SIKU YA VIJANA DUNIANI 2019: MAENEO YATAKAYOTUMIKA YABAINISHWA


Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama, anasema Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanayoongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Tayari, Baraza la Maaskofu Katoliki Panama limebaini maeneo makuu yatakayotumika katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Vijana wameanza kuwasha joto miongoni mwa vijana wenzao kwa kuandika nembo pamoja na wimbo maalum utakaotumika kwa ajili ya maadhimisho hayo, ambayo kimsingi ni sehemu ya mbinu mkakati wa Mama Kanisa, katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Eneo lililochaguliwa ni “Cinta Costera”, maana yake mji ulioko kwenye “Ukanda wa Ufukwe wa Bahari”. Hili ni eneo linalopambwa kwa rangi ya kijani na mazingira yanayovutia hata kwa macho! Eneo lililokubalika linakidhi vigezo msingi kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa mahujaji watakaohudhuria maadhimisho haya, sanjari na kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ulinzi na usalama wa kutosha pamoja na utunzaji bora wa mazingira, mambo ambayo pia yametiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta nasema, idadi kubwa ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini inaundwa na vijana wa kizazi kipya, lakini kwa bahati mbaya sana, wengi wao wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira, hawa ndio ambao Kanisa linataka kuwaonjesha huruma ya Mungu kwa njia ya sera na mikakati makini ya utume wa vijana.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI