BENKI YA MKOMBOZI YATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA TETEMEKO KAGERA



Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salum Kijuu akipokea msaada wa mabati na mifuko ya simenti kutoka kwa mwenyekiti wa Bodi ya Mkombozi Commercial Bank Plc, Method A. Kashonda ili kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea katika mkoa wa Kagera. Wengine kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Edwina Lupembe na Meneja wa Tawi la Bukoba, James Manyama. Picha kwa hisani ya Executive Solutions.


Benki ya biashara ya Mkombozi imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa waathirika wa tetemeko lililoukumba mkoa wa Kagera hivi karibuni.
Msaada huo ni pamoja na mifuko mia mbili( 200)  ya saruji na mabati mia moja (100) ambayo utasaidia kujenga baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na tetemeko hilo.
Mwenyekiti wa bodi  ya benki ya biashara ya  Mkombozi bwana Method Kashonda  amesema wameguswa kwa namna ya kipekee na janga hilo hivyo kuamua kuungana pamoja na watanzania wengine kuwasaidia waathirika wote ili waweze kurudi katika hali yao ya kawaida.
“Ni jambo la kuhuzunisha hasa kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika tetemeko hili, tunawaombea Mungu awape nguvu na kwa waliobaki tunaomba wavute subira kwani janga hili ni la kila Mtanzania”. Amesema.
Amesema wao wameathirika moja kwa moja pia kwa sababu benki hiyo ina tawi mjini Bukoba na baadhi ya wafanyakazi waliguswa moja kwa moja na maafa hayo.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salum Kijuu  ameishukuru benki ya Mkombozi kwa moyo wa kizalendo na kusema msaada huo utachanganywa na mingine ili ikasaidie wale walioathirika na tetemeko hilo.
“Mahitaji ni mengi na tunashukuru kwa muitikio wenu kuja kuungana mkono na watanzania wengine katika janga hili”. Amesema.
Wafanyakazi wa benki hiyo pia walipata nafasi ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuwapa pole baadhi ya waathirika.
Benki ya biashara ya Mkombozi ilianzishwa mwaka 2009 na kanisa Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kusaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha. 
Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza nguvu.
Benki hiyo ina matawi sita yakiwemo matawi matatu Dar es Salaam, moja Mwanza jingine Moshi na Bukoba pamoja na vituo vya huduma za kibenki Morogoro na Tegeta Dar es Salaam.

Na mwandishi wetu

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU