ASKOFU MFUMBUSA AANDIKA REKODI KONDOA
ASUBUHI na Mapema ya siku ya
Jumapili ya tarehe 15/10/2017 katika Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki Kondoa
Mkoani Dodoma, palifurika waamini kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya
wilaya, ndani na nje ya Nchi kuja kujionea namna upendo wa Mungu unavyofanya
kazi kwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa Mhashamu Bernardin Mfumbusa
aliyetimiza miaka 25 ya Upadri.
Misa iliyoambatana na maandamano
yaliyofanywa na Maaskofu, Mapadri pamoja na wageni wengi waalikwa kuanzia
katika bustani ya uaskofu na kuelekea kanisani, imefanyika katika Kanisa Kuu la
Jimbo na kuwashirikisha waamini wengi wakiwemo Maaskofu, Mapadri, Washangwera,
viongozi wa Serikali pamoja na viongozi wa Siasa.
Washiriki wa adhimisho hilo la kihistoria
kwa wakati tofauti walipata fursa ya kutoa salamu mbalimbali huku wakiuongelea
utume wa Askofu Mfumbusa.
Katibu Mkuu Shirikisho la wanachama
Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati (AMECEA), Padri Ferdinand Lugonzo
kutoka nchini Kenya amesema kuwa amefurahi sana kushiriki sherehe hii na
kumpongeza Askofu kwa hatua aliyoifikia.
"Nimefurahi kushirikiana nanyi
katika sherehe hii, nawapongeza sana, hii inadhihirisha ukaribu uliopo
kati ya Askofu, watumishi na waamini. Niseme mmebarikiwa sana kwa
sababu Askofu wa Jimbo hili ni mtu wa kufanya kazi kwa ukaribu na kila mtu. Kwa
muda wote amekua akifika katika ofisi za AMECEA Kenya, na kuuliza ni lini
tutafika jimboni Kondoa? Amekuwa akiniambia kuwa Kondoa kuna River Side (
Kando ya Mto), ni kweli nimefika na nimejionea Kondoa namna ilivyo,"
Amesema Padri Lugonzo.
Ameongeza kwa niaba ya wenzake
waliofuatana naye kuwa "Tunaposherehekea maadhimisho haya lazima tumshike
mkono kwa kazi alizofanya, niseme asante sana kwa nafasi hii niliyopewa kwa
kusema chochote kwake."
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora,
Mhashamu Paulo Ruzoka, amesema kuwa uthibitisho wa mahudhurio ya Maaskofu
kutoka katika majimbo mbalimbali yakiwepo Mpanda, Geita, Singida, Mahenge
pamoja na Kigoma pia Washangwera waliosoma Seminari za Tabora, Segerea
pamoja na Songea ni ushahidi kuwa Askofu Mfumbusa ni mtu wa kuigwa kwa
ushirikiano alioufanya katika kipindi chake cha miaka 7 ya kuliongoza Jimbo
Katoliki Kondoa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Walei Jimbo, Tius Justine amesema kuwa pamoja na kumpongeza Askofu, Jimbo hilo limetoa
fedha kiasi cha milioni kumi na moja, laki saba na elfu kumi na tatu na sabini
(11, 713, 70) kumuunga mkono, fedha ambazo zimeelekezwa katika shughuli za
maendeleo katika parokia mbalimbali ndani ya Jimbo.
“Ni ukweli usiopingika kuwa tangu
Askofu awepo jimboni hapa tumeona maendeleo makubwa yakiwa ni pamoja na kuwepo
kwa bustani ya nyanya, ufugaji wa kuku wa mayai, bwawa la samaki pamoja na
kuanzishwa kwa mahali pa kupumzikia ambapo ni kandokando ya mto Mkondoa (RIVER
SIDE). Pamoja na yote, mafanikio mengine
ni kuanzishwa kwa parokia mpya ambazo ni Parokia ya Soya, Kidoka, Gonga, Lalta
pamoja na tunayotarajia hivi karibuni parokia ya Chemba," amesema Justine.
Wanenavyo
Waamini
Naye Valenina Joseph Mkazi wa
Tanesko amekiri kwa kusema kuwa jitihada za Askofu zimeonekana kwa haraka
pamoja na ukweli kuwa ni muda mchache amelitumikia Jimbo Katoliki Kondoa, hivyo
ni shukrani za kipekee kwa Mungu kumleta mtumishi mwenye roho ya kipekee.
Godhard Hunja, Mkazi wa Kilimani
amesema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kwani Askofu Mfumbusa ana maono ya
mbali, kwa jambo kama hili ni kumshukuru Mungu kwani kwa muda mrefu kama huo
kwa kumtumikia Mungu kwa kutoa huduma, ni kwa kuongozwa na Mungu.
Shukrani
za kipekee
Askofu Bernardin Mfumbusa licha ya
kuwashukuru wote Mwenyezi Mungu pamoja na wote waliohudhuria adhimisho hilo, amesema
kuwa miaka 25 iliyopita walikua 36, katika safari moja lakini leo wamebaki
27, na 9 kati ya hao wameaga Dunia.. "Niseme Ahsanteni sana kwa
namna ya kipekee namna mlivyoonesha upendo mkubwa mbele za Bwana, leo katika
safari yetu ya mapadri 36 tumebaki mapadri 27, wenzetu 9 wametangulia,"
amesema Askofu Mfumbusa.
Utume mwema
ReplyDelete