UJUMBE WA BABA MTAKATIFU DOMINIKA YA MISIONI 2016



KANISA LA KIMISIONARI, SHUHUDA WA HURUMA
Wapendwa Kaka na Dada,
Jubilei isiyo ya kawaida ya Huruma ambayo Kanisa linaadhimisha, hutoa mwanga wa pekee juu ya Dominika ya Misioni Duniani 2016:
Inatualika ili tutafakari Uenezaji Injili kwa mataifa (Missio ad gentes) kama jukumu kubwa
na kazi nzito ya huruma, kiroho na kimwili. Katika Dominika hii ya Misioni Duniani, sisi sote tunaalikwa “kwenda” kama wafuasi wa umisionari, kila mmoja akitoa kwa ukarimu  vipawa, ubunifu, busara na mang’amuzi yake, ili kufikisha ujumbe wa wema na huruma ya Mungu kwa familia nzima ya wanadamu. Kwa muktadha wa fadhila ya kimisionari, Kanisa linajali na kuwahudumia wale ambao hawajaijua Injili, kwa sababu linapenda kila mmoja aweze kuongoka na kushuhudia upendo wa Bwana. Kanisa “limekasimiwa kuutangazia ulimwengu huruma ya Mungu, moyo wa Injili unaodunda” (Misericordiae Vultus, 12) na kuhamasisha moyo wa huruma pande zote za dunia, hadi kumfikia kila mtu, kijana au mzee.
Aidha, huruma inapomfikia mtu, huwasilisha furaha ya kina katika moyo wa Baba; kwani toka mwanzo Baba kwa upendo wote, amewaelekea wale ambao wako katika hali hatarishi ya kuweza kudhuriwa, kwa vile ukuu na nguvu zake zimedhihirika waziwazi katika uwezo wake wa kutambua kupitia wadogo, wanyonge na wanaokandamizwa (rej. Kum 4:31; Zab 86:15; 103:8; 111:4). Yeye ni mwema, anajali na ni Mungu mwaminifu ambaye yuko karibu kwa wahitaji, hususani maskini; anajihusisha mwenyewe kwa upole katika uhalisia wa maisha ya binadamu kama baba na mama wanavyojitoa kwa ajili ya maisha ya watoto wao (rej. Yer 31:20). Biblia inapoelezea juu ya mimba, hutumia neno linaloashiria huruma: kwa hiyo, linahusisha upendo wa kimama kwa wanae, ambao daima atawapenda, katika mazingira yoyote yale, bila kujali kile kitakachotokea, kwa sababu ni matunda ya mimba yake. Hiki ni kipengele muhimu pia kuhusu upendo ambao Mungu anao kwa watoto wake wote, ambao amewaumba na ambao pia anataka kuwalea na kuwaelimisha; mbele ya hali zao za udhaifu na kukosa uaminifu, moyo wake umetiishwa na huruma (rej. Hos11:8). Mungu ni mwenye huruma kwa wote; upendo wake ni kwa watu wote na huruma yake inaenea kwa viumbe vyote (rej. Zab 144: 8-9).
Huruma inajidhihirisha kiuadilifu katika Neno Mwilisho. Yesu anaonyesha uso wa Baba ambaye ni tajiri wa huruma: “anazungumza juu ya huruma na kufafanua kwa kutumia ufananisho na mifano, lakini juu ya hayo yote, yeye mwenyewe huumwilisha na kuupa uhai” (John Paul II Dives in Misericordia 2). Tunapomkaribisha na kumfuata Yesu kwa njia ya Injili na sakramenti, tunaweza, kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kuwa na huruma kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma; tunaweza kujifunza kupenda kama anavyotupenda sisi na kuyafanya maisha yetu kama zawadi isiyo na masharti, ishara ya wema wake (rej. Misericordia Vultus, 3). Kanisa kati ya watu, kwanza kabisa ni jumuiya inayoishi kwa rehema ya Kristo: Kanisa huhisi kutazamwa na Kristo na kwamba amelichagua kwa upendo na huruma yake. Aghalabu, ni kwa upendo huo, Kanisa hugundua mamlaka yake, kuyaishi na kuyafanya yajulikane kwa watu wote kwa njia ya majadiliano murua na kila aina ya tamaduni na imani za dini.   
Upendo huu wa huruma, kama ilivyokuwa siku za mwanzo wa Kanisa, unashuhudiwa na watu wengi, wake kwa waume, wa kila rika na hali iwayo. Kutokana na ongezeko kubwa la uwepo wa wanawake katika ulimwengu wa kimisionari, wakifanya kazi bega kwa bega na wenzi wao wanaume, ni ishara dhahiri ya upendo wa kimama wa Mungu.
Wanawake, walei na watawa, na kama ilivyo siku hizi familia nyingi zinatekeleza wito wao wa kimisionari katika nyanja mbalimbali; kuanzia kutangaza Injili hadi kwenye matendo ya huruma. Pamoja na uinjilishaji na utoaji huduma za kisakramenti za wamisionari, wanawake na familia mbalimbali kila mara hujitanabaisha kwa uelewa mpana wa matatizo ya binadamu na wanajua jinsi ya kuyadadavua (kuyashughulikia) ipasavyo na wakati mwingine kwa kutumia mbinu mpya: jinsi ya kuyakabili kwa daima, wakilenga yale ya utu badala ya miundo-mbinu (vitu) kwa kupanga nguvukazi watu na huduma ya kiroho ili kuweza kujenga mahusiano mazuri, ya maelewano, amani, mshikamano, majadiliano, ushirikiano na udugu, miongoni mwa watu binafsi na katika ustawi wa jamii na maisha ya kiutamaduni, husuani kwa kuwahudumia maskini.
Katika maeneo mengi uinjilishaji huanza na utoaji elimu, ambako kazi ya kimisionari huelekeza muda na nguvu kwa wingi; kama vile mtunza shamba la mizabibu katika Injili (rej. LK 13:7 – 9; Yn 15:1) akingojea tunda kwa uvumilivu baada ya miaka mingi tangu kupandwa; kwa njia hiyo, wanawaleta watu wapya wawezao kuinjilisha, ambao wataipeleka Injili kwenye maeneo ambayo vinginevyo ingekuwa vigumu kufikishwa. Kanisa pia linaweza kufafanuliwa kama “mama” kwa wale ambao siku moja watamfuasa Kristo. Hivyo natumaini kwamba watu watakatifu wa Mungu, wataendelea kutoa huduma hii ya huruma na ya kimama ambayo huwasaidia wale wasiomjua Bwana waweze kukutana naye na kumpenda. Imani ni zawadi ya Mungu na siyo matokeo ya nathari, kumbe inakua (shukrani kwa imani na hisani ya wainjilishaji wanaomshuhudia Kristo. Kadiri wanavyotembea kwenye mitaa ya dunia, wafuasi wa Yesu wanahitaji kuwa na upendo usio na mipaka, kipimo kilekile cha upendo ambao Bwana wetu anacho kwa watu wote. Tunazitangaza zawadi za kupendeza sana na mashuhuri ambazo ametupatia: Uhai wake na Upendo wake.
Watu wote na wa tamaduni zote, wana haki ya kupokea ujumbe wa wokovu ambao ni zawadi ya Mungu kwa kila binadamu. Hiyo ni ya msingi zaidi tunapotafakari juu ya ukosefu wa haki, vita na majanga dhidi ya utu ambayo bado yanatakiwa kupewa suluhu. Wamisionari wanajua kutokana na mang’amuzi ambayo Injili ya msamaha na huruma iwezavyo kuleta furaha na upatanisho, haki na amani. Hivyo, mamlaka ya Injili, “enendeni, basi na kufanya wafuasi wa mataifa yote, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, mkiwafundisha kuzingatia yote niliyowaamuru” (Mt 28: 19 – 20) hayajakoma; bali amri hiyo inatutaka sisi sote, katika mabadiliko yaliyopo na changamoto zake, ili kusikiliza mwito wa umisionari uliohuishwa kwa “mapigo,” kama nilivyodokeza katika mausio yangu ya kitume Evangelii Gaudium: “Kila mkristo na kila jumuiya hawana budi kufuata njia ile ambayo Bwana anailekeza, kumbe sote tumealikwa kutii mwito wake kwenda mbele kutoka katika ukanda wetu mtulivu ili mradi kuwafikia wale wote wa ‘pembezoni’ ambao wanahitaji mwanga wa Injili” (20).

Mwaka huu wa Jubilei unaadhimisha kumbukumbu ya 90 ya Siku ya Misioni Duniani, kama alivyoidhinisha mwasisi wake Papa Pius XI mwaka 1926 na kuratibiwa na Shirika la Kipapa la Uenezaji wa Imani. Ina mantiki kwa hiyo, kujikumbusha mafundisho ya busara ya watangulizi wangu walioamuru kwamba shirika hili lipewe matoleo yote yaliyokusanywa kutoka katika kila jimbo, parokia, mashirika ya kitawa, vyama vya kitume po pote duniani kwa ajili ya kuzitegemeza jumuiya za Kikristo zenye kuhitaji na katika kusaidia kueneza Habari Njema hata mwisho wa dunia. Leo pia, tunaamini katika alama ya umoja wa Kanisa la kimisionari. Kamwe tusiifumbe mioyo yetu kwa maslahi yetu wenyewe tu, bali tuifumbue kwa maslahi ya wanadamu wote.
Maria Mtakatifu, kielelezo kitukufu kwa wote waliokombolewa, mfano wa wamisionari kwa ajili ya Kanisa, wafundishe watu wote, wanaume, wanawake na familia kusitawisha na kulinda wanaoishi na uwepo wa kiajabu wa Bwana Mfufuka kila mahali, awaye yote anayehuisha uhusiano baina yao, tamaduni na watu, na anayewajaza wote kwa huruma pendevu.

Kutoka Vatikano, 15 Mei 2016 Sikukuu ya Pentekoste.
Fransisko

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU