TANZIA: Aliyekuwa mbunge wa Rufiji na daktari bingwa wa moyo, Prof. Mtulia afariki dunia

Profesa Idris Mtulia aliyefariki dunia jana, ameacha pengo katika sekta ya afya huku wagonjwa zaidi ya 20 wakimsubiri awafanyie upasuaji. 

Daktari wa Hospitali ya Tumaini, Profesa Chalonde Yongolo (aliyewahi kufanya kazi na Profesa Mtulia) alisema licha ya kuwa mwalimu wake, alikuwa akishirikiana naye kufanya kazi hospitalini hapo.

 Profesa Mtulia (pichani) aliyefariki dunia ghafla nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam jana asubuhi imeelezwa alikuwa mchapakazi, mwenye maadili msaada mkubwa kwa jamii.

“Ni pigo kubwa, leo alikuwa na wagonjwa 20 ambao walitarajia kupata huduma ya upasuaji. Nimepokea taarifa za msiba huu saa sita mchana na kwa mujibu wa mke wa marehemu kifo chake ni cha ghafla kwa kuwa aliamka salama na alipata kifungua kinywa na akaenda kupumzika na kupitiwa na mauti.” 

Profesa Mtulia aliwahi kuwa mbunge wa Rufiji na Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD). 

Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema licha ya kuwa alikuwa amemaliza muda wake lakini Profesa Mtulia aliitumikia bodi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu. 

“Bado alikuwa mshauri katika mambo mbalimbali yahusuyo bodi.”
 
Bwanakunu alisema Profesa Mtulia alikuwa mchangamfu, mcheshi na huru kuzungumza na watu wote pasipo kujali rika. 

“Hakuwa mtu wa kawaida, alikuwa daktari hivyo alifanya majukumu yake kama mtu anayeelewa vizuri kitu anachokifanya na hata baada ya kumaliza muda wake mchango wake ulikuwa ni muhimu. 

"Alikuwa mtaalamu wa afya, msikivu na mpenda haki aliyehakikisha watu wanapata huduma kwa muda mwafaka."

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU