VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUWAPIGA VITA WAVUNJA AMANI NCHINI
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaomba
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi zote za kidini nchini wahakikishe
wanawapiga vita watu wote wanaopanga na kutaka kuvuruga amani na utulivu
uliopo nchini kwa sababu watakwamisha maenendeleo.
Amesema
Serikali inaelewa kwamba dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya
maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu kwani inatoa elimu ya maadili mema
yenye kuwafanya waumini waepukane na maovu mbalimbali.
Majaliwa
ametoa kauli hiyo Oktoka 01, 2017 wakati akifungua mkutano Mkuu wa
mwaka wa 48 wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya uliofanyika katika eneo
la Kitonga kata ya Msongola wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Amesema
kila Mtanzania anatakiwa ahakikishe anadhibiti matukio yote yenye
viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutoa taarifa katika mamlaka
husika.”Tanzania ni nchi salama na yenye utulivu, hivyo ni lazima wote
tushirikiane kuitunza.”
“Napenda
niwahakikishieni kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za Jumuiya za
kidini katika kupiga vita maovu ya kila aina; mathalan utumiaji wa dawa
za kulevya, wizi, rushwa, uzinzi ambao husababisha madhara mengi ukiwemo
ugonjwa wa UKIMWI.”
Amesema
iwapo dini zetu zitatumika vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza
agizo la Rais Dkt. John Magufuli la ‘Hapa kazi tu’ kwani kila mtu
ataepuka uzembe na kuwajibika ipasavyo.
Majaliwa
amesema ana imani kwamba jumuiya hiyo kama zilivyo taasisi zingine za
kidini itaendeleza kazi kubwa ya kupambana na maovu katika jamii yetu
kwa kuwapatia waumini wao na wananchi kwa ujumla elimu na maarifa ya
kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho.
Amesema
amani na utulivu uliopo nchini unatokana na mambo mengi ikiwemo na
wananchi kupata ustawi, kuweza kufanya shughuli zao vizuri na kuwa na
imani na Serikali yao, ambayo imejiwekea mikakati ya kuhakikisha
wananchi hususan wanyonge wanapata faraja ndani ya nchi yao.
Amesema
mambo yameweza kupatikana baada ya Serikali kupambana na rushwa na
ufisadi pamoja na kuimarisha maadili ya watumishi wa umma, ambayo
vimekuwa ni vyanzo vya kupotea kwa amani na utulivu katika baadhi ya
nchi.
“Serikali
imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ufisadi, kupitia mikataba
mibovu na kuimarisha maadili ili kujenga imani kwa wananchi, kuondoa
migongano na tofauti ya kipato, kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali za
umma, kuleta tija kwa kuongeza thamani ya huduma na kudhibiti mianya ya
upotevu wa mapato.”
Kabla,
Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Tanzania,
Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry amesema Jumuiya hiyo imekuwa ikifanya
mikutano kila mwaka kwa lengo la kukumbushana misingi sahihi ya dini
tukufu ya kiislam pamoja na kukuza undugu wao.
Sheikh
Chaudhry amesema mkutano wa mwaka huu umejumisha watu zaidi ya 4,000
kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wageni kutoka
nchi za Uingereza, Canada, Rwanda, Uganda, Ujerumani, Kenya, Burundi,
Malawi na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Amesema
Jumuiya hiyo mbali na masuala ya kidini pia inatoa huduma mbalimbali za
kijamii kama elimu, maji na afya kwenye mikoa tofauti tofauti nchini.
Comments
Post a Comment