Askofu Ngalalekumtwa awataka waamini kuwaombea Mapadri



ASKOFU wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amezindua mwaka wa Jubilei ya miaka 100 ya mapadri wazalendo na kuwataka waamini kuendelea kuwaombea mapadri popote walipo.
Uzinduzi wa jubilei hiyo umefanyika kwenye kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Kihesa kwa  kuwashwa kwa mshumaa mara baada ya Askofu Ngalalekumtwa kumaliza kutoa daraja la ushemasi kwa mafrateli Jerome Mtatifikolo wa parokia ya Ilole na Jerome Mponzi wa parokia ya Nyakipambo.
Akitoa homilia kwenye misa hiyo Mhashamu Ngalalekumtwa amesema kwamba, sambamba na utoaji wa daraja hilo lakini pia waamini wanatakiwa kuwaombea viongozi wa Serikali ili waweze kutenda kazi zao kiuaminifu.
Mhashamu Ngalalekumtwa amesema Kristo ndiye mfalme wa amani, kwa hiyo wanapokumbuka hayo katika historia kuuawa kwa watoto wadogo tena wasio na hatia wamuombe Kristo ili aweze kuratibu kwa wale wanaosimamia maslahi ya ulimwengu kusudi hawa watawala wawajibike ipasavyo.
“Leo ni siku ya kuwaombea wote kuanzia rais John Pombe Magufuli na utawala  wake na wote walio kama yeye   tuwaombee kusudi wawajibike ipasavyo waelewe kwamba hawapo pale kwa  ajili ya kuongeza dola  kwenye akaunti zao au mitungi yao bali wapo pale kusudi wongeze raha, amani na ustawi wa maisha yao, maana kuna maelekeo ya kujisahau, akina Herode tumekuwa nao wengi wa kutosha,” amesema Mhashamu Ngalalekumtwa
Aidha amesema kuwa Mungu amewapatia  zawadi ya mashemasi ili waweze  kuwa wahudumu katika ngazi ya ushemasi na imetokea tu wote ni akina Jerome, imetokea tu sasa katika mapokeo na mfumo wa kanisa, mashemasi ni watumishi, mawakili wasimamizi, walinzi na watunzaji wa familia ya Mungu wakiwa wasaidizi wa Maaskofu wao na pia mapadri.
“Ili kazi hiyo ifanyike na ilete baraka na izae matunda, Paulo anasema kwamba Mashemasi wawe na wastahimilivu si watu wa kauli mbili au kutumia mvinyo sana, si watu wa kutamani fedha ya aibu, wanapoingia huku si kwamba nawaajiri, hawa wanaajiriwa na nyie waamini, muwatunze hawa mashemasi, mapdri na masista, lakini wao kama wao wasiwe kama watu wa kutamani fedha ya aibu.
Wawe watu wasafi, waandamane na Kristo ambaye kazi yake ni kutakatifuza, kuwatunza watu, wawe watu wa Mungu, Mungu awakubali na nyie pia muwakubali.”
“Daraja wanalopewa leo ni la mpito, wapo kwenye safari ya kuendea ukuhani (upadri), wanapitia huku ili waweze kujua nini maana ya kuwa watumishi wa watu, tuwaombee wawe na mwenendo safi kwa wote, ili kukutana wao iwe mwanzo wa baraka, tunawaombea wawe watu wa sala na vitendea kazi tumewapatia, vitabu ambavyo vina sala maalumu ya kanisa.
Watabatiza, watatangaza injili watafungisha ndoa, watazika wafu, watu watakuja kuomba ushauri kwenu, watu wajifunze kwenu, maisha yenu yawe mfano bora kwa wengine, watu wajifunze kwenu maana ya kuwa wafuasi wa Kristo, shikeni kiaminifu maisha ya useja kwa sababu yule ambaye anataka muendeleze kazi yake alikuwa mseja Krito, ndiyo maana kanisa Katoliki linabaki na msimamo huo na usafi huo wa ubikira, muige mfano wa Kristo mwenyewe.”

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU