UKRISTO WAZIDI KUIMARIKA MAFIA


Zaidi ya watoto 800 wahiji na kuacha historia kisiwani humo
10 waacha dini zao na kukubali kubatizwa

“NENDENI Mafia mkainjilishe. Kwa watoto wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam wanatambua kwa nini huwa tunaenda Mafia kila mwaka. iIa ninyi wengine mtakaporudi nitawaambia” hayo ni maneno ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati akiwaaga watoto wa Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Ifakara na Mpanda katika viwanja vya Msimbazi Centre, jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza safari ya kuelekea Mafia.

Safari hiyo ilianza saa 1:42 asubuhi ikiongozwa na askari wa usalama barabarani, huku takribani watoto 800 wakiwa wenye furaha wakiimba na kusali, na hatimaye waliwasili Mafia saa 11:30 jioni.

Watoto hao walipokelewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa pamoja na Paroko wa Parokia ya Mafia Padri Francis Massawe.

“Mwanzoni mtu ukipangiwa kuja Mafia iwe kwa shughuli ya kikazi au shughuli nyingine, unaona kama umeadhibiwa. Tangu nchi hii ipate uhuru watu waliiona Mafia sio mahali pa kwenda. Kwa kulitambua hilo Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akasema yeye atakwenda na watoto wadogo kwa kuwa waliokuwa wanapanyanyapaa walikuwa ni watu wazima. Lakini watoto ni wanyoofu, wasikivu, wanyenyekevu, na hawana hila mioyoni mwao” ameeleza Askofu Nzigilwa

Akiongea na gazeti la Kiongozi Padri Francis Massawe amesema kuwa Mafia ni kisiwa ambacho asilimia 90 ya wakazi wake ni waislamu hivyo kina changamoto kubwa katika uinjilishaji, huku akimuomba Kardinali Pengo azidi kuhamasisha vyama vingine vya kitume kwenda kisiwani humo kuinjilisha kwani kuhiji kwao kunahamasisha waamini wengine kubatiza watoto wao na kufunga ndoa.

Kutokana na Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2013, idadi ya wakristo kisiwani humo ni 1693, ila hija ya Utoto Mtakatifu kila mwaka imepelekea waislamu 10 kukubali kumpokea Kristo kwa kubatizwa.

 Geofrey Hilmary, Mafia

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU