kimaendeleo, ili yafanyike pia nchini mwao.
Yapo mengi ya kujivunia sisi kama watanzania mpaka kufikia miaka 55. Moja kati ya mambo hayo ni taifa kuendelea kuwa na AMANI NA UTULIVU. Siyo siri kwamba kila kukicha ufunguapo luninga, redio ama kusoma magazeti na mitandao kadhaa, utakutana na migogoro katika mataifa kadhaa na kushuhudia madhara ya migogoro hiyo. Mauaji, ubakaji, wizi, uharibifu wa miundombinu, hofu, majonzi na maumivu vyote huonekana waziwazi.
Ni vyema kila mtanzania akahakikisha hali hii waliyoiasisi viongozi wa taifa hili hayati Mwalimu J.K.Nyerere na hayati Sheikh Abeid Amani Karume inaendelea kulindwa na kudumishwa kwa hali yoyote ile.
Hakuna unafuu wowote yanapotokea machafuko, hata kuyatibu makovu yatokanayo na machafuko kuyatibu siyo kazi ndogo hata kidogo. Zipo nchi zimeingia katika migogoro takribani miaka 50 iliyopita lakini licha ya kurejesha amani, bado makovu ya migogoro hiyo yapo. Wahenga walisema kinga ni bora kuliko tiba, hima watanzania tuungane katika kuilinda amani tuliyonayo.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU WABARIKI WATANZANIA.









Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU