ZIGO LAKO USIMTWISHE MTU, PAMBANA NALO MWENYEWE
Binadamu tuna hulka ya kuwatwisha watu zigo la lawama pindi
tunapoonekana tumeshindwa kutimiza malengo au wajibu wetu iwe nyumbani ama
katika jamii zinazotuzunguka.
Mifano ipo mingi. Baba katika familia ameshindwa kutimiza
majukumu yake kama baba kwa mama; kumtunza, kumjali, kumheshimu, kumvumilia,
kutosaliti ndoa na zaidi kumpenda kwa dhati. Matokeo yake mama kaona hayo
hayapati kaanza naye kupoteza sifa za “umama” ndani ya nyumba. Mzee kaanza mara
ooh dada zake wanamrubuni, ooh mashoga zake wanamhadaa, ooh wazazi wake ndio
chanzo, ooh kapata mtu mwingine nje ya ndoa n.k.
Kijana hasomi, hajibidiishi, hana machungu na ada na gharama
wazazi au walezi wake wanazotoa ili afaulu vizuri masomo yake. Kutwa yupo
mitandaoni akichati hili na lile, anajiingiza katika mahusiano akiwa mdogo,
anajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, unywaji viroba, mwisho wa siku
anapofeli utasikia aah dingi mnoko, maza anabana, ticha ananifuatilia sana.
Kabla hajapata ajira na baada ya kuteseka sana mtaani
akisaka ajira au kupata unafuu wa maisha, kijana anapata ajira. Na ikumbukwe
kabla hajaipata hiyo ajira aliapa kuwa akiipata kazi ataifanya kwa jitihada
zote ili atimize malengo. Kinyume na hayo, yeye kawa mtu wa kushinda
mitandaoni, kupiga majungu, kuchochea wenzake wagome, uzembe, kutotimiza
wajibu, umbea n.k. matokeo yake kitumbua kinaingia mchanga na hapo utasikia
mara nimerogwa, fulani kanichoma kwa bosi, aagh bosi mnoko na sababu kedekede.
Haya, wengi wetu hatupendi kujishughulisha kutokana na hali
tulizonazo. Wasomi wengi vijana wanataka tu wanapohitimu basi wapate kazi
katika ofisi mbalimbali, wapate mishahara mikubwa, waendeshe magari, wajenge
nyumba, waishi raha mustarehe, si vibaya..lakini je, wanapokosa hizo kazi
wanafanya nini? Hawana njia mbadala. Vijana wengi wapo mitaani hawana ajira
rasmi, kutwa kushinda vijiweni na kujihusisha na tabia mbaya zikiwemo ukabaji,
ujambazi, ulevi, matumizi ya dawa za kulevya n.k, lakini waulize tatizo nini?
Wote hawa watakwambia tatizo Serikali. Ukimwuliza Serikali imefanya nini,
utasikia mara ooh haitupi mitaji, haitupi fursa n.k..kwani serikali ni nani?itawapa
vijana wangapi hiyo mitaji nchi nzima? Mmejiunga katika makundi ikawanyima?
Kama nilivyosema mifano ni mingi. Nionavyo mimi ni kuwa
kumbe kabla hujapata muda wa kumnyooshea mtu kidole kuwa yeye ndio chanzo cha
wewe kutofanikiwa katika jambo fulani, jitathimini kwanza wewe, je upo sahihi?
Mara unapoona mambo hayaendi vizuri shuleni, nyumbani,
kazini, katika jamii na sehemu zingine ambazo wewe unahusika nazo kila siku,
usimtafute mchawi kwanza. Chukua muda wa kutosha, kaa peke yako katika eneo
tulivu kabisa bila kumshirikisha mtu yeyote yule. Tafakari kwa kina
(meditation). Ongea na hisia zako tu huku ukimshirikisha Mungu tu. Jiulize mara
nyingi kuwa hao watu unaowatwisha zigo la lawama ghafla wakitoweka katika
maisha yako utafanikiwa zaidi au ndio mwisho wako utakuwa umefika?
Nionavyo mimi mchawi wa mtu ni yeye mwenyewe. Hivyo, jenga
utaratibu wa kukaa na kufanya meditation na kujiuliza nakosea wapi? Fukuza
kabisa hisia za kumtaja mtu katika sababu za wewe kutofanikiwa.
Na ndio maana wataalamu wa afya mara nyingi wanashauri kuwa
unapopata tatizo katika maisha, tulia kwanza. Chukua muda wa kutosha
kulitafakari kwa kina. Kwa namna hiyo tena katika hali ya utulivu mkubwa
utafahamu chanzo (kama ni wewe) na utatabasamu sababu njia ya kulimaliza tatizo
hilo yawezekana ni rahisi mno.
Kwa kufanya hivi hakika utaishi kwa furaha huku kila kitu
unachopanga ukiona kinafanikiwa. Na utaondoa uwezekano wa kupata magonjwa
mbalimbali hasa shinikizo la damu.
Na; Bernard James
Comments
Post a Comment