Maaskofu watoa angalizo kuhusu mwelekeo wa nchi
· Wahimiza utawala wa sheria, haki, amani na uwajibikaji · Watahadharisha kukithiri kwa uharibifu wa mazingira KATIKA kusherehekea Sikukuu ya Noeli nchini, baadhi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania wamewataka watanzania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, na kuachana na matendo ya giza yanayosababisha rushwa, ufisadi na utendaji wa kazi unaofanywa kwa mazoea. Akitoa homilia yake katika Misa ya Krismasi ndani ya Kanisa la Bikira Maria wa Fatima lililopo Geita, Askofu Flavian Kassala wa Jimbo Katoliki Geita amesema kuwa kila mtanzania anapaswa ajione kuwa ni chanzo cha amani. Askofu Kassala ameonya kuwa kisiwepo kisingizio chochote kwa mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi ambayo imekuwa zawadi kubwa na ya kipekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ametoa mfano wa nchi zilizo katika vita, ambako watu wanavyoishi kwa shida kubwa huku maelfu ya watu ...