Ask. Ruwa’ichi: Kutokujua Neno la Mungu ni utapiamlo wa Kiroho

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza Mhashimu Yuda Thadei Ruwa’ichi amesema mkristo yeyote asiyejua neno la Mungu ni sawa na kusakamwa na utapiamlo wa kiroho.
Ametoa kauli hiyo katika Adhimisho la Misa Takatifu liliyofanyika sambamba na sherehe ya kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Buzuruga iliyofanyika parokiani hapo.
Askofu Ruwa’ichi amesema mkristo akitaka kuwa thabiti ni lazima asome, atafakari na apende neno la Mungu kila wakati maana baadhi ya waamini hawapendi kusoma neno la Mungu.
Amesema Yesu Kristo ndiye mchungaji wao mkuu aliyejitoa pale msalabani na kufa kwa ajili ya dhambi zao ili waokolewe na wawe na uzima tele, sasa basi wakristo wasichoke kumwomba na kumwambia Mungu shida zao kila wakati.
Pia katika misa hiyo kulikuwa na sakramenti ya ubatizo ambapo amewahimiza wazazi kuzingatia umuhimu wake akinukuu maneno na kusema  “….wakati akiwa na wanafunzi wake aliwaambia enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, hivyo msibabaishwe kwa kukosa maarifa someni neno la Mungu na kulielewa ili mpate ukweli,” Amesema.

Pamoja na hayo Askofu Ruwa’ichi amewasihi waamini wapende kuikimbilia huruma ya Mungu wasiogope sakramenti ya “kitubio” kwani Mungu ni Baba wa huruma kwa sababu hata muumini akiacha kusimamia imani ya kweli na kuacha kufanya yale yanayopaswa kufanya na kuwa katika upendo wake Mungu hatamtupa akija na kutubu, maana yeye ni Baba wa huruma na siku zote anawasihi kurudi na kutubu dhambi.
Askofu Ruwa’ichi pia ametoa sakramenti ya ndoa ambapo amesema kuwa sakramenti hiyo ni wito wa msingi wa kupokea utume na fursa ya kumtumikia Mungu katika uumbaji na kuwakumbusha wanandoa kuwa katika ndoa kuna mihimili minne, ambayo ni upendo, umoja, udumifu na uaminifu na wapende kuyashika hayo na kuyatendea kazi ili ndoa zao zidumu katika Kristo.

Sambamba na hayo Askofu Mkuu amewaombea neema na Baraka wanaparokia ya Buzuruga waendelee kustawi katika nyanja zote katika vigango, parokia na hata jimbo pia akiwapongeza kwa kukamilisha nyumba ya mapadri kabla ya kuizindua nyumba hiyo na kuibariki. 

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU