UTAKATIFU WA NYERERE, MCHAKATO UNAENDELEA




IKIWA WATANZANIA wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 tangu kufariki kwa muasisi na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kanisa Katoliki nchini linaendelea na mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri na baadaye Mtakatifu.

Wakizungumza na gazeti hili kuhusu mchakato huo, baadhi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini  wameeleza kuwa, Kanisa halijanyamaza, halijalegea wala kupuuzia zoezi hilo, bado linaendelea na mchakato huo ambao wameeleza kuwa unahitaji muda kuukamilisha.

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma ameeleza kuwa awali Jimbo la Musoma ambalo ndilo jimbo Mama la Mwalimu Nyerere lilianza kufanya maandalizi ya awali ya mchakato huo lakini Kanisa liliona ni vyema kuhamishia mamlaka ya mchakato huo katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam likishirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwakuwa zaidi ya nusu ya maisha ya mwalimu Nyerere yalikuwa Dar es Salaam ambako aliishi na kufanya kazi.

“Mamlaka ya mchakato wa kumtangaza mwalimu Nyerere Mtakatifu yalihamishiwa Dar es Salaam huku Msemaji Mkuu akiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo ambaye ana mamlaka kamili ya kuratibu na kuteua mahakama (tribunal) za kushughulikia mchakato huo akishirikiana na TEC.

Kwetu sisi tunasubiri barua rasmi ya kusema kuwa Mahakama (tribunal) ya Mchakato wa Kumtangaza Nyerere Mtakatufu katika Jimbo la Musoma imepewa mamlaka ya kuwa sehemu ya mchakato  huo ili tuendelee na hatua nyingine. Tukishapata kibali hicho rasmi tutashirikiana na mahakama nyingine ambazo zimeundwa (zimepewa kibali rasmi) ili tuendelee na hatua nyingine.
Waamini waendelee kusali kwani Kanisa linaendelea na mchakato huo tukiamini kuwa utakamilika kwa wakati,” ameeleza Askofu Msonganzila.

Askofu Nzigirwa aeleza
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Euzebius Nzigilwa ameeleza kuwa, Kanisa linaendelea na mchakato huo hususani kwa upande wa Dar es Salaam ambapo Msemaji Mkuu wa Mchakato huo ni Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu ya afya yake.
“Ninachokifahamu ni kwamba ni kweli mchakato ulianzia jimboni Musoma na baadaye ukahamishiwa Dar es Salaam. Mwadhama anaendelea kuratibu shughuli zote ikiwemo kuunda mahakama (tribunal) za mchakato huo ili pamoja na ile ya Musoma zipewe mamlaka kamili ya kuendelea na hatua nyingine ikiwemo utafiti kwa watu mbalimbali ndani na nje ya nchi ambao wanamfahamu vizuri mwalimu Nyerere aidha kwa kuishi ama kufanya pamoja naye,” amesema Askofu Nzigilwa.

Katibu Mkuu wa Baraza wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raymond Saba ameeleza kuwa, ni kweli Mamlaka ya kusimamia na kuratibu mchakato huo (Competence Forum) ilihamishiwa Dar es Salaam na Baraza la Maaskofu lilikubali kushirikiana na Jimbo Kuu Dar es Salaam ili kufanikisha zoezi hilo.

Rais Mgufuli anamuenzi Nyerere kwa vitendo

Pamoja na juhudi hizo za Kanisa za kumtangaza Nyerere Mtakatifu, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini ameeleza kuwa, Mwalimu Nyerere anakumbukwa na watanzania kwa tunu alizoziacha ziliendeshe taifa hili hususani, umoja wa kitaifa, uadilifu, mapambano dhidi ya rushwa, ubinafsi na ufisadi.

“Jambo mojawapo alilisema Julai 29 Julai, 1985, kwamba: “Kazi iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi, ilikuwa ni kujenga Taifa lenye umoja kwa msingi wa heshima na usawa wa binadamu.”


Lakini yapo mambo mengine ya uongozi wake ambayo tunapaswa kuyakumbuka na kuyaenzi , hususan suala la uadilifu katika uongozi (au maadili ya uongozi), Azimio la Arusha, miiko ya uongozi, mapambano yake dhidi ya rushwa, ufisadi na mengineyo.
Hayo ndyo pia yanalisaidia taifa hili kukua na kusonga mbele licha ya changamoto mbalimbali tulizo nazo,” amesema Askofu Kilaini.

Ameeleza kuwa, rais wa sasa John Magufuli anafanya juhudi za kurudisha heshima katika uongozi. Hilo ni jambo muhimu katika nchi iliyo na maadili na yenye uchu wa maendeleo. Ndiyo maana akikuta kiongozi anayefanya kazi kinyume na taratibu anamfukuza kwasababu anajua miiko ya uongozi.

“Kuna wakati nchi hii kiongozi akiiba ama akifanya kazi kinyume na taratibu anahamishiwa katika wizara nyingine. Kumbe anaenda kuiba sehemu nyingine. Nyerere hakufanya hivyo kamwe na ndio maana Rais Magufuli atachukiwa na wengi kwasababu ya kusimamia miiko ya uongozi. Hata Nyerere alichukiwa lakini alikumbukwa baadaye.

Rais wa sasa aendelee kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya taifa hususani kujali wanyonge. Nchi isitawaliwe na matajiri wanaokwepa kodi halafu mnyonge anyanyasike. Asimamie uadilifu na kujenga taifa moja lenye amani na maendeleo kama alivyokuwa Baba wa Taifa,” amesisitiza.

Nitapeleka ushahidi Roma kuhusu maisha ya Nyerere - Museveni


Wapo wengi wanaoguswa na maisha ya Mwalimu Nyerere katika Nyanja mbalimbali. Ndiyo maana baadhi wanaguna kuchelea kutangazwa Mtakatifu hadi leo.

Ibada ya Misa Takatifu ya kumuombea Baba wa Taifa ilifanyika katika Kanisa la Mashahidi wa Uganda, Namugongo Uganda Juni 1 mwaka 2014 ambapo ibada hiyo iliendeshwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Kampala, Dk. Cyprian Kizito Lwanga.
Hiyo ilikuwa ni mara ya nane ibada ya kuombea mchakato wa kumfanya baba wa Taifa kuwa Mwenyeheri na hatimye mtakatifu unafanyika katika kanisa hilo nchini Uganda ambapo mchakato huo ulianza mwaka 2006. 
 Katika ibada hiyo ambayo ilihudhuria na maelfu ya Watanzania, pamoja na mataifa mbalimbali duniani, pia ilihudhuriwa na familia ya Marehemu Baba wa Taifa, Waziri Mkuu wa Uganda Amama Mbabazi (Wakati huo) mawaziri na wabunge kutoka Uganda, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Balozi wa Tanzania nchini Uganda.

Mwandishi Paul Mallimbo, aliandika hotuba ya Rais Museven aliyehudhuria Ibada hiyo ya Misa Takatifu huku akijawa na maneno mazito yaliyosababisha baadhi ya waamini kububujikwa na machozi kwa jinsi alivyomzungumzia Mwalimu Nyerere.
Rais Yoweri Museveni, alisema kiongozi bora ni yule anayefuata maagizo ya Mungu na kuwatumikia binadamu wote kwa usawa na haki.
Alisema hata kwenye maandiko matakatifu ya Biblia kuna mistari inayomtaka binadamu ampende binadamu mwenzake kama anavyojipenda yeye;
“Kwenye biblia kuna sehemu inauliza kuwa utampendaje Mungu ambaye hujawahi kumuona, na ushindwe kumpenda binadamu mwenzako,” Alisema kwa sababu aliwahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere, anaweza kutoa ushahidi kwamba mwalimu alifanya yote mawili, kumtii Mungu na kuwatumikia binadamu. 
 Mojaya sababu iliyomfanya Marehemu Papa Paulo II kutangazwa mtakatifu ni pamoja na kuisaidia Ulaya Mashariki, ambayo wananchi wake walikuwa hawamwamini Mungu. “Marehemu Papa Paulo II alisaidia kuikomboa Ulaya Mashariki kutoka kwenye ukomunisti, wananchi walikuwa hawaamini kuna Mungu, lakini kwa juhudi zake aliwafanya wamwamini na kumpenda Mungu,”alisema. 
 Rais Museveni alisema anatarajia kupeleka ushahidi kwa Papa Benedict (Kwa wakati huo sasa ni Papa Fransisko) kwamba Mwalimu anasifa za kutangazwa kuwa mtakatifu kwa sababu alimtii Mungu na kuwatumikia binadamu. “Mimi nitapeleka ushahidi kwa Papa, kwamba mbali na mwalimu kumtii Mungu na kuwpenda binadamu wote, pia aliwakomboa Waafrika kutoka Ruvuma mpaka Capetown, huu ni ukweli siyo hadithi,alisisitiza Rais Museveni. 
Kufuatia hatua hiyo ya kwenda Roma kutoa ushahidi, Rais Museveni alisema katika maadhimisho ya kuombea mchakato wa Mwalimu kuwa Mtakatifu yatakayofanyika mwakani (wakati huo), ameahidi kuwaita maraisi wote waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere ili kuuthibitishia ulimwengu kuwa Marehemu Baba wa Taifa ameweza kuwaunganisha waafrika. 
 Alifafanua kuwa Mwalimu ametoa mchango mkubwa wa ukombozi kwa nchi za Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika Kusini, Uganda na Tanzania yenyewe. Hivyo kuja kwa viongozi hao kushiriki ibada hiyo itakuwa baraka kubwa.   
“Jitihada za mwalimu kuikomboa Uganda, ndipo nasi tulipoweza kuzisaidia nchi za Rwanda, Sudan Kusini na Congo kujikomboa na kuongeza kuwa kama si juhudi za mwalimu tusingekuwa na uwezo wa kuwasaidia wengine. 
Upande wa viongozi weusi, hakuna kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa kama Marehemu Mwalimu Nyerere. 
 Hapa Duniani sidhani kama kuna mtu mweusi mwingine ambaye ametoa mchango kama mwalimu, na hili nimelishudia mwenyewe sikuambiwa na mtu. Hata mzee wetu Nelson Mandela alifanya kazi kubwa Afrika ya Kusini lakini Mwalimu alifanya kazi kubwa zaidi ya ukombozi wa Afrika, Alisema. 
Mwalimu aliikomboa Tanzania na kuwafundisha dini ya Kristo, kwa vitendo siyo kwa maneno. Nchi nyingine za Afrika zimepatwa na machafuko ya ukabila na dini kutokana na msingi mbaya wa viongozi waliotangulia. 
Tanzania ni nchi ya Wakristo, Waislamu na wale wengine wanaoamini dini za kienyeji lakini mwalimu aliwafundisha Watanzania fikra za kizalendo za umoja. 
Uganda haikupata elimu nzuri juu ya jambo hilo, viongozi wa kwanza wa taifa letu waliwapandikiza wananchi chuki, kwamba dini ni kumchukia mwenzako, waumini wa dini moja kuwachukia waumini ya dini dini nyingine na matokeo yake ni umwagaji wa damu.  
Biblia inasema kile unachopanda ndicho unachovuna, kwa hiyo sisi hapa tulipanda mbegu mbaya na tukavuna umwagaji wa damu.
Tanzania haijawahi kuona umwagaji mkubwa wa damu zaidi ya ajali za magari na ile ya kipindi kile wakati askari wa Tanzania walipokwenda Uganda kupigana na Idd Amin. Nadhani hii ndiyo damu pekee mmeona.
Mpaka 1986 wakati naingia madarakani raia 800,000 wa Uganda walikuwa wamekufa kutokana na chuki za udini na ukabila.  “Uganda imeshuhudia umwagaji mkubwa sana wa damu, Congo wameona damu, Sudan, Somalia, Kenya, Rwanda na Burundi ni Tanzania pekee ambayo imekuwa kama kisiwa cha amani, hii yote ni kutokana na mchango wa mwalimu Nyerere ambaye alidumisha amani, umoja na maendeleo kwa watu wake.
Sababu mojawapo ya kumfanya mtu awe mtakatifu ni watu kutoa ushahidi wa matukio mbali mbali yaliyofanywa na mtu huyo wakati wa uhai wake.
Nitakwenda Roma kutoa ushahidi kuhusu matendo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. 
 Nikienda kwa Baba Mtakatifu nitatoa ushahidi mzuri juu ya marehemu Mwalimu Nyerere tena nitatoa kwa maandishi siyo kwa maneno pekee yake.
 Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU