Shinyanga washauriwa kusomesha watoto wa kike

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ametoa wito kwa  jamii kuwekeza zaidi katika elimu kwa kuwasomesha  watoto wa kike na kuacha mila na desturi mbaya ya kuwaozesha kwa tamaa ya ng’ombe.

Akiongea na wazazi na walezi katika mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya Don Bosco iliyopo Didia jimboni Shinyanga, Askofu Sangu ameitaka jamii kuwekeza zaidi kwenye elimu kwa kutoa upendeleo kwa wasichana  kwa sababu ukimwelimisha  mtoto wa kike umeelimisha taifa.

Askofu Sangu amesema familia bora hutokana na mama aliyeelimika na kuitaka jamii kuacha mila na desturi mbaya zilizopitwa na wakati za kuwaozesha watoto wa kike katika umri mdogo kwa ajili ya tamaa ya mali na ng’ombe.

Amesema katika ukanda wa mkoa wa Shinyanga unaokabiliwa na changamoto ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi ( albino )  kwa imani za kishirikina kutokana na ujinga na tamaa  ya mali jamii inatakiwa kupiga vita vitendo hivyo  kwa kuwekeza kwenye elimu  inayowajenga watu kwenye uelewa.

 “ Ujinga ni mbaya sana hasa kwa  nyakati  hizi ndiyo unaosababisha baadhi ya watu kuwaua wenzao kwa imani za kishirikina, huwezi  ukamtafuta Mungu kwa ujinga, tunahitaji  elimu ya ukombozi itakayotusaidia  kumjua  Mungu  katika maisha yetu,” amesema Askofu  Sangu.

Askofu  Sangu amewaasa vijana wanaohitimu elimu yao kuishi kwa matendo mema  na wawe mitume wa  upendo  kwa wazazi na walezi wao na mahala  popote  watakapoishi na wawe chimbuko la maendeleo  ya kiroho na kimwili huku akiwataka wasibweteke na elimu hiyo bali wajiendeleze zaidi.

Naye Mkuu wa shule ya Sekondari ya Don Bosco yenye wanafunzi mchanganyiko  wa kiume na kike Padri Richard Mtui katika taarifa yake amesema jumla ya wanafunzi 176 wamehitimu kidato cha nne na kuwataka kutumia malezi na  elimu  waliyoipata vizuri katika kupambana na changamoto mbalimbali katika maisha yao.


Kwa upande wake Padri  Mathias Isaka amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwasaidia watoto  hao katika  kuwajenga kiroho na kimwili  juu ya kuwaasa, kuwakemea, kuwaonya kwa sababu dunia ya sasa vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ili  wasiweze kujiingiza katika makundi maovu yenye tabia mbaya miongoni mwa jamii.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU