‘Matendo yenu yasiwakwaze waamini’ Ask. Nzigilwa awaasa watawa


WATAWA nchini wamekumbushwa kubadilika kimtazamo kwa kuachana na mambo ya ulimwengu, kwa kuwa wao wana wajibu wa kuutakatifuza wakati na kuubadilisha ulimwengu ili uendane na mpango wa Mungu.
Rai hiyo imetolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa katika Sherehe za kuweka nadhiri za daima na Yubilei ya mika 25 ya watawa wa Shirika la Fransisko wa Asizi, wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam.
Askofu Nzigilwa ametahadharisha kuwa endapo watawa hawatakuwa makini watajikuta ulimwengu unawabadilisha ili waendane na matakwa ya ulimwengu badala ya wao kuubadilisha ulimwengu ili uendane na mpango wa Mungu.
“Tunaishi kwenye ulimwengu wenye mambo mengi ya kisasa, ulimwengu unaokwenda na wakati na kutoa nafasi ndogo kwenye mambo ya kimungu. Na tusipojiangalia hata sisi tunaweza kuchukuliwa katika ulimwengu huo. Tunataka na sisi tuonekane wa kisasa. Ninyi siyo wa ulimwengu ingawaje mmetolewa katika ulimwengu huu. Msikubali kukumbwa na malimwengu. Tusiwakwaze waamini. Tusifanye vitu ambavyo waamini hawatarajii kuviona kutoka kwetu” ameeleza.
Aidha Askofu Nzigilwa amewatia nguvu watawa hao kwa kuwakumbusha kuwa katika kila wito Mungu ameweka neema za kutosha katika kutekeleza wito huo kwa hiyo wasiogope, bali washirikiane na neema hiyo na kazi ya Mungu wataifanya kwa ufanisi mkubwa.
Pia amewataka kuendelea kutoa huduma zao kwa upendo ili wanaopokea huduma hizo waone tofauti kutokana na kuhudumiwa na watu wanaompenda Mungu.

“Daima watu wamefurahia huduma zenu, na wamependa watoto wao au wao wenyewe wahudumiwe katika taasisi zenu. Mnafanya huduma hizo katika mikono na macho ya Kristo. Huduma zenu lazima zionekane tofauti, ili wanaopewa huduma waone kuwa wanahudumiwa na mtu anayempenda Mungu na kujali watu. Upendo wa Mungu uongoze huduma mnazotoa kwa watu na kwa jamii. Ndiyo maana wengi wanapenda kupata huduma zenu” ameongeza.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU