Kard. Pengo: Bikira Maria ni matumaini ya amani ulimwenguni

Rais wa Radio Maria Tanzania Humphrey Kira akimpokea Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipowasili Makao Makuu ya Radio Maria Tanzania kuzindua Groto ya Bikira Maria. Kushoto ni Mkurugenzi wa Radio Maria Tanzania Padri John Maendeleo (Picha na Pascal Mwanache)


ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa Bikira Maria ni chimbuko la Baraka na matumaini ya amani, siyo tu kwa taifa la Tanzania, bali kwa ulimwengu mzima.
Ameeleza hayo hivi karibuni katika uzinduzi wa Groto ya Bikira Maria, uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Radio Maria Tanzania, Mikocheni, jijini Dar es salaam, na kuwataka waamini kutoka sehemu mbalimbali kutumia Groto hiyo ili kujichotea za Mungu kupitia maombezi ya Mama Maria.
“Natumaini na ni ombi langu kwenu kuwa Grotto hili halitakaa bure. Wale wote tuliopo hapa na wale waliopo popote, mtakapopata nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya Radio Maria Tanzania, msikose kupita hapa kumsalimia huyu Mama. Huyu Mama ni chimbuko la neema, chimbuko la Baraka na ni matumaini ya amani, siyo tu kwa  ajili ya Taifa letu bali kwa ulimwengu mzima. Tumtembelee na tumuombe amani kwa ajili ya ulimwengu wote” ameasa Kardinali Pengo.
Aidha Kardinali Pengo amewashukuru waamini kutoka sehemu mbalimbali ambao wamefanikisha kukamilika kwa Groto hiyo kupitia michango yao ya hali na mali. Ameongeza kuwa hata uwepo wake katika kushuhudia uzinduzi huo umetokana na Baraka za Mungu kupitia kwa Mama Maria.
“Siku ya leo ni ya kumbukumbu kubwa kwa Radio Maria Tanzania na ulimwengu mzima. Tunawashukuru wale wote, waliochangia kwa namna moja ama nyingine kutengeneza Grotto ya Mama Bikira Maria. Mimi  namshukuru Mungu na Mama Maria kwa namna ya pekee ambaye ameniwezesha kuwa hapa pamoja nanyi, kwa sababu kulikuwa na vizuizi na matatizo mengi ambayo yangeweza kunifanya nishindwe kuhudhuria” ameeleza.
Kwa upande wake Rais wa Radio Maria Tanzania, amewashukuru wote waliojitoa na kufanikisha kukamilika kwa Groto hiyo, huku akitoa mwaliko kwa waamini kuitumia Groto hiyo kuomba Baraka za Mungu kw maombezi ya Mama Maria.
“Tunapenda kuwashukuru wote waliojitoa kwa hali na mali katika kufanikiha ujenzi huu. Tunawakaribisha wafike hapa Mikocheni kwa ajili ya kujichotea neema na Baraka za Mungu kupitia Mama yetu Bikira Maria” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Radio Maria Tanzania Padri John Maendeleo amesema kuwa ujenzi wa Groto hiyo umewezeshwa na michango ya waamini kutoka maeneo mbalimbali, huku akitoa rai kwa watu wote kuitumia Groto hiyo kwa ajili ya kuomba Neema na maombezi ya Mama Maria.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU