Maaskofu watoa angalizo kuhusu mwelekeo wa nchi

·      Wahimiza utawala wa sheria, haki, amani na uwajibikaji

·      Watahadharisha kukithiri kwa uharibifu wa mazingira

KATIKA kusherehekea Sikukuu ya Noeli nchini, baadhi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania wamewataka watanzania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, na kuachana na matendo ya giza yanayosababisha rushwa, ufisadi na utendaji wa kazi unaofanywa kwa mazoea.
Akitoa homilia yake katika Misa ya Krismasi ndani ya Kanisa la Bikira Maria wa Fatima lililopo Geita, Askofu Flavian Kassala wa Jimbo Katoliki Geita amesema kuwa kila mtanzania anapaswa ajione kuwa ni chanzo cha amani.

Askofu Kassala ameonya kuwa  kisiwepo kisingizio chochote kwa mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi ambayo imekuwa zawadi kubwa na ya kipekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ametoa mfano wa nchi zilizo katika vita, ambako watu wanavyoishi kwa shida kubwa huku maelfu ya watu wakipoteza maisha, na hivyo akatoa wito kila mtu kuhakikisha anakuwa chanzo cha amani kuanzia ngazi ya familia.

Aidha Askofu Kassala amewahimiza wazazi wote katika familia zao kuwa chanzo cha habari njema ili watu wauige mwenendo mwema, na hatimaye  familia zao zibaki daima katika amani ambayo ni zawadi kubwa inayoletwa na Kristo anayezaliwa kama mfalme wa amani.

Askofu Shao aonya wanaopinga mapambano dhidi ya rushwa
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar Mhashamu Agustino Shao amewaonya watu wenye nia ya kukwamisha jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ambayo inapambana na  vitendo vya rushwa na ufisadi, ili kuiwezesha nchi kufikia maendeleo endelevu yenye tija kwa kila mtanzania.
Aidha amesema kuwa jambo la msingi kwa Serikali ni kujikita katika utawala wa sheria, kuzingatia haki, amani na uwajibikaji bila ubaguzi, na kuwa watanzania wenye mapenzi mema wataendelea kuunga mkono jitihada za serikali hiyo.


Askofu Mapunda atahadharisha kukithiri kwa uharibifu wa mazingira
Askofu wa Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda amewakumbusha watanzania kuwa wana dhamana na wajibu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira ‘nyumba ya wote’ ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowaathiri watu wengi.
Amesema kuwa kwa sasa nchi inakumbwa na uhaba mkubwa wa mvua kutokana na uharibifu wa mazingira. Ametoa rai kuwa matukio mbali mbali ya maisha iwe ni fursa ya kupanda mti na kuboresha mazingira kama mwendelezo wa kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitekeleza.
Askofu NiweMugizi aonya wanaoyumbishwa kiimani
Kwa upande wake Askofu Severin NiweMugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, amewataka watanzania kutubu na kumwongokea Mungu ili kuondokana na vitendo na maisha ya dhambi na giza kwa kutambua uwepo wa Mungu kati yao.
Aidha Askofu NiweMugizi ameonya tabia ya waamini ambao kila kukicha wanakimbilia kwenye makanisa yanayoahidi miujiza ya njia za mkato katika maisha.
Amesema kuwa kinachowakimbiza waamini hao ni kutaka fedha za haraka bila ya kufanya kazi, upwonywaji wa magonjwa na ibada zisizo na utulivu. Ameeleza kuwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, iwe ni fursa kwa waamini kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha nao na kwamba, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, bila kukata wala kukatishwa tama.
Askofu Mkude akemea matabaka
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphory Mkude amebainisha kuwa nidhamu, uadilifu, na uwajibikaji vitaondoa  matabaka yaliyokuwa yanaanza kujengeka nchini kwa kuwa na tofauti kubwa kati ya matajiri na maskini.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU