Wakristo watahadharishwa juu ya manabii wa uwongo.

ASKOFU Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki Lindi amewataka wakristo kujihadhari na manabii wa uwongo wanaofika kwa kisingizio kuwa wana uwezo wa kuponya magonjwa na kutoa fedha bure.

Askofu Bruno Ngonyani ameyasema hayo hivi karibuni katika Dominika ya pili ya majilio wakati akihubiri katika Kanisa kuu la Mtakatifu Matias Mulumba mjini Songea.

Amesema  waamini wengi wamekuwa wakitekwa na baadhi ya wahubiri wanaojifanya wana uwezo wa kuponya magonjwa na kuwapatia fedha.

“ Tuwe waangalifu na wahubiri wanaosema wana uwezo wa kuponya magonjwa na kutengeneza pesa, tusiamini kila roho, tuzijaribu kama zimetoka kwa Mungu au la, kama ametoka kwa Mungu tumwamini na kama hajatoka kwa Mungu tuachane naye,” amesema Askofu Bruno Ngonyani.

Ameongeza kuwa, Yesu Kristo alisema angalieni mtu asiwadanganye, maana manabii wengi wa uwongo watatokea na kuwadanganya wengi msiwasadiki. Amesema Mungu anaruhusu mwanadamu apate maradhi  na anataka abandukane nayo kwa njia halali.

Pia amewataka waamini kuwa na imani thabiti isiyoyumbishwa na kuishi kama Yesu Kristo,  alivyoishi, kumtambua na kumkiri Yesu Kristu aliye Bwana, mwalimu na kiongozi  katika maisha ya Imani ya kikristo.

Akiwa jimboni Songea Askofu Bruno Ngonyani ameongoza misa takatifu ya mazishi ya Sister Maria Bernada Mbepera OSB wa shirika la Mtakatifu Agnes Chipole, ambapo amesema,”sisi ni raia wa mbinguni na msingi wa muungano wetu na Yesu Kristo ni ubatizo, ambamo tunapata hadhi na kufanyika kuwa watoto wa Mungu na warithi wa mbingu, hapa duniani tunakaa kwa muda tu na ikifika wakati tutapaswa kuondoka kwenda mbinguni kwenye makao ya kudumu.”

Sr. Bernada alikuwa muuguzi na mkunga na amewahi kufanya kazi ya utume katika hospitali ya Peramiho na Ikelu iliyopo katika jimbo la Njombe. Pia alikuwa mtu wa sala, mtii, mpole, mnyenyekevu, mwenye kujituma, mcheshi, mpenda amani, mvumilivu katika mateso,na  mpenda kutoa na kupokea ushauri.


Alizaliwa mwaka 1977, akajiunga na shirika la Mtakatifu Agnes Chipole mwaka 1997, alifunga nadhiri za kwanza mwaka 2004 na nadhiri za daima mwaka 2013.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU