‘Jamii isiyowajibika chanzo cha mmomonyoko wa maadili’

IMEELEZWA kuwa kukithiri kwa vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili nchini kunachangiwa na kutowajibika kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, alipokua anaongea na watoto waliopo katika mahabusu ya watoto Upanga jijini Dar es salaam, kabla ya kutoa zawadi za Krismas, zilizotokana na michango ya Watoto wa Shirika la Kimisonari la Utoto Mtakatifu, Dekania ya Mtakatifu Yosefu.
Askofu Nzigilwa amesema kuwa kitendo cha watoto kuwa mahabusu au gerezani na kukithiri kwa watoto wa mitaani, ni ishara kuwa kuna watu wazima, iwe wazazi, walezi au jamii, haijawajibika, jambo linalopaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Kuna picha iliyojengeka kwa watu wengi ambayo siyo sahihi kuwa watu waliofungwa siyo wema. Picha hii haina uhalisia, huko mtaani kuna watu wengi ambao wanatenda uovu kila kukicha. Kwa uwepo wenu hapa wanaopaswa kulaumiwa siyo ninyi, bali kuna watu wazima hawajawajibika” ameeleza.
Aidha Askofu Nzigilwa amesema kuwa utoaji wa zawadi hizo za Krismas uliofanywa na watoto wa kipapa, umetokana na malezi wanayopatiwa watoto hao ya kumpenda Mungu na jirani, hasa wenye mahitaji na waliozuiliwa.
“Zawadi hizi ni ukarimu wa hawa watoto, siyo sisi maaskofu au wazazi wao. Kazi yetu sisi ni kuwalea ili wawe na moyo wa kujitoa. Hivyo nawapongeza watoto hawa ambao hufanya matendo haya ya upendo kila mwaka, nah ii leo wamejigawa katika makundi na wametembele sehemu 6” ameongeza.
Katika hatua nyingine Askofu Nzigilwa ameagiza kufanyika kwa tathmini na upembuzi yakinifu ili kuona uwezekano wa kuchimba kisima kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji, ambayo inakabili mahabusu hiyo kwa muda mrefu.
Askofu Nzigilwa amemuagiza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Mtakatifu Maurus Kurasini, Bwana Melkiori Ngonyani, kushirikiana na uongozi wa mahabusu hiyo katika kufanya tathmini ya awali, na iwapo watabaini uwepo wa maji chini ya ardhi, waamini watahamasishwa kuchangia ili kumaliza changamoto hiyo.
“Mshirikiane katika kupima tuone kama kuna maji, baada ya hapo tutawaomba waamini na nina uhakika watachangia na kumaliza kabisa changamoto hii ya maji. Hivyo kuhusu suala la changamoto ya maji naomba hilo tulibebe sisi” amesema.
Awali akielezea changamoto zinazoikabili mahabusu hiyo, Afisa Mfawidhi wa Mahabusu hiyo Ramadhan Yahaya amesema kuwa baadhi ya kero zinazohitaji kupatiwa suluhisho ni ukosefu wa dawa na upungufu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

“Tangu nimekuja kituo hiki miaka mitatu iliyopita, kituo kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji. Tunadaiwa bili kubwa zaidi ya Sh. Milioni 5, hadi kupelekea kukatiwa huduma ya maji” ameeleza Bwana Yahaya.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU