DESEMBA 9 RASMI SIKU YA KULIOMBEA TAIFA....

KUFUATIA kutolewa kwa kibali kutoka kwa Baba Mtakatifu, Desemba 9 ya mwaka 2016 na ya kila mwaka, ambayo ni kumbukumbu ya siku ya uhuru wa Tanganyika,  imeidhinishwa kuwa ni siku maalum ya kufanya Misa Takatifu ya kuliombea Taifa la Tanzania.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba, ambaye ametoa rai kwa waamini nchini kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kusali kujiombea wenyewe na kuiombea Tanzania na viongozi wake.
“Kuanzia Desemba 9 ya mwaka huu na kuendelea, tutaanza kufanya Ibada maalum ya kuliombea Taifa letu. Tutakuwa na Misa Takatifu ambayo imeratibiwa rasmi kwa kibali cha Baba Mtakatifu, kwa ajili ya kuliombea Taifa letu lililowekwa chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria. Hivyo nitoe wito kwa waamini, tukutane makanisani tusali, kujiombea sisi wenyewe na Taifa letu. Tuanze adhimisho hili kwa sala” ameeleza Padri Saba.
Akielezea sababu za kuchaguliwa kwa Desemba 9 kuwa siku ya kuombea Taifa, siku ambayo ni kumbukumbu ya uhuru wa Tanganyika, Padri Saba amesema kuwa mara baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII aliandika sala kwa ajili ya kuliombea Taifa la Tanzania  na alilikabidhi Taifa hilo chini ya ulinzi wa Bikira Maria.
“Na ikumbukwe kuwa mwaka 1984 Papa Yohane Paulo II alitoa hati maalum kwa ajili ya Kanisa la Tanzania, kwamba linaweza siku hiyo ya Desemba 9, tunapofanya kumbukumbu ya uhuru wetu, tufanye adhimisho kwa heshima ya Mama Maria ambaye amewekwa kuwa mlinzi wa Taifa letu” amesema.
Aidha ameongeza kuwa kwa hati hiyo ya mwaka 1984 Baba Mtakatifu ameipatia Tanzania uwezo na mamlaka ya kuwa na Ibada maalum ya Misa Takatifu ya Masifu kwa ajili ya heshima ya Mama Bikira Maria, mlinzi na msimamizi wa Taifa la Tanzania.
Kufuatia taarifa hiyo, Padri Saba ametoa rai kwa wakristo wakatoliki, kila mara kumkimbilia Mama Maria ili aweze kuilinda Tanzania na kuiepusha na laana na balaa zinazoweza kuikabili.
Pia amewaasa watanzania kutumia fursa hiyo kuwaombea viongozi wa serikali, vyama na wa dini ili wadumu katika kutenda haki na kumthamini kila mtu.
 “Tuwaombee viongozi wetu wawe na hekima, busara na upendo. Kila aliye kiongozi, awe wa serikali, vyama na dini, adumu katika misingi ya haki inayojenga amani” ameongeza.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU