"VIJANA WAJIKABIDHI KWA BIKIRA MARIA"
VIJANA wanaopokea Sakramenti ya
Ekaristi takatifu wameshauriwa kujiweka katika tunza ya Bikira Maria ambaye ni
tabenakro ya kwanza ya Kanisa hasa wakati huu Kanisa Katoliki ulimwenguni kote
linapokaribia kuingia katika mwezi wa rozali takatifu ili mama Maria aweze
kuwaombea katika maisha yao.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na
paroko wa parokia ya Mwili na Damu padri John Greyson katika ibada ya kutoa
sakramenti ya Ekaristi takatifu kwa vijana 64 iliyofanyika katika Kanisa la
Mwili na Damu lililopo Kola jimboni Morogoro.
Padri Greyson amesema kuwa ibada ya
rozali takatifu ni msingi wa Kanisa ambao unamwezesha muamini kuungana na Yesu
Kristo katika sala mbalimbali za Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria mama wa
ekaristi takatifu ili kupata neema ya utakataso.
Aidha padri Greyson ameyataja baadhi
ya mambo yatakayowawezesha vijana hao kuungana na Yesu Kristo mojawapo ikiwa ni
matendo ya huruma kwa kuwasaidia wahitaji, kujimega kama Yesu alivyojimega kwa
ajili ya ukombozi wa mwanadamu.
“Msiache kuwa na ibada kwa mama huyu
mwenye huruma awaombee na kusisitiza hilo nitampatia kila mmoja rozali
tano muwasisitize wana familia muungane nao katika kusali rozali takatifu,
nawakumbusha msiache kuungama mnapoanguka dhambini, mnapoteza mastahili ya
kupokea sakramenti ya ekaristi takatifu, ili kupata mastahili hayo lazima
kupata sakramenti ya kitubio, hayo ndio maisha ya Ekaristi zingatieni hayo,”
amesema padri Greyson.
Wakati huohuo padri Greyson
amewahimiza wazazi na walezi wa watoto hao kuwasaidia na kuchochea imani ya
Kanisa Katoliki katika familia zao, kwa kuwakumbusha kuwa Kristo ndiye tumaini
lao na Mungu ndiye msaada katika maisha yao yote, waendelee kuungana na Mungu
kamwe wasimuache kwa kuishi nje ya mafundisho ya Kanisa.
“Ndugu zangu wazazi na walezi watoto
hawa wamejifunza mambo mengi ya kiimani na mazuri, na mimi ninawaomba
muwasisitize wazingatie imani ya Kanisa Katoliki kama dira ya maisha yao,
wajifunze hayo yote kwa kuona mifano adilifu ya maisha yenu, kwa maombezi ya
mama Bikira Maria mama wa ekaristi takatifu awape nguvu wasipoteze huo
muunganiko kwa kusaidiwa na ninyi wazazi,” amesema padri Greyson.
Comments
Post a Comment