KUJITEGEMEA HAKUEPUKIKI-KITIMA



Na Bernard James, Dsm
Watanzania wametakiwa kuishi kivitendo falsafa ya elimu ya kujitegemea kama  ilivyojengwa na Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili kuliletea taifa maendeleo ya kudumu kwa vizazi vyote.
Akiongea na gazeti hili jijini Dar es salaam makamu mkuu mstaafu wa chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania  dokta Charles Kitima amesema falsafa(mtindo wa kufikiri) ya elimu hiyo itasaidia kizazi cha sasa na kijacho kujitawala kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na hivyo kudumisha uhuru wa Taifa huru la Tanzania ambapo raia wake huishi kama ndugu.
Amesema Mwalimu Nyerere alihakikisha elimu ya kujitegemea inaleta maendeleo kwa kila aipataye,  kujijengea maaarifa na utaalamu, kutatua matatizo kitaalamu, na ilimfikia kila mtanzania katika eneo lake  pasipo na ubaguzi wowote.
“Tunahitaji falsafa ya elimu ya aina hii kwakweli, ili wasomi  na raia wote kwa ujumla wawe na uwezo wa kufikiri na kupambanua masuala mbalimbali kwa uelewa mpana”. Dokta Kitima amesisitiza.
Amesema japokuwa katika miaka ya 1970 mfumo wa elimu ya kujitegemea ulikuwa na lengo la kumfikia kila mtu na kumwezesha kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini ulipata changamoto kadhaa zikiwemo upatikanaji wa walimu bora na mazingira ya ufundishaji, bado elimu hiyo iliweka misingi bora ya kujenga taifa la watu wanaoamini kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji watu huru, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
“Kipindi kile elimu iliwaandaa watu ili wajitawale, wasaidie kuleta maendeleo na ilitolewa kwa kila aliyestahili jambo lililowafanya wanufaika wa elimu kuhangaika huku na kule kuliletea taifa mafanikio makubwa wakikumbuka kuwa taifa liliingia gharama kubwa kuwasomesha ndani na nje ya nchi”.
Dokta Kitima amesisitiza pia kuwa elimu ya kujitegemea ilihakikisha inamwandaa mwanafunzi ajifunze vizuri ili aweze kumudu maisha na kujipatia mafunzo ya juu tofauti na hali ilivyo sasa ambapo kwa kiwango kikubwa kinachoangaliwa ni ufaulu wa mitihani wa mwanafunzi.
“ Kwenye utawala wa Mwalimu Nyerere wazazi ambao ni wadau wakubwa katika elimu walipewa nafasi na walishirikishwa kupitia uwakilishi unaojali matarajio ya wazazi na watoto katika kuandaa sera na mifumo ya elimu ya watoto wao tofauti na sasa ambapo serikali inasimamia kila kitu na wazazi wakishirikishwa kidogo ama kutoshirikishwa kabisa na ndio maana kila waziri huja na mambo yake. Hii ni kutokana na serikali kutokuzingatia falsafa ya Taifa juu ya kujitawala kwetu” Amesisitiza.
Amepinga vikali tabia ya wasomi wengi wa sasa kukataa kwenda kufanya kazi na kukaa vijijini kuwasaidia watanzania wengi waishio huko akisisitiza juu ya malengo ya kuwatumia wasomi, akikumbusha jinsi Baba wa Taifa mnamo mwaka 1961 wakati wa uanzishaji wa chuo kikuu cha kwanza nchini aliposema ‘ elimu ya vyuo vikuu ilenge kuwatumikia watu, na kwa vile watu wengi wapo vijijini, basi wasomi wajipatie weledi wa kubobea ili kuinua hali ya maendeleo vijijini’.
“Kwa sasa  Serikali inataka maendeleo vijijini, tazama inapeleka pesa nyingi huko ili ziwasaidie wananchi kuinua hali ya maisha  katika kilimo, maji, miundombinu, elimu na afya lakini pesa hizo badala zikasimamiwe na wasomi wetu tuliotumia gharama kubwa kuwasomesha, zinasimamiwa na viongozi katika ngazi za chini kabisa huko vijijini wasio na utaalamu wa kutosha kama wa hawa wasomi wetu, endapo hali hii haitadhibitiwa maendeleo ya vijijini yatakuwa ni ndoto”.
Akizungumzia utendaji wa serikali  ya sasa maoni yake ni kuwa serikali ya Rais John Joseph  Magufuli imeonyesha ishara nzuri za kuirejesha elimu ya kujitegemea mfano harakati za kutatua matatizo katika  sekta ya elimu nchini hasa katika kuweka mazingira rafiki ya watoto kufikia shule ya sekondari na kujifunza, mikopo vyuo vikuu, upatikanaji wa madawati, maabara na kadhalika vyote vimefanyika kwa jitihada kubwa ili kumfanya kila mtanzania apate elimu na imsaidie katika kuliletea taifa maendeleo.
`Pamoja na jitihada hizo, serikali inapaswa kwa umakini na uzalendo kujifunza kushirikisha wadau wa elimu ya msingi na sekondari ili mkazo wa kuwa na walimu wazuri na ufundishaji mzuri wa kumwezesha mwanafunzi kujifunza vizuri(emphasis should be on excellence in teaching and learning)’,aliongezea dokta Kitima.
Cha kuangaliwa ni: je  ufundishaji na  weledi wa waalimu unakidhi vigezo?, mazingira ya kujifunzia ni rafiki?, je, vifaa na vitabu vya kiada, maabara , wanafunzi wa sekondari za kata wanapata mlo wa mchana ili waweze kumudu masomo kwa siku nzima , na je wazazi wanachangia kiasi gani kuisaidia serikali kutoa elimu msingi? Hayo na mengine  vipo vya kutosha?, haya ndiyo yanayotakiwa ili kuifanya falsafa ya hayati Mwalimu ya elimu ya kujitegemea irejee katika historia ya Tanzania.”
Zaidi ya hapo dokta Charles Kitima ametahadharisha kuwa falsafa ya elimu ya kujitegemea ya Baba wa Taifa inaweza kufutika hasa kwa vizazi vijavyo endapo watanzania hawataendeleza kupitia mfumo wa elimu, mambo ya msingi yaliyoliletea taifa uhuru na misingi ya taifa( founding Principles of Tanzania)  iliyolijenga taifa ambayo ni: Mshikamano wa Kitaifa, Umoja na Amani ,Hisitoria yetu ,Utamaduni wetu(mf.lugha ya Kiswahili ) na falsafa ya Kujitegemea.
“ Nchi nyingi zilizoendelea haziwezi kuchezea mambo(founding principles) yaliyozipatia uhuru na kuudumisha, sisi pia tunatakiwa kuienzi misingi hiyo hasa elimu ya kujitegemea, nashauri misingi hii iwekwe katika mitaala ya elimu katika ngazi ya msingi, sekondari na vyuoni,  pia walimu waisome na kuielewa vizuri misingi hii kabla ya kuwafundisha wanafunzi wao”
Dokta Kitima amesema hayati  waziri mkuu Edward Moringe Sokoine alipambana na rushwa na kwa sasa taifa limepata kiongozi mwingine anayepambana na Rushwa na ambaye utendaji wake wa kazi unazingatia misingi aliyoiasisi hayati Baba wa Taifa huku akisisitiza wananchi wampe ushirikiano ili nchi irejee  njia ya kujitegemea na kujenga uchumi wa Taifa kwa kuongozwa na falsafa ya kujitegemea.
“ Tatizo kubwa lililopo nchini mwetu kwa sasa ni watanzania wengi kujali maslahi binafsi badala ya kukuza maslahi ya taifa. Uzoefu dunia kote umeonyesha kuwa maskini wakiwa wengi  matajiri wachache ndani ya nchi hawatafurahia huo utajiri wao. Tabia ya kutanguliza maslahi binafi ama  utamaduni huu hautatufikisha kwenye Tanzania ya mwaka 2025 ya uchumi wa kipato cha kati, kwa kifupi nasema tujenge sekta binafsi ya kitanzania inayoshirikiana na serikali kujenga utajiri wa nchi yetu.”
Makamu mkuu huyo mstaafu wa  SAUT ameshauri pia suala la sekta binafsi ya kitanzania nchini lipewe kipaumbele na liingizwe  kwenye mitaala ili kuliletea taifa mafanikio makubwa kiuchumi kama yalivyo mataifa mengine.
Akigusia mapungufu ya  zamani kitaifa amesema tofauti na miaka ya nyuma ambapo mkazo uliwekwa zaidi kwenye sekta ya umma, sasa ili kuendana na mfumo wa uchumi wa soko huria, taifa haliwezi kuwa tofauti na mataifa mengine, wazalendo wapewe fursa na kuzitumia fursa zilizopo hasa kwenye uwekezaji .  Serikali licha ya kusimamia na kuratibu, pia iweke mazingira mazuri na kuwajengea uwezo kiteknolojia na kimtaji wa wekezaji wa Kitanzania hali ambayo itawajengea raia wanaothubutu uwezo wa ushindani na sekta binafsi za mataifa ya magharibi na Asia.
Pia amesisitiza kuwa hali hii ndio pekee itakayokuza uchumi kwa haraka. Anawaaminisha watanzania kuwa sekta binafsi ya raia unayoratibiwa vizuri na serikali itakuza ajira na uwezo wa ushindani  wa biashara na teknolojia kimataifa.
“ Nchi zilizowekeza katika sekta binafsi za raia wao zimepiga hatua kubwa hasa katika kujitafutia masoko ya bidhaa zao, wananchi kuuza wenyewe katika masoko ya dunia, kuwa na mazao na bidhaa zinazomudu ushindani;   kwa hiyo sisi tusihangaike kutazama wawekezaji wa nje tu kuwa ndiyo  wawekezaji , wakati hata hapa nyumbani wapo wa kutosha tukiwajengea mazingira ya mazuri , hayo yakitiliwa mkazo tutakuwa kama nchi zingine zinazoanza kupiga hatua  mfano  ni Rwanda katika zao la kahawa na maziwa; Kenya katika utalii, chai na usafiri wa anga.
Tanzania ikijipanga vizuri na kurejea kujiamini na kurejesha falsafa ya kujitegemea, tunao uwezo wa kuwa na sekta binafsi ya kitanzania itakayoshirikiana na serikali kushikilia utajiri wa Tanzania, ambao utabaki ndani kwa asilimia kubwa ukirithishwa kizazi hadi kizazi kuliko sasa unaposombwa na sekta binafi za mataifa ya nje. Hivi ndivyo nchi zenye kutumia uzalendo na falsafa ya kujitegemea zilivyofanya na zinavyofanya” , Amesisitiza .
 Amesema “watanzania wengi hawaweki utaifa mbele ndiyo maana kila tatizo la kiuchumi, kisiasa na kijamii lenye kuhitaji utatuzi  utasikia kiongozi akisema ‘tunatafuta mwekezaji  ama mfadhili’. Akaonya falsafa dhaifu ya kujiona ili uendelee lazima mtu atoke nje ya nchi kuja kusaidia haikuwa na nafasi kwenye uongozi wa Baba wa Taifa.
Ni kweli tunahitaji kushirikiana na wengine bali  sisi tukiwa tumeshikilia msingi wa utajiri na uchumi wetu”.
Akihitimisha mahojiano na gazeti hili ameshauri watanzania wanapomkumbuka Baba wa Taifa kila mwaka na kurudia rudia wosia wake kwenye hafla mbalimbali wawe wa kweli kwenye misingi ya utaifa  na hasa kwa yale aliyoyaamini kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni  kama yeye mwenyewe alivyoyaainisha katika hotuba yake ya Mei Mosi 1995, Mbeya.
Ameitaka serikali isikilize maoni ya wazazi, wasomi na vijana katika kurejesha falsafa ya elimu ya viwango na kujitegemea.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU