MWONGOZO WA MALEZI YA KIPADRI: MABORESHO


Baba Mtakatifu Francisko anasema, malezi na majiundo ya kipadre kwanza kabisa ni kazi ya Mwenyezi Mungu ambayo inamtaka jandokasisi au Padre kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumfunda kadiri anavyotaka! Pili, Kasisi mwenyewe anapaswa kutambua kwamba, ni mhusika mkuu wa majiundo katika wito, maisha na utume wake wa kipadre. Tatu, wadau wakuu wa malezi ni walezi waliopewa dhamana hii kwa kusaidiana na Maaskofu huku wakitambua kwamba, wito unazaliwa, unakua na kukomaa ndani ya Kanisa ambaye ni mama na mlezi wa miito yote mitakatifu!
Baba Mtakatifu Francisko,ameyasema hayo, Jumamosi, tarehe 7 Oktoba 2017 wakati alipokutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Kimataifa juu ya Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”, wakati wa kuhitimisha Kongamano hili, lililofunguliwa, Alhamisi, tarehe 5 Oktoba 2017 huko Castel Gandolfo. Wajumbe wa Kongamano hili wamefafanuliwa kwa kina na mapana sababu ambazo zimepelekea Mama Kanisa kuamua kuandika Mwongozo Mpya wa Malezi ya Kipadre.
Kwanza kabisa, Kanisa linapenda kukazia malezi na majiundo ya Mapadre wake katika uhalisia wa maisha na utume wao katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ili kusoma alama za nyakati na hatimaye, kutoa majibu muafaka kwa maswali magumu ya maisha na changamoto za kila siku, tayari kuwajengea Mapadre matumaini thabiti katika maisha na utume wao miongoni mwa familia ya Mungu, kwa kutambua kwamba, wao ni mitume wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko.
Askofu mkuu Joèl Mercier, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Wakleri amepembua kwa dhati kabisa: dhamana na wajibu wa walezi wa maisha, utume na wito wa kipadre ndani ya Kanisa. Hii ni dhamana nyeti inayopaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa ndani ya Kanisa, ili kupata mapadre watakaojisadaka bila yakujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Kanisa linawahitaji mapadre: wema, watakatifu na wachamungu; wanaoweza kutambua changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zilizoko katika maisha, tayari kuzifania kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu wanaowahudumia kwa moyo, akili na nguvu zao zote!
Majiundo ya mapadre ni dhamana ya Kanisa ambaye ni mama na mwalimu anayependa kutumia rasilimali watu, muda na vitu ilikufanikisha azma hii. Utekelezaji wa majiundo na malezi ya kipadre ni sehemu ya maisha ya Jimbo au Shirika husika, kila mtu kadiri ya dhamana na nafasi yake ndani ya Kanisa, Ni dhamana inayojielekeza katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji na miito kijimbo; malezi makini ya awali na endelevu seminarini na kwenye nyumba za malezi. Hapa dhana inayopewa msukumo wa pekee kwa wakati huu: ni Jumuiya inayounda na kudumisha malezi; kwa kushirikiana na kukamilishana kwani wote hawa wanategemeana katika makuzi ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kiakili na katika shughuli za kichungaji.
Kwa upande wake Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Wakleri upande wa Seminari anasema, Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” unafafanua mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Makanisa mahalia katika mchakato wa malezi na majiundo ya kipadre. Ni mwongozi makini unaotoa sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa katika hija ya malezi ya majandokasisi na mapadre kama sehemu ya majiundo endelevu. Mkazo umewekwa katika majiundo ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; umuhimu wa maisha ya Kisakramenti; Mafundisho Tanzu ya Kanisa bila kusahau malezi  na majiundo ya kiakili, kiutu na kichungaji kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.
Ni mwongozo ulioboreshwa zaidi kwa kusoma alama za nyakati sanjari na kujikita katika Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ikilinganishwa na Mwongozo wa Malezi ya Kipadre wa Mwaka 1970. Kuna mabadiliko makubwa katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mambo yanayoathiri tamaduni za watu na uelewa makini wa Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kina, uzoefu na mang’amuzi katika maisha, utume na wito wa mapadre kutoka kwa Makanisa mahalia mintarafu malezi na majiundo ya kipadre. Ni mwongozo ambao umeandaliwa na wataalam mbali mbali wa maisha na utume wa Kanisa, ili kumwezesha Mama Kanisa kupata mapadre makini katika maisha na utume wake.
Huu ni mwongozo ambao umepokelewa kwa mikono miwili na mapadre wa kizazi kipya, wanaohitaji zaidi maboresho katika maisha yao ya kiroho na kiutu; kielimu na kichungaji. Inafurahisha kuona kwamba, Maaskofu wengi, wameamua kutumia Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” kuwa ni mwongozo rejea katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao katika malezi na makuzi ya miito ya kipadre! Kwa hakika, mwongozo huu unazima kiu ya malezi na majiundo ya maisha, wito na utume wa kipadre; muhimu sana kwa Makanisa mahali na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI