MALEZI IMARA:”MAWILI HAYA” ndio,ila wewe zaidi.




Tumeshuhudia kauli mbalimbali za majuto toka kwa baadhi ya watu wakidai kuwa isingekuwa baba, mama, kaka au rafiki yangu yule maisha yangu yasingekuwa hivi.
Lakini pia tumesikia kauli za kutia moyo za watu waliofanikiwa na kudai kuwa ni kwa sababu ya fulani nina maisha mazuri hivi, nisingemsikiliza ningeharibikiwa maisha.
Kauli hizo  hapo juu ni uthibitisho kuwa  malezi imara ni matokeo ya muunganiko wa ushauri wanaotupatia watu mbalimbali, athari za jamii inayotuzunguka na mwishowe lile mtu mwenyewe baada ya kupokea hayo mawili analoona ni muhimu kulizingatia.
Mambo haya matatu ni lazima yawekwe pamoja ili kumsaidia mtu kuwa na maamuzi bora na mwishowe kuwa imara katika malezi yake. Kila jambo lina umuhimu wake.
Nafasi ya washauri:
Hawa wanajumuisha wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zako wanaotumia nafasi walizonazo kwako kukushauri la kufanya.
Hawa wana umuhimu sana kwani waliokuzidi umri hukupatia yale yaliyowasaidia kuwa watu wa heshima katika jamii walimo, ila wanakuepusha na mitego mibaya waliyowahi kukutana nayo hivyo usije ingia huko.
Lakini swali msingi hapa ni, Je ni kila litokalo kwa washauri unalizingatia kama dira yako ya malezi bora? kisa tu aliyekuambia ni Baba au Mama yako au rafiki yako ambaye hutaki kugombana naye hata siku moja.
         Jamii:
Huchangia pia katika makuzi yetu kimalezi.Kuna mifumo ya kijamii ambayo huna budi kuwa nayo kama unataka kuwa mtu mwenye malezi bora, kwa mfano kushirikiana na wenzako katika misiba na michango mbalimbali ya huduma za kijamii.
Ushauri wa wanajamii pia ni mwingi la msingi ni hili tena, Je, kila linalofanyika kijijini ni la kuzingatia? Je, kwa sababu michango ni muhimu utashiriki kuchangia kuleta mganga wa kienyeji ili awatoe wachawi hasa jirani yako uliyekuwa unamhisi hivyo?
           Mawili haya sawa ila wewe mwenyewe zaidi:
Ni katika msingi huu kuwa si kila kitu wanachotoa washauri au kinachofanywa na jamii ni cha kuzingatia.
Ni yale tu mazuri ndiyo huwa tunayalenga ili yatusaidie kukua katika misingi imara ya malezi.
Makundi hayo hapo juu ni muhimu ila nafasi ya mtu binafsi ni ya muhimu zaidi katika kuwa na malezi imara na endelevu. Kauli nyingi za wale ambao wamejikuta wakifuata makundi haya bila kuwa na maamuzi yao binafsi zimekuwa daima, NAJUTA! SIKUJUA! NILISHAWISHIWA! NIKIMWONA FULANI NATAMANI KUTAPIKA.
Majuto ni mjukuu, daima uwe na sera ya “SAWA, ILA MIMI NAONA HIVI”  yaani jitihada binafsi kupokea ya washauri mbalimbali na jamii husika kisha upime na kufanya maamuzi yako mwenyewe lile ambalo kimsingi litabaki kwako mwenyewe na hutamsingizia mtu.
Maisha ni jinsi unavyoyatengeneza.
FR  SAMUEL MVATI.
NDUNGU PARISH [SAME DIOCESE]


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU