TAFITI BINAFSI: HATUA MUHIMU YA KURITHISHA MALEZI BORA.



Kila mwanadamu ana sauti ya ndani ambayo humpa taarifa juu ya mwenendo wake. Taarifa hii ambayo twaweza kuiita “mazungumzo binafsi” (self-talk) kwa kiasi kikubwa huwa ya msaada endapo mtu atakuwa na muda wa kupalilia taarifa au mitazamo hii ya ndani iwe  chanya.
Malezi bora ambayo pia yanafaa kuwashirikisha  wengine lazima yaanzie na kujiamini kwa mtoaji , kuwa yeye mwenyewe anaamini atakayotoa ni sahihi. SAUTI HIZI NI LAZIMA ZISIKIKE NDANI MWETU ILI KUTOA MALEZI BORA.

MIMI NDIO MABADILIKO YENYEWE:
Upendo huanzia nyumbani. Huwezi kutoa usicho nacho. Mzazi ni lazima ajiamini kuwa jinsi anavyoishi, maadili aliyonayo ni safi na bora, ndipo itakuwa rahisi kwake kumfundisha mtoto hayo anayoamini kuwa bora. Ni rahisi sana kuwaelekeza wengine mema kama sisi wenyewe ni wema. Ni kwa kutojua tunakosea mara nyingi tunaposubiri kupata sifa za mtu kioo katika jamii [model] ndipo eti tuwalee watoto wetu kadri ya sifa za mtu huyo.

MIMI NI WA MUHIMU:
Tunaposahau umuhimu wetu mara nyingi tunajikuta tukifanya vitu vinavyopingana na jinsi tulivyo. Sisi sote ni wa muhimu kwa jinsi tulivyoumbwa na Mungu. Kwa mantiki hii kwa nini usiwe kielelezo cha ubora unamtafuta mtu mwingine ili uige kwake?.
Ni wangapi tunajijua kuwa tuna sura nzuri, sauti nzuri, tabia nzuri?, kinyume chake tunapoteza muda kutafuta tabia njema kwa fulani. Nasema hivi, RAHA JIPE MWENYEWE! lazima utafute mazuri ndani yako mwenyewe, ukisubiri hadi wakuambie una maadili mema ni siku ya maziko yako kwa taarifa yako ndipo watasoma wasifu wako, huko kuzimu unaenda kutoa malezi gani, utakuwa umechelewa.
Siku moja niliuliza kikundi kimoja, nani mwenye tabia nzuri hapa anyooshe kidole?. Nilishangazwa na umati ule kwa jinsi walivyokaa kimya bila jibu. Nikawahoji tena kwa nini hamnyooshi vidole nikifikiri labda wote walikuwa wameungua vidole walau hata niwaambie wanyooshe hata miguu. Wakasema, BABA PADRI HUWEZI KUJUA TABIA YAKO MPAKA WENGINE WAKUELEZE. HAAA! Ni shida. Hawakukosea sana kwani ni kweli zipo tabia huwezi kuzijua wewe wengine wanajua, ila  ni zote?. Tuanze  kufanyia kazi zile tabia njema  zilizomo ndani mwetu.

 “MCHAWI” NI MTAZAMO WAKO:
Neno “mchawi” hapa lieleweke kuwa ni bahati mbaya, jambo lolote baya, chanzo cha matatizo au kutokufanikiwa. Hivi mwaikumbuka ile hadithi ya BABU NA KIOO? tukumbushane kwa wale waliosahau.
Babu mmoja wa kijijini aliamua kwenda zake mjini. Alipofika katika kukaa kwake siku moja aliona kioo akajiangalia na bila kujua alisema “ Haa! hii ni picha nzuri ya Baba yangu”. Akaamua kuinunua ile picha(kioo). Akiwa njiani alikumbuka kuwa mke wake alikuwa hampendi baba yake, akanuia moyoni kuwa ni lazima aifiche ile picha(kioo) awe anaangalia tu kwa muda. Asubuhi moja baada ya kuondoka, mke wake alienda kuangalia ni nini kile ambacho mme wake alikuwa akikitazama mara kwa mara. Alipoenda akaangalia na kusema “ Kwa hiyo huyu mchawi mbaya hivi ndio mume wangu anamwangalia kila mara, kweli mjinga huyu!” (meseji senti).
Ni muhimu kujijua upoje. Watu wengi wana picha mbaya yao wenyewe, ya familia zao, bila kujijua. Jiulize mwenyewe nini kizuri ulicho nacho? na hapo utaweza kushirikisha wengine.
Mtazamo wa jinsi tulivyo ndio utakaotusaidia kuwalea watoto na vijana wetu kwani tunaamini katika yale yaliyopo ndani mwetu yanayotusaidia. Mwandishi THICH NHAT HANH anasema “…..huhitaji kukubaliwa na wengine. Jikubali mwenyewe”.
Tujikubali kuwa tuna maadili mema ndipo itakuwa rahisi kuwapa wengine ushauri mzuri kwani unalowashauri wanaliona kwako. Tujitafiti tuna mazuri gani ili iwe rahisi kuwapa wengine.

Padri SAMUEL KALISTI MVATI
(PAROKIA YA NDUNGU)
JIMBO KATOLIKI SAME.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU