WAZIRI MKUU ALISHUKURU KANISA KATOLIKI KWA HUDUMA ZA KIJAMII LITOAZO

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema amefurahishwa na uamuzi wa Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wa kutafuta viwanja Dodoma ili wajenge ofisi za makao yao makuu pamoja na makazi ya viongozi wao wakuu.
Ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na Askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki Dodoma Beatus Kinyaiya.
“Sina shaka juu ya maombi yenu ya kupatiwa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu pamoja na makazi ya viongozi wakuu. Sasa hivi Master Plan ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi inapitiwa upya ili izingatie mahitaji ya msingi sababu zamani ilikuwa haijapangwa kwa mazingira ya sasa ya ujio wa Serikali,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema wiki tatu zilizopita alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ili atafute makampuni yenye uwezo wa kupima viwanja kwa haraka. “Hii itatusaidia kutambua tuna eneo kiasi gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana na mahitaji yake,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyashukuru makanisa kwa huduma za kijamii zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama ambavyo ameshuhudia katika baadhi ya maeneo alikopita hapa nchini.
Pia amewakubalia ombi lao la kuwa na kikao cha pamoja baina ya watendaji wa Serikali na makanisa ambacho kitajadili namna ya kuimarisha ubia katika utoaji wa huduma za kijamii hususan za afya na elimu.
Mapema, Baba Askofu Mkuu Kinyaiya alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanahitaji eneo la kujenga ofisi za makao makuu na makazi kwa ajili ya kanisa hilo pamoja na makanisa yaliyo chini ya CCT ambayo kwa pamoja yanaunda Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC). Alisema wanahitaji eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi wa Baba Mtakatifu.
Alisema walipowasilisha maombi yao CDA, waliahidiwa kupatiwa eneo la makazi tu lakini bado wanahitaji eneo la ofisi.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU