NAMWUNGAMIA MUNGU MWENYEZI NANYI NDUGU ZANGU


Kuhani na wahudumu wakishafika mbele ya madhabahu huinama sana mbele ya  Msalaba, lakini kama  kuna Ekaristi Takatifu hupiga goti, kisha kuhani huenda kubusu altare. Altare ni meza ya kumtolea Mungu sadaka, lakini ni pia ishara ya Yesu Kristo.Tendo la kubusu altare ni ishara ya kuisalimu na kutoa heshima kwa Kristo.
Ndivyo kila mkristo anavyotakiwa kuinamia Msalaba  aingiapo kanisani. Iwapo mbele imehifadhiwa Ekaristi anatakiwa kupiga goti ishara ya kumwabudu Yesu katika tabernakulo; lakini kama hakuna Ekaristi Takatifu, anatakiwa kuinama sana ndipo kwenye benchi na kusali.
Tafakari haitolewi  
Baada ya kufika mahali pa kuanzia Adhimisho la Ekaristi, kuhani huanza Adhimisho kwa Ishara ya Msalaba na kisha huwaamkia Wakristo kama tulivyoeleza katika makala iliyopita. Hapo mwongozo katika Kanuni ya Misa unasema hivi: Kuhani, au shemasi, au mhudumu mwingine  anaweza kuwaeleza waamini nia maalum ya Misa ya siku hiyo kwa maneno machache kabisa.
Baadhi hutumia nafasi hiyo kutoa tafakari ya masomo ya Misa ya siku hiyo. Binafsi ninashangaa na kujiuliza: utaratibu huo umeanzia wapi? Mwongozo unasema ni nafasi ya kuwaeleza waamini nia maalum ya Misa. Haisemi chochodte kuhusu Masomo ya Misa. Hiyo siyo nafasi ya kutoa tafakari ya Masomo wala kueleza maisha ya mtakatifu ambaye hukumbukwa siku hiyo kwamba alizaliwa wapi, mwaka gani, aliishi vipi, karama zake  na kadhalika. Kufanya vile ni kinyume cha mwongozo.
Tafakari fupi ya Masomo hata kama ingekuwa ya sentensi mbili au tatu hutolewa  baada ya kutangaza Injili. Nafasi hiyo ni ya kuwaeleza waamini nia maalum ya Misa na aina ya Misa  inayoadhimishwa siku hiyo tena kwa maneno machache sana. Tukumbuke waamini huwa wamesimama na katika hali hiyo si vema kusikiliza tafakari au historia ya maisha ya mtakatifu wa siku. Mara nyingi mtoa tafakari hupata kishawishi cha kuaendelea kutoa tafakari waamini wakiwa wamesimama. Inatupasa sote kujitahidi kufuata Uongozi wa Kanisa unavyoelekeza, na siyo kufuata matakwa yetu katika kuadhimisha  Liturujia.
Tukiri dhambi zetu
Kisha kueleza nia ya Misa, Kuhani huwaalika waamini wote waweze kukiri kwamba ni wakosefu na  waweze kusali kwa pamoja sala ya kumwungamia Mungu na kila mmoja. Tafsiri tuliyoizoea ilisema: Tujute dhambi zetu tupate kujiweka tayari kutoa sadaka takatifu. Tafsiri hiyo imeachwa na badala yake kuhani husema: Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu ili tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu. Kuna tofauti kubwa kati ya tafsiri hizo mbili.
Tofauti ya kwanza ni katika uchaguzi wa  maneno. Badala ya neno Tujute sasa kuhani anasema Tukiri.Neno kujuta linaendana zaidi na Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Tunapoadhimisha Sakramenti hiyo tunafanya liturujia ya majuto kisha tunakwenda kuungama dhambi kwa kuhani. Kila Mkristo lazima aziungame dhambi kubwa zote  katika Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho.
Tafsiri mpya inasema: tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu. Maneno hayo ni muhimu pia. Ni Roho Mtakatifu  anayetuwezesha kuadhimisha mafumbo  matakatifu. Katika kutenda yale yanayotupasa mbele ya Mungu, daima ni Mungu mwenyewe hutangulia kwa neema yake kutuhimiza na tufanye na kutuwezesha au kutusindikiza kufanya vizuri. Mwaliko huo sasa umekaa vizuri zaidi kuliko ule wa mwanzo.  
Tufahamu vizuri tendo tunalolifanya mwanzoni mwa Misa ni la kujiweka tayari kwa Adhimisho la Ekaristi. Mwaliko anaotoa kuhani anaposema: “Tukiri dhambi zetu ...”  unadhihirisha kwamba tendo hili ni tofauti na lile tunalolifanya katika Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Tunakaa kimya kitambo kifupi kutafakari hali yetu ya dhambi. Nafasi hiyo ya unyamavu nayo ni muhimu sana.
Katika ukimya kila mmoja ajione yupo mbele ya Mwenyezi Mungu, hujinyenyekea na kujiona yu mkosefu. Hata iwapo  Mkristo hana dhambi kubwa, katika unyamavu huo, kabla ya kuadhimisha mafumbo hayo matakatifu,  ajione ni mkosefu.   Wakristo huwa wamesimama, na kuhani anaposema “Tukiri dhambi zetu...” ndipo waamini hupiga magoti na kutafakari.
Kwa bahati mbaya sana, pengine nafasi hiyo haitolewi kwani wakishapiga magoti,  kuhani huanza mara: “Namwungamia Mungu mwenyezi...” Tunawaomba makuhani watoe nafasi ya unyamavu hata robo dakika tu na waamini wafahamu umuhimu wa unyamavu huo ni wa kila mmoja kutafakari dhambi zake, na hali yake ya dhambi. Mababa wa Mtaguso wamehimiza nafasi hizo zizingatiwe (Hati ya Lit. 30).
Baada ya unyamavu huo kwa pamoja waamini hukiri mbele ya Mungu na waamini wote waliopo kanisani kwamba ni wakosefu. Kuhani anaanza:   Namwungamia Mungu mwenyezi.” Waamini wote huendelea kusali sala hiyo ya kukiri dhambi. Tafsiri ya zamani ilisema: Nakuungamia Mungu mwenyezi. Kwa kuwa ni tendo la kukiri dhambi pamoja  Sala inaanza Namwungamia Mungu mwenyezi.” Tendo ni la kukiri kwamba tu wakosefu; siyo la kuadhimisha Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Sakramenti ya Ekaristi haipo kwa ajili ya kuondoa dhambi kubwa ndivyo tunavyofundishwa katika Katekisimu Katoliki.
Tunasoma hivi: “Ekaristi hutukinga tusitende dhambi za mauti... Ekaristi haipo kwa lengo la kuondolea dhambi za mauti. Kuondolea dhambi za mauti ndiyo kazi hasa ya Sakramenti ya Upatanisho. Ekaristi ni hasa Sakramenti ya wale walio katika ushirika kamili na Kanisa.”  Basi  tendo tunalolifanya mwanzoni mwa Misa ni tendo la kukiri dhambi na kujiweka tayari kwa Adhimisho la Ekaristi.
Kila Mkristo inampasa kusali sala hiyo ili kukiri mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya waamini wote waliopo kwamba ametenda  dhambi. Mkristo ambaye hufumba mdomo na hasali  tunapasa kumwuliza: Je, mwenzetu umefika kanisani kufanya nini?
Tuzingatie Matini ya Liturujia.
Kwamba kuhani anaweza kubadili maneno  sehemu mbalimbali katika kuadhimisha Liturujia ni fursa inayoelekezwa sehemu mbalimbali katika Adhimisho lenyewe. Hata hivi tuzingatie matini, na kuelewa nini tunaelekezwa. Kwa nafasi hii kuhani alisema zamani: Tujute dhambi zetu... kumbe sasa anatakiwa  kusema: Tukiri dhambi zetu.  
Baba Askofu Salutaris Libena, Askofu wa Jimbo la Ifakara na msimamizi wa Idara ya Liturujia kitaifa alipotoa mada katika Kongamano la kitaifa la Ekaristi kule Mwanza aliwasihi makuhani kuzingatia matini ya tafsiri hii mpya katika kuadhimisha Ekaristi. Kwa namna ya pekee aliwaomba kuzingatia jambo hilo hapo mwanzoni ambapo mabadiliko ya tafsiri  hayajazoeleka kwa Wakristo wengi, ili nao wanapofuata katika vijitabu vile ambavyo vimeandaliwa kwa ajili yao waweze kufuata vizuri.
Kwa nafasi hii basi turudie wito ule aliotoa Baba Askofu na kwa kweli ndivyo inavyotakiwa kusema kadiri ya tafsiri na maana ya tendo tunalolifanya. Tukiri dhambi zetu na siyo Tujute dhambi zetu.

Na Padri Paul Chiwangu

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU