PADRI LUKA, LULU YA MAENDELEO ILIYOZIMIKA



Ikiwa ni mwaka mmoja tangu afariki dunia marehemu Padri Walter Lukewille, Ambapo kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na Katavi walimzoea kwa jina la Fr.Luka kupitia sherehe za jubilei ya miaka 25 ya parokia ya Familia Takatifu dominika ya29 ya mwaka c, wamemshukuru mungu kupitia nafsi ya Padri Luka, Mmisionari aliyekuza imani na kuleta maendeleo makubwa ya kiroho na kiuchumi katika jimbo la Sumbawanga na jimbo la Mpanda.
"Marehemu Padri Luka ni mmisionari ambae kwa kiasi kubwa amekuwa ni kumbukumbu kwa waamini na wasio waamini wa jimbo la sumbawanga na Mpanda. Padri Lukani lulu ya mkoa wa Rukwa na Katavi  kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoifanya enzi za uhai wake". Amesema Joseph Msengezi mmoja wa waumini wa parokia ya familia Takatifu iliyojengwa na Padri Luka iliyotimiza miaka 25 tangu kuanza kwake.
Mbali ya kufanya mambo mengi kama padri, mtawa na mmisionari mtiifu mnamo mwaka 1994 baada ya kifo cha mhashamu Askofu Kaloro Msakila padri Luka aliteuliwa na Vatican kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo katoliki Sumbawanga, na alifanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa kwa muda wa miaka mitatu hadi pale baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II alipomteua Askofu Damian Kyaruzi kuwa askofu wa jimbo Katoliki  Sumbawanga.
Marehemu PadrI Luka alizaliwa tarehe 1 february 1930 katika kijiji cha Verl nchini Ujerumani. Baada ya majiundo yote katika shirika la wamisionari wa Afrika katika malezi ya kiseminari tarehe 26 Mei 1955 alipata daraja takatifu la upadri na mnamo mwaka 1959 alitumwa rasmi nchini Tanzania Sumbawanga kama mmisionari.
Enzi za uhai wake marehemu padri Luka alifanya kazi  katika parokia ya chiwanda wakati ule  1959 hadi 1962 (chala) 1971 hadi 1984 (Mamba) 1984 hadi 2002. Na baada ya hapo akisaidiana na waamini aliweza kuanzisha parokia ya Kristo mfalme, Roho mtakatifu -malangali na parokia ya familia takatifu ambapo mnamo mwaka 2002 hadi 2004 alisaidia kulijenga kanisa la Mpanda (cathedral) akishirikiana na marehemu askofu Pascal Kikoti na waamini wa jimbo katoliki Mpanda.
Mnamo mwaka 2004  kwa maamuzi ya wakubwa wa shirika na kwa vifungo vya utii, padri Luka alirudi ujerumani katika nyumba ya wamisionari wa Afrika (Afrikanum) iliyoko mjini Kolon. Hapo aliendelea kutoa huduma ya kiroho kwa jumuiya na kwa waumini ambapo January 2014 alihamishiwa katika nyumba ya wazee huko Trier ambako aliishi na wazee wengine waliofanya kazi ya umisionari katika maeneo mbalimbali ya Afrika.
Mwezi Mei 2015 Padri Luka aliadhimisha jubilei ya miaka 60 ya upadri wake na siku chache baadae alipata shida za kiafya na akagundulika kuwa na saratani ya ini. Ugonjwa huu ulimletea udhaifu mkubwa wa kimwili, kwa kipindi cha miezi mitano tu tarehe 17 Oktoba 2015 saa 4: 45 asubuhi Mwenyezi Mungu alimwita kwake kuhani, mmisionari kipenzi cha wanajimbo katoliki Sumbawanga na Mpanda.
Muuguzi aliemuuguza anasema dakika za mwisho alitamka "Sasa ninakwenda" na kwa uso wa tabasamu akatoa pumzi yake ya mwisho.
Tarehe 23 Oktoba 2015 Padri Luka alizikwa katika nyumba ya mwisho pamoja na wamisionari wengine huko Trier Ujerumani. Ibada ya mazishi ilihudhuriwa na umati mkubwa wa wamisionari wa Afrika wake kwa waume, ndugu jamaa na marafiki pamoja na wawakilishi wachache kutoka jimbo katoliki Sumbawanga na Mpanda ambako alifanya kazi takribani miaka 50.
"Mbali ya kazi za kiroho na ujenzi wa makanisa kama hili ambalo alilijenga Padri Luka na mimi nikiwa mmoja wa mafundi, Padri Luka pia alikuwa ni mtu wa hali ya juu lakini hakuwa na matabaka kwa mtu yeyote wala dini wala kabila na alijali maendeleo ya wananchi wote na kila alipofanya utume aliweza kujenga shule na kituo cha afya kila mahali ili watu wanufaike. Padri Luka alikuwa ni mtu wa kwanza kuleta maji ya bomba mkoani Rukwa, hatukuwahi kujua maji ya bomba yalivyo, ameanzisha shule mbalimbali za chekechea na sekondari, kumbi na nyumba za kufikia wageni pia tuliokuwa vijana wafanyakazi kwake tuliweza kunufaika sana" amesema Bwana Didas Lunkonto.
Mbali ya mawazo tofauti kutoka kwa watu wa dini tofauti kuhusiana na maendeleo yaliyofanywa na Padri Luka jimbo Katoliki Sumbawanga linajivunia kuwa na kituo cha Radio ijulikanayo kama Radio Chemchemi ambayo ilianzishwa na Padri Luka na kwa zaidi ya miaka 20 imekuwa ikitoa huduma kwa jamii ya watu wa mkoa wa Rukwa na Katavi.
Kupitia serikali ya Jamhuri ya Tanzania Kwa kutambua mchango mkubwa alioufanya Padri Luka enzi za uhai wake, Raisi wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Ali Hasani Mwinyi alimtunuku Padri Luka Tuzo ya Cheti cha mgeni mmisionari kuleta maendeleo makubwa katika nchi ya Tanzania na kupitia kanisa katoliki jimbo katoliki Sumbawanga kupitia maadhimisho ya jubilei ya miaka 125 iliyofanyika mwaka 2011 kwa niaba ya waumini, watawa na mapadri, Askofu Damian Kyaruzi alimtunuku Padri Luka tuzo ya utume na maendeleo alivyovifanya katika jimbo la Sumbawanga na kanisa la Tanzania.

Raha ya milele umpe ee Bwana , Na mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani Amina.

 Na Emmanuel Mayunga, Sumbawanga

Comments

  1. Namkumbuka sana aliwahi kutupatia semina nzuri mwaka 1999 familia takatifu iliyo simamiwa na Padri Ediga mbegu. Mungu Amkumbuke kwa namna ambavo alijitoa katika Utume.

    ReplyDelete
  2. Nakumbuka Mwaka 2004 aliongoza misa ya kutuaga waamini wa Jimbo la Mpanda alipokua anajiandaa kurudi Germany. M/Mungu amrehemu ampe pumziko la amani 🙏🙏🙏

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU