Kanisa Katoliki latathmini hali ya uchumi nchini


Wachumi waombwa kutoa takwimu zenye uhalisia
Wadau wataka uchumi unaojali masikini na mazingira

IMEELEZWA kuwa ukuaji wa uchumi usiojali uhifadhi wa mazingira, maliasili na utu wa kila mwananchi ni pigo ambalo haliakisi uhalisia wa ukuaji huo.
Hayo yamebainishwa na wadau wa masuala ya uchumi na mazingira katika Kongamano la kitaaluma la siku mbili, lililojadili juu ‘Mchango wa mafundisho jamii ya Kanisa Katoliki katika kukua kwa uchumi na maendeleo ya jamii’ lililofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris Mtwara.
Akitoa mada katika Kongamano hilo Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, amesema kuwa kukua kwa uchumi ni lazima kuendane na ari ya kutunza mazingira, matumizi ya rasilimali yenye kujali na kuheshimu mpango wa Mungu wa uumbaji na moyo wa kugawana sawa mapato yatokanayo na rasilimali hizo.
“Ili kuwa na uchumi wenye tija na maendeleo endelevu, ni lazima tutoke kwenye dhana ya kusema ‘nini ninataka’ na kujikita katika dhana ya ‘nini Mungu anataka’. Vinginevyo tujiandae kulipa deni la kuharibu Ekolojia, na kusababisha utu wa mwanadamu ukose maana” ameeleza Askofu Nyaisonga, ambaye kitaaluma ni mwana Jiografia.
Aidha Askofu Nyaisonga amebainisha kuwa kutoweka kwa wanyama na mimea ya asili huchangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji usio na tija, na kusababisha uchafuzi wa mazingira, ambo ni dhambi dhidi ya asili. Amewataka wadau wa maendeleo, wachumi na watanzania kwa ujumla kubadili mtazamo wao dhidi ya mazingira, kwa kuyachukulia mazingira kama ndugu.
“Kama wakristo, tumeipokea dunia kama Sakramenti ya Ushirika, ambayo tunapaswa kushirikishwa na Mungu na vizazi vijavyo. Hivyo, tunapaswa kubadili mtazamo wetu dhidi ya mazingira. Tuyaone mazingira kama kaka au dada yetu. Uzuri wa mazingira humdhihirisha aliyeyaumba” ameeleza.
Kwa upande wake mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza (SAUT), ameeleza kuwa takwimu za kukua kwa uchumi hazina uhalisia kwa kuwa hazijumuishi uharibifu wa hali ya juu unaofanywa na shughuli za uzalishaji.
Ameongeza kuwa ukuaji wa uchumi unaowaacha nyuma maskini na wanawake hauna uhalisia, na hivyo kuwataka wanaotoa takwimu za kukua kwa uchumi kujumuisha athari za mazingira zinazoletwa na kukua kwa uchumi.
“Uchumi wetu unakua sana kwa kuwa kiwango cha uharibifu kiko juu pia. Uchumi unakua kwa kasi kwa sababu tunatumia mno rasilimali zetu. Lakini tumewahi kujiuliza gharama za uharibifu tunaoufanya kwenye mazingira yetu? Tumejiuliza gharama za matatizo tunayoyazalisha kwa watu wengi ambao wengi wao ni maskini? Kama hatuangalii gharama hizi basi kipimo chetu cha kukua kwa uchumi siyo sahihi” ameeleza.
Ameongeza kuwa kukua kwa uchumi hakuzingatii mahitaji ya vizazi vijavyo, na kuonya kuwa uharibifu wa rasilimali utaleta hatari na balaa. Pia ametoa angalizo kuwa kazi ya mwanadamu ni kuwa waangalizi wa rasilimali kwa ajili ya manufaa ya vizazi vingine.
Akitoa mchango wake katika kongamano hilo mdau wa mazingira na Balozi Mstaafu John Kambona amesema kuwa elimu ya utunzaji wa mazingira inapaswa kuwekwa kwenye mtaala wa elimu, ili iwe sehemu ya utamaduni wa mtanzania.
 “Somo hili likiwekwa kwenye mtaala litawainua watoto wetu kuliko kuwafundisha ‘pie’. Pia liwekwe kwenye sala ili itukumbushe kuwa kukata miti ni dhambi” amesema.

Kongamano hilo la kitaaluma limehudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, Askofu Bruno Ngonyaji wa Jimbo Katoliki Lindi, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Raymond Saba, Makamu Mkuu wa Chuo Stella Maris Mtwara Padri Charles Kitima. Wengine ni mtafiti kutoka REPOA Dkt. Blandina Kilama, mwakilishi wa Shirika la CRS ndugu Julius Marwa, wahadhiri, wanachuo na jumuiya ya Stella Maris Mtwara.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU