Haya hapa mafundisho ya uongo tunayoaminishwa wakatoliki



LAKINI jamani, sisi nasi tu watu kamili wala hakuna aliyelaaniwa kati yetu. Sikiliza orodha hii ya mambo yanayofundishwa kuwa ishara za mtu aliyelaaniwa.

Sikiliza uniambie atapona nani katika orodha hii: magonjwa ya kifafa, kisukari, moyo, BP, saratani, ukoma, ukichaa, upofu wa macho, asthma, ukimwi, kifua kikuu; hali za ugumba wa kutozaa, utasa, ufakara, umaskini, kuonewa na kunyanyaswa; vifo vya ghafla, vifo vya ajali kama magari, pikipiki na baskeli; tabia za ulevi, kukojoa kitandani, kupenda ushirikina (uchawi), kuoa wanawake wengi, kuoa na kuacha, uzinzi au uasherati, uvivu au uzembe; mikasa ya kuibiwa, kuunguliwa nyumba au vitu moto, kuumwa na mbwa, kuumwa na nyoka; hali za kutoolewa, kufiwa na waume au wake na kuachika.

Shida zingine katika orodha hiyo ni: kutopata kazi, kutofikia daraja la upadre au utawa, kutomaliza mambo fulani fulani, kutopendwa, kusingiziwa mambo, mafarakano katika familia au ukoo, fedha kutokukaa, kutofunga ndoa katika familia, kukataliwa, kuzaa watoto wafu, kuzaa watoto nje ya ndoa, kutopenda kujihusisha na wokovu;

Kudhulumiwa, kutokuwa na makazi, kujiua au kuua, kufa kwa mifugo, kupelekwa jela au mahakamani, kuliwa na wanyama wakali, kuzaa kwa kufanyiwa upasuaji, kutopandishwa cheo, kutoaminiwa na kutegemewa, kunyang’anywa mke, kununua vitu vilivyoharibika n.k.. Je, umepona hapo?

Halafu katika kitabu kiitwacho Tufanye Nini Kabla ya Kuanza Mafungo? Moyo Mtakatifu wa Yesu na Mapambano Dhidi ya Ushirikina, Uchawi – Mazindiko - Ramli na Maruhani cha Pd. H.J. Mambwe, imeandikwa kwamba kuna mikoa hapa Tanzania imelaaniwa. Unashtuka? Usishtuke, inasomeka hivi:

“Laana ya kitaifa inafanya kazi kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini katika taifa husika, kuanzia ngazi ya – Kata, Wilaya, Majimbo, Mikoa na Taifa. Inategemea na agano lilofanywa na watu au viongozi husika na katika jamii husika, kwa wakati uliopo au uliopita. Hata hivyo, zipo laana zenye kutawala watu wa jamii fulani zaidi. Mfano, ukitazama kwa makini ipo mikoa inayoongoza kwa vitendo vya uchawi na ushirkina.

Maagano yanayosimama katika mikoa hiyo au jamii hiyo na watu wa eneo hilo ni pamoja na uasherati na uzinzi, ombaomba, kutoa wasichana wa kazi za ndani (house girls), kutoa watu wa kufanya biashara za mikononi na katika mazingira magumu na pia watu wake hupendelea kujinyonga.

Haya na mengine mengi ukiyafuatilia utagundua ipo mikataba mbalimbali iliyowekwa na viongozi au watawala wa jadi waliotangulia katika jamii husika kwa ulimwengu wa giza, na kusababisha roho hiyo kuendelea na kurithiwa kutoka vizazi hadi vizazi kwa jamii husika” (uk. 27-28).

Hebu sasa tujiulize, maneno haya kweli ni ya Kikristo? Hivi kama si ya kuwadhalilisha Wakristo ni nini? Mikoa iliyolaaniwa na nchi zilizolaaniwa ni katika bara la Afrika, Asia au Marekani na Ulaya pia? Hivi kweli mambo kama haya unaweza kuthubutu kuwafundisha Wakatoliki wa Ulaya na Marekani pia?

Hivi Baba Mtakatifu na Cantalamesa wanaweza kupokea mawazo ya kipuuzi kama haya? Karismatiki aliyoiruhusu Baba Mtakatifu ndiyo yenye kufundisha mambo kama haya kati ya wanadamu? Thubutu yake, siyo. Haya yetu hapa hapa Tanzania!

Basi, kumbe ukiaminishwa mambo ya laana, lazima utaniuliza, “Nifanye nini kwa vile nimelaaniwa?” au “Tufanye nini kwa vile kata, wilaya, jimbo au taifa letu limelaaniwa?” Hapo ndipo nitakapokuja na upotoshaji mwingine. Nitakuambia eti uvunje mti wa ukoo au mti wa familia. Aidha nitakwambia taifa lifanye maombi livunje laana yake.

Wapi na wapi! Kama jambo la laana ya ukoo au familia lingelikuwa kweli angepona nani? Au taifa gani lingepona? Kwa hilo hata Yesu asingelikuwa mtakatifu, maana babu yake Daudi alikuwa mzinzi mkubwa aliyemuua Uria kwa shauri la mkewe na Sulemani alioa wanawake mia saba na kuwa na nyumba ndogo ndogo mia tatu (rej. 1Fal 10:1-3).

Hapo Yesu mjukuu wao asingeliweza kuishi useja, hata kidogo. Kwa kuwa fundisho la laana halina mashiko, ndiyo maana hatusikii Yesu eti akivunja mti wa ukoo au kulizungumzia jambo hilo katika Agano Jipya.

Kumbe, tuliachilieni mbali fundisho la laana. Kwa hakika hili ni fundisho linalotudhalilisha sana Waafrika. Waliokuwa wakituchukia walitumia sana mafundisho ya laana ili tutawalike. Zamani, tulifikiriwa kuwa manyani makubwa (chimpazee) hata huko Afrika ya Kusini, Dutch Reformed Church lilikuwa linawabatiza Waafrika kwa sharti, wakisema, “Kama huyu ni mtu, nambatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu”.

Lakini enzi hizo zimepita, tusiseme tena wenyewe kwamba tumelaaniwa. Tuchange karata zetu vyema, tuishi vyema.

Matatizo, magonjwa, vifo na dhiki ni mambo ya kawaida ulimwenguni pote (rej. YbS 40:1-11). Tusiyachukulie kama laana za koo zetu, makabila yetu au mataifa yetu. Tungeweza kuyachambua matatizo yetu kisayansi na kisiasa. Sijui mnaiona aibu iliyopo? Hivi ajira, inapatikana kwa kuvunja miti ya familia na ukoo au kuadhimisha misa ya kufunguliwa? Kwanza ni misa gani hiyo?
Hivi wasomi wetu wanakubali kwamba ajira inapatikana kwa kuombeana? Hivi umaskini na ufukara wetu unasababishwa na laana iliyopo katika familia, koo zetu, mikoa yetu au taifa letu?
Msinitake nicheke. Kweli tumefikia kiwango cha chini cha umbumbumbu hivi? Hivi hatuwezi hata kujua zinavyotengenezwa ajira katika nchi?

Hivi hatuelewi wanachofanya Wajapani, Wachina, Wamerakani na Wazungu? Wao wanapotengeneza ajira kati yetu hatuoni? Wanapochukua rasilimali zetu hatuoni? Ndiyo suluhisho liwe kwenda kuomba makanisani na kuvunja miti ya familia na ukoo?

Basi, kwa aibu yetu kuna maelezo mawili tunayonadishiwa. Mosi, kwenye vyuo vyetu vikuu majalimu yanafundisha kwa utaalamu somo la uchumi na kujaribu kufafanua sababu za kukosekana ajira na kutamalaki kwa umaskini na ufukara.

Pili, kuna wanaojiita Wakatoliki wanaopita huko na huko wakiporomosha usomi na kusema kukosekana kwa ajira na kutamalaki kwa ufukara na umaskini sababu yake ni laana tu na dawa yake ni rahisi tu – kuombeana na kukemea laana hizo zilizomo katika familia na koo zetu. Nani wanasema ukweli hapo? Lazima kundi moja liwe linasema uongo, wanazuoni au wahubiri holela? Amueni.

Mimi wala siko njiapanda. Huo msimamo wa pili, mimi nauonea haya sana, natamani kuuficha hata uso wangu. Huo si msimamo wa watu katika karne hii ya ishirini na moja, karne ya sayansi na teknolojia. Aidha si msimamo wa Kanisa makini kama Kanisa Katoliki. Ni msimamo wa watu wa zamani kabisa. Ni msimamo wa enzi za ujima!

Kumbe mtu aliyekubalishwa uongo wa kwamba amelaaniwa anaweza kuingizwa kuingizwa katika ushauri na sala ya kitoto kama ifuatayo:

“Fanya maombi na ukiri, ukitamka kwa kinywa chako. Mfano: Ewe laana ya ufukara ninakutaa kwa jina la Utatu Mtakatifu ondoka kwangu. Laana ya magonjwa ondoka kwangu. Laana ya kutangatanga ondoka kwangu. Laana ya ukahaba ondoka kwangu. Laana ya wizi ondoka kwangu. Laana ya fitina, chuki, uongo, wivu, usengenyaji, uchonganishi, ushirikina, ondoka kwangu. Laana ya kutaka ukubwa kwa njia ya ushirikina ondoka kwangu.

Laana ya kukata tamaa, kutoamini, kutokuwa na matumaini ondoka kwangu. Laana ya maneno niliyojinenea au niliyonenewa na wahenga, babu na bibi na wazazi wangu baba na mama ondoka kwangu.

Kataa nafasi ya wanadamu walio hai na waliokufa kuishi ndani yako. Nafasi za mizimu. Nafasi za wachawi ziambie zikuache kwa nguvu ya Utatu Mtakatifu na kwa maombezi ya Mama Maria.
 Angusha ngome zote ziletazo balaa katika maisha yako. Ngome ya mawazo na kila kinachojiinua, kinyume na mapenzi ya Mungu. Jitangazie kuwekwa huru, na uanze kumshukuru Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kwa maombezi ya Mama Bikira Maria” (Tufanye Nini Kabla ya Kuanza Mafungo uk. 31).

Hebu niwaulizeni ndugu zanguni, hivi haya kweli ni mafundisho na sala katika Kanisa Katoliki? Utatu Mtakatifu umetajwatajwa mahali ambapo hapana mafundisho ya Kikatoliki kabisa.

Aidha Mama Maria ametajwa mahali ambapo hapana mafundisho ya Kikatoliki. Kanisa Katoliki linatangaza kuzimu kumefungwa na Bwana Yesu na badala yake kufungua hali tatu tu: mbinguni, toharani na motoni. Sasa ni Wakatoliki gani hawa wanaoamini tena habari za kuzimu? Semeni, msiogope. Semeni, Kanisa lipone.

Na Padri Titus Amigu

Comments

  1. Ahsante Baba natamani niendee kupata mafundisho halisi ya kanisa nitayapata wapi kwa njia ya mtandao

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU