PAPA FRANSISKO: VIJANA TAFUTENI ELIMU, MATUMAINI NA AMANI


Chuo kikuu ni maabara ya ubinadamu na mahali pa majadiliano ya kisayansi, yanayojikita katika mchakato wa kumfunda mwanadamu na kumpatia utambulisho wake wa ujumla na katika ujenzi wa Jumuiya ya mwanadamu. Ni mahali ambapo wanafunzi huku wakiwa wamemzunguka mwalimu wao, wanajipatia ujuzi, maarifa na elimu, tayari kushirikisha tunu hizi msingi katika uhalisia wa maisha yao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Chuo kikuu ni mahali panapowakutanisha watu wote pasi na woga wa watu kuchanganyikana.
Huu ni ushuhuda unaotolewa na watu mbali mbali ambao wamebahatika kufundwa katika Chuo kikuu cha Bologna, kilicho kaskazini mwa Italia. Hawa ni watu waliotoka ndani na nje ya Italia, daima wakiongozwa na kauli mbiu iliyowataka kujikita katika mambo msingi yanayowaunganisha kama wasomi! Chuo kikuu cha Bologna, kimekuwa ni makutano ya mahusiano ya watu katika kukabiliana na changamoto za maisha na kwamba, mfumo wa Elimu wa Erasmus unaweza kuendeleza jitihada hizi za wito wa elimu katika jamii!
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumapili, tarehe 1 Oktoba 2017 wakati wa hija yake ya kichungaji Jimboni Cesena kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 300 tangu alipozaliwa Papa Pio VI na Jimbo kuu la Bologna, kama sehemu ya kufunga Kongamano la Ekaristi Kijimbo. Baba Mtakatifu huku akiwa amezungukwa na umati mkubwa wa ulimwengu wa wasomi kwenye Uwanja wa Mtakatifu Bosco, Jimboni Bologna, amekazia kwanza kabisa haki elimu, inayopata chimbuko lake katika ubinadamu na hivyo kuwa ni ushuhuda wa mfumo wa elimu Barani Ulaya, ambao umechangiwa na serikali pamoja na Kanisa, kila taasisi ikijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake.
Bologna ni mahali ambapo pamekuwa ni kivutio kikuu cha wanafunzi kutoka ndani na nje ya Italia, wanaotamani kujifunza Sheria za Kanisa na Kijamii. Kati ya wasomi wanaokumbukwa kutoka katika Chuo kikuu cha Bologna ni Mtakatifu Dominico, aliyebahatika kujifunza kitabu cha upendo, yaani Maandiko Matakatifu ambayo ni chemchemi ya ujuzi na maarifa ya kila aina. Utafiti wa mafao ya wengi ni ufunguo wa mafanikio ya wanafunzi, chachu muhimu sana ya elimu na ujuzi, unaojikita katika haki msingi za binadamu. Mambo makuu matatu, yanapaswa kupewa uzito wa pekee anasema Baba Mtakatifu Francisko ambayo ni: haki ya kitamaduni, haki ya matumaini na haki ya amani!
Haki ya utamaduni na elimu ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani kuna vijana wengi sehemu mbali mbali za dunia, hawana nafasi ya kusonga mbele katika masomo, hali ambayo inakwamisha matumaini yao kama binadamu. Vijana wawe na uvumilivu, juhudi na bidii katika masomo, ili kuweza kupata maana halisi ya maisha, kuliko kutafuta njia ya mkato inayowatumbukiza katika ulaji wa kitamaduni! Vijana wawe imara na thabiti kufanya maamuzi mazito katika maisha; kwa kujikita katika tafiti, maarifa, ujuzi na hatimaye, kushirikishana na wengine amana hii katika maisha yao, tayari kwa ajili ya huduma makini kwa jami. Mzizi neno wa utamaduni anaendelea kufafanua Baba Mtakatifu, unawawezesha kukuza utu wao kama binadamu, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Vijana waendelee kujisadaka kwa ajili ya kutafuta ujuzi na maarifa yatakayosaidia kusongesha mbele maendeleo endelevu ya binadamu!
Baba Mtakatifu anawataka vijana kudumisha haki ya matumaini dhidi woga usiokuwa na mvuto wala mashiko; chuki na uhasama; au kutafuta umaarufu usiokuwa na tija; vijana waondokane na hali ya kukata na kujikatia tamaa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kutambua kwamba, katika maisha, kuna mambo mema na mazuri na ambayo yanadumu; haya ni mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga, kwa kujikita katika upendo wa dhati na kwamba, ajira ni haki ya wote, ahadi ambayo inapaswa kutekelezwa. Itapendeza anasema Baba Mtakatifu Francisko, ikiwa kama vyuo vikuu vitakuwa ni maabara ya matumaini kwa vijana, yanayowawajibisha kwa ajili ya utunzaji wa nyumba ya wote, kila kijana ana uwezo wa kuwa ni chombo cha ujenzi wa matumaini kwa wengine!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, haki ya amani ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu inashinda na kuvuka ghasia na kinzani. Mwaka 2017, Jumuiya ya Ulaya imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 ya Mkataba wa Roma, ulioanzishwa kwa makusudi mazima, ili kulinda na kudumisha haki ya amani na umoja wa Bara la Ulaya. Vijana wanapaswa kuendeleza ndoto ya umoja na amani iliyoanzishwa na waasisi wa Umoja wa Ulaya kwa kuondokana na vita isiyokuwa na mashiko wala mvuto! Kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Katika changamoto ya haki ya amani, Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa ajili ya ujenzi wa amani, maridhiano pamoja na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa.
Biashara ya silaha duniani inawanufaisha wajanja wachache kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia! Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa na wote; kuna kuwepo na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Bara la Ulaya linapaswa kuwa ni kielelezo cha Mama mwema anayethamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; Mama anayetoa matumaini kwa watoto wake; Ulaya inayojikita katika ukweli na haki; uzuri na wema; utamaduni na maisha ya kawaida; mahali ambapo vijana wanaweza kufunga ndoa na wakibahatika kupata watoto, wana wawajibikia katika elimu na malezi kwa kutambua kwamba, watoto ni furaha ya familia na wala si chanzo cha matatizo na ukosefu wa fursa za ajira. Baba Mtakatifu Francisko anatamani kuona Chuo kikuu cha Bara la Ulaya, kikiwa ni alama ya Mama mwema, anayekumbuka utamaduni wake unaofumbatwa katika matumaini kwa ajili ya watoto wake na amana ya amani duniani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI