USIFIKIRIE UZEE, FIKIRIA KUISHI
OKTOBA Mosi ya kila
mwaka ni siku iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa kuadhimisha uwepo wa wazee
katika jamii kote ulimwenguni. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi Oktoba 1,
1991 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu mambo yanayowalenga wazee ikiwemo
kutoheshimu haki za wazee, kutazama mahitaji na maslahi ya wazee na kuhakikisha
mzee popote alipo ulimwenguni anapata huduma za msingi za kijamii kama vile
huduma bora za afya.
Maadhimisho ya siku ya
wazee duniani ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN)
katika kutambua na kuhamasisha jamii
kuweza kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote.Umoja wa Mataifa umetenga
siku hii kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili;
na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi
maisha ya heshima, hadhi, na kuthaminiwa utu wao.
Siku hii inaakisi mila
na desturi nzuri za kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndiyo chanzo cha
urithi wa historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, watu wenye hekima, na
walezi katika jamii. Hivyo jamii inao wajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee
katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua pale ambapo
mzee ananyanyaswa au kutendewa isivyostahili.
Wazee wapewe mafao yao
kwa wakati kwakuwa ni nguvu kazi yao na ni haki yao, lakini uzee si mwisho wa
maisha. Uzee si mwisho wa kufanya maendeleo. Uzee si mwisho wa ndoto ya
mafanikio. Mtu mmoja alipostaafu kazi kwa mtazamo wake baada ya kupata mafao
alianza kutapanya mafao yake.
Alifanya sherehe,
alifanya starehe za kila aina, aliwafurahisha watu mbalimbali kwa pesa yake
akidhani yeye anakaribia kufa kwa sababu kustaafu ni uzee, hivyo kwa nadharia
yake na mapokeo yake ya kidunia aliamini ukiitwa mzee unasubiri kufa. Mwezake
aliyestaafu naye baada ya kupata mafao alijiwekeza kibiashara. Yule
aliyefikiria kufa alishangazwa miaka ikienda lakini ‘hakioni’ kifo.
Wakati huo akiwa na
hali mbaya ya aibu mtaani, alimtafuta rafiki yake aliyestaafu naye na alipompata
alimkuta akiwa tajiri mkubwa anayetegemewa katika Wilaya fulani. Alishangaa,
lakini alisaidiwa kiuchumi naye akawa mfanyabiashara.
Uzee si kufa wala uzee
si ugonjwa ama uzee si uchawi. Uzee ni umri si mvi. Siku hizi hata vijana
wanaota mvi. Siku hizi baadhi ya vijana wanaonekana wazee na wazee wanaonekana
vijana. Jambo hili linatokana na mazingira ya wakati na mtindo wa maisha. Kuwa
mzee si kwamba huwezi kufanya kazi. Usifikirie uzee ni kifo, bali fikiria
kuishi.
Yoshiharu Shiozaki wa
nchini Japani, mwenye umri wa miaka 73, anafanya kazi ya kushauri wale
wanaotaka kununua au kuuza ardhi au nyumba anasema hivi: “Ninatambua kwamba ili
niwe na afya nzuri ni lazima nifanye mazoezi kwa ukawaida. Nimekuwa nikitunza
bustani ndogo kwa muda wa miaka michache iliyopita.
Ninajisikia vizuri sana
baada ya mazoezi hayo. Ili nitimize mengi iwezekanavyo nimejitahidi kufuata
kanuni hii: ‘Kusitasita ni mwizi wa wakati; na kuahirisha mambo ni msaidizi
wake.” “Ninatambua kwamba ili niwe na afya nzuri ni lazima nifanye mazoezi kwa
ukawaida.” “Nina maumivu ya kiuno, msukumo mkubwa wa damu, na ugonjwa wa
masikio. Ninasafiri kwa baiskeli kutoka nyumbani hadi ofisini siku nne kila
juma; kwenda na kurudi ni umbali wa kilometa 12.
Mazoezi hayo ni mazuri,
kwa kuwa hayaumizi mgongo wangu lakini huimarisha misuli yangu ya miguu.
Ninajitahidi kuishi kwa amani pamoja na wengine hasa majirani. Ninajitahidi
kutozingatia udhaifu na makosa ya wengine. Nimetambua kwamba watu huitikia
upesi wanapotiwa moyo kuliko wanapochambuliwa.” ‘Ninajitahidi kutozingatia
udhaifu wa wengine.’
Endapo kila mtu
angepewa nafasi ya kueleza nini maana ya uzee angesema vile anavyofikiria. Wengine
wangesema uzee ni kukunjamana kwa ngozi, uzee ni kuwa na mvi nyingi, uzee ni
kuwa na hekima, uzee ni kutembelea fimbo, uzee ni kuwa na macho mekundu, mzee
ni yule anayepinga mabadiliko ya kijamii, uzee ni ugonjwa, mzee ni yule
anayeshindwa kutembea na wengine wangesema kustaafu kazi ni uzee.
Wengi hudhani kwamba
wazee wengi hutegemea watu wengine. Hiyo si kweli. Gazeti la The New York Times
Magazine lilisema kwamba nchini Marekani, ‘wazee wengi wanaojitegemea ni watu
wa tabaka ya kati katika jamii ambao wana fedha nyingi, na watu wanaochunguza
jamii wametambua kwamba idadi ya wazee wenye nguvu walio matajiri inaongezeka.’
Hekima ya wazee inaonwa
kuwa yenye thamani kubwa katika jiji la Troyes huko Ufaransa na mahali
penginepo. Hekima hiyo inafaidi watoto wanaofundishwa na wazee ufundi kama vile
useremala, kutengeneza kioo, kukata mawe, ujenzi, na ufundi wa mabomba baada ya
shule.
Bila shaka, furaha yetu
ya uzeeni inaweza kuathiriwa kwa sababu ya ubaguzi na maoni ya wengine, lakini
kwa kawaida inaathiriwa pia na mtazamo wetu. Wewe mwenyewe unaweza kufanya nini
ili uwe mtendaji, kimwili na kiakili, hata ingawa mwili wako unazidi kuzeeka?.
Utaona kwamba wazee hao
wote wanaendelea kufanya kazi ama kazi ya kuajiriwa ama ya kujitolea. Ukweli
usiofurahisha ni kwamba, sasa hivi unaposoma habari hii wewe pia unaendelea
kuzeeka. (Mhubiri 12:1) Hata hivyo, kwa hekima utatii maneno haya ya gazeti la
Bulletin of the World Health Organization: “Kama vile afya nzuri inavyomwezesha
mtu kuwa mtendaji, ndivyo utendaji unavyofanya mtu awe mwenye afya.”
Comments
Post a Comment