MISAADA YA KIGENI ITUSAIDIE KUWA KANISA LA KUJITEGEMEA




NAANZA Makala haya kwa maneno ya Hayati Mwalimu Nyerere aliyesema kwamba: “Itatufaa zaidi kutumia muda katika vijiji tukiwaonesha watu namna ya kuleta maendeleo kutokana na juhudi zao wenyewe kuliko kufanya safari ndefu na za gharama kubwa kwenda ng’ambo kutafuta fedha ya maendeleo”.
Maendeleo waliyoleta wamisionari ni mengi sana na mpaka leo wanazidi kutuendeleza. Lakini bado hatujafikia lengo letu jingine la kulijenga Kanisa la Kitanzania linalojitegemea. Kwa nje inaonekana kama Kanisa letu linajitegemea kiuchumi lakini tuko mbali kabisa na lengo hilo.
Maendeleo ya Parokia zetu yasidhaniwe kuwa ni maendeleo ya Kanisa. Kujitegemea kwa wamisionari wa kwanza si kujitegemea kwa wakristo wa Tanzania. Si jambo la ajabu kumsikia mmisionari akishangaa kama mapadri waafrika watapata wapi wataalamu na fedha za kuendeleza shughuli zote zilizoko Parokiani hivi sasa.
Hii ni kwa sababu kile wanachokitoa wakristo wengi kwa kusaidia Kanisa lao hakitoshi kuendesha shughuli zote tulizonazo hivi sasa maparokiani na majimboni.
Leo tunapata matatizo kupata zaka ya kanisa sababu parokia zetu zina vitu ambavyo kwa watu ni alama ya utajiri. Mahali pengine ni kweli kuna vitu vingi lakini hivyo havikuletwa na wakristo wa Tanzania au wakristo mahalia bali wa ng’ambo, ndiyo maana wakristo wetu inawapasa waanze toka sasa kujifunza kutoa zaidi kwa ajili ya kanisa lao kama vile hao ndugu wa huko Ulaya na Marekani.
Namna nyingine baadaye watakapoondoka kabisa watafikiri kuwa Kanisa letu hapa linajitegemea kiuchumi kumbe sivyo, bali ni kiutumishi tu.

Watu walizoea kupata bure:
Kanisa ambalo ni mahali pa ibada, ni kitu kimojawapo kati ya vile vya maana sana ambavyo wakristo wanahitaji kwa ajili ya ibada na mambo ya liturujia.
Toka mwanzo ingekaziwa sana kwamba wakristo lazima watoe kiasi fulani kwa ajili ya ujenzi wa makanisa. Lakini inasikitisha kwamba makanisa makubwa na majumba kadhaa yamejengwa bila wakristo kutoa hata senti moja mahali pengine. Si lazima watoe sehemu kubwa hasa kama hawana chochote.
Lakini kiasi kidogo wangeweza kutoa, bora tu kama wanashirikishwa katika ujenzi wake. Tuanze polepole kuondoa mawazo ya kwamba makanisa na majumba ya mapadre yatajengwa daima na maaskofu bila wakristo kusaidia.
Wakatoliki wengi katika sehemu fulani hawakuzoea kulipa kitu kwa ajili ya ujenzi wa makanisa, nyumba za mapadre, ghrama ya mahitaji ya kanisa na safari ya kichungaji ya mapadre katika vigango.
Ndiyo maana mahali pengine wanaona kama ni fundisho jipya kutoa zaka ya kanisa na michango mingine kwa ajili ya kujenga kanisa au kutoa posho ya makatekista wo. Wanafanya hivyo si kwa sababu ya ubishi, bali ni kwa sababu hawafahamu wajibu wao kutokana na mazoea waliyopata toka mwanzo.
Kama wangefahamu mapema bila shaka wangetoa. Wakati fulani wakristo tangu mwanzo walipewa misaada bila maelezo kwamba nia ya misaada hiyo ni kutaka baadaye wajitegemee.
Mwalimu Nyerere alisema kwamba: “Kuna njia moja tu tunayoweza kutumia kuwafanya watu wajiletee maendeleo yao wenyewe. Njia yenyewe ni kuwaeleza na kuwaongoza”.
Kwa njia hizo watu wanaweza kusaidiwa wakaelewa shida zao na mambo yanayoweza kufanya kumaliza shida hizo. Kwa hiyo inatupasa kuwaonesha watu njia ya maelezo kwamba ingawaje wanaona majengo mazuri, bado kanisa haliwezi kujengwa na mambo hayo, isipokuwa waamini wenyewe wanashughulika kuinua hali ya Kanisa la Tanzania.
Misaada ya ndugu zetu wa ng’ambo iwe tu ni ya kuendeleza kile ambacho tunacho au kutafuta kingine kwa mtaji wa kutoka nje. Kama wataelewa maelezo hayo sina shaka wakristo wengi watakuwa tayari kulipa zaka na michango yao ya kulijenga Kanisa.
Wakristo waelezwe kwa mafundisho ya kina kuhusu matumizi na namna ya zaka na michango mbalimbali ya Kanisa kabla ya kutiliwa mkazo utoaji wake. Kama watu wameelewa ndipo hapo wanaweza kuanza kutilia mkazo utoaji wake.
Waamini waelezwe kwamba zaka ya Kanisa hutumika kwa kuendeshea shughuli zote za Kanisa. Zaka ya Kanisa ni kwa ajili ya mahitaji ya Parokia, Jimbo na Kanisa lote kiujumla.
Kutoa Zaka si jambo jipya, ni Amri pia ya 5 ya Kanisa. Hata mababu zetu Abrahamu Mw. 14:20, Mw. 28:22, kumb. 14:22-28, 26:12-15 na Hes. 18:21-22, walitoa Zaka na walifundishwa na Musa. Hata Wafarisayo walikuwa waamini katika kutoa zaka Mt. 13:23, Lk.11:42. Ni mazoea na ya kufaa ambayo humnyunyizia mafaa juu ya mlipa zaka, Parokia na Kanisa lote ulimwenguni.
Wakati wowote wa kulipa zaka, mambo yafuatayo daima yakumbukwe, yaani ni lazima nitoe zaka kwa sababu:
1)      Nampenda Mungu na jirani yangu.
2)      Nataka kuona kanisa linaendelea.
3)      Mungu anadai, na
4)     Malipo yake ni mara mia zaidi kwa mtumishi mwaminifu.



Na Syllvanus Kayanda



Mwandishi ni Padri wa Kanisa Kuu,
Jimbo Katoliki Kigoma
P.O.Box 71 KIGOMA.                                                  

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU