MIAKA 25 YA PAROKIA YA FAMILIA TAKATIFU




Waamini wa parokia ya Familia Takatifu jimboni Sumbawanga wanamshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 25 tangu kupandwa kwa mbegu ya imani parokiani hapo.

Wakizungumza katika sherehe za jubilei hiyo wananchi na waamini wa parokia ya Familia Takatifu wamesema kuwa kanisa katoliki ni nguzo ya maendeleo kwa waamini na wananchi kwa ujumla kwa maeneo mbalimbali.

"Miaka 25 ya parokia ya Familia Takatifu ni ukomavu wa huduma za kiroho na kimwili kwa waumini wake na wananchi kwa ujumla kwani kwa muda huu kumekuwa na shughuli za kijamii ambazo ni msaada kwa watu wote wakatoliki na wasio wakatoliki kama vile shule ya chekechea, mashine za kusaga na kukoboa hali kadhalika kupata mapadri na watawa ni matunda ya parokia hii". amesema ndugu Nolasco Kalikwenda katibu wa parokia.

Akiongoza maelfu ya waamini waliohudhuria misa ya jubilei ya miaka 25 ya parokia ya familia takatifu Askofu wa jimbo katoliki Sumbawanga Mhashamu Damian Kyaruzi amesema kuwa katika mwaka huu wa huruma ya Mungu na jubilei ya parokia, ni vema kuziishi fadhila za kimungu yaani Imani, Matumaini na Mapendo kama ilivyokuwa katika familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosephu.

"Ili kuhusisha maisha wa somo wa parokia hii yaani familia ya Yesu ,Maria na Yosephu na kupitia makuzi ya miaka 25 tangu kupandwa kwa mbegu ya imani katika parokia hii ni vema kuziishi fadhila za kimungu yaani imani, matumaini na mapendo. Na kwa kufanya hivyo mtaweza kulea watoto wenu katika maadili yanayokubalika kama ilivyokuwa kwa mtoto Yesu ambapo itafanya watoto wawaheshimu na kuwasikiliza wazazi wao na kwa namna hiyo jamii ya Sumbawanga na Tanzania nzima hatutakuwa na watoto vibaka, wapiga nondo, wavuta bangi, wahuni na hata walioshindikana hata kwa wazazi wao" Amesema Askofu Kyaruzi.

Aidha Askofu Kyaruzi ameongeza kuwa jina la parokia hiyo ya familia takatifu  limesababisha kiasi cha wengi kushindwa kutambua jina la asili la sehemu ile na kila mtu awe wa imani gani ukimuuliza unakwenda wapi, hana cha kutaja zaidi ya Familia takatifu kwahiyo ni vema familia za kikristo zikalienzi jina hilo pamoja na parokia yao kwa kuhudumia jamii inayozunguka kwa kuyaishi maisha ya familia ya Nazareti.

Parokia ya Familia Takatifu ilianza mwaka 1990 na kuwekwa wakfu tarehe 13 Mei 1990 na Mhashamu Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa.

Katika kipindi cha miaka 25 Parokia hii imeongozwa na Mapadri mbalimbali na kwa vipindi tofauti ambao ni Paroko na mwanzilishi Padri Luka Ville akifuatana na Paroko Hugo, Maparoko hao walisaidiwa na Mapadri Peter Durie, Padri Baisloji na Padri Alois Monsiwenga na Brother Sikeleni.



Walifuatiwa na Maporoko Peter Vander Pass Simchile, Emil Luwaga, Joachim Sangu na sasa anayeongoza ni Padri Leonard Teza akisaidiwa  na Padri Gaudensi Sindani.



Mapadri wengine  waliofanya kazi ya utume  Parokiani hapo ndani ya miaka 25 nao ni Padri Demetrius Kazonde, Padri John Chiwalala, Padri Boniface Nyama na Padri Charles Kasuku.
 Na Emmanuel Mayunga, Sumbawanga







Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU