WASIFU WA HAYATI BABA ASKOFU CASTORY MSEMWA WA JIMBO KATOLIKI TUNDURU-MASASI



BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA

WASIFU WA BABA ASKOFU CASTORY PAUL MSEMWA WA JIMBO KATOLIKI TUNDURU-MASASI

Tarehe 19.10.2017 saa saba mchana Mungu amemwita katika Makao yake Mtumishi wake Baba ASKOFU CASTORY PAUL MSEMWA.

Baba Askofu Castor Paul Msemwa alizaliwa tarehe 13.02.1955 katika kijiji cha Kitulira wilaya ya Njombe.

Alisoma shule ya awali Kitulira kisha kuhamia Shule ya Msingi Matola alikohitimu masomo ya Msingi mwaka 1973.

Mwaka 1974 alijiunga na  seminari ndogo ya Mafinga – na kumaliza kidato cha nne mwaka 1977. Mwaka 1978 alijiunga na  seminari ya Likonde –Mbinga na  kuhitimu masomo ya kidato cha sita mwaka 1980 mwezi wa sita.

Mwezi wa saba mwaka huo huo 1980 alijiunga na jeshi la kujenga taifa katika kambi ya Mlale- Songea. Akiwa jeshini alijishughulisha sana na mambo ya sanaa na michezo hadi alipohitimu mafunzo yake mwezi Julai mwaka 1981.

Mwaka huo huo wa 1981 mwezi Julai  alijiunga na masomo ya Seminari Kuu Peramiho akianza na masomo ya Falsafa kwa muda wa miaka miwili na kisha akaendelea hapo hapo na masomo ya Teolojia  na kuhitimu mwezi Mei mwaka 1987.
Tarehe 07/06/1987 alipewa daraja ya upadri katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Njombe na Mhashamu Askofu Raymond Mwanyika.

Mara baada ya upadri alifanya kazi ya Kichungaji katika Parokia ya Njombe kwa muda wa miaka mitatu na nusu kabla ya kutumwa kwenda kufundisha Seminari Kuu Peramiho mwaka 1991. Alifundisha masomo ya maisha ya kiroho  kwa muda wa miaka miwili na nusu.

Mwaka 1993 mwezi wa nane, alikwenda Roma kwa ajili ya  masomo ya juu ya maisha ya kiroho. Kwa muda wa miaka miwili alichukua masomo ya maisha ya kiroho katika chuo cha Mtakatifu Teresia wa Avila  mjini Roma. Mwaka 1995 mwezi Juni alitunukiwa shahada ya pili katika maisha ya kiroho.

Mwaka 1995 mwezi Oktoba alijiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmo katika mji huo huo wa Roma ambapo alichukua masomo ya kiroho ya kitawa hadi mwaka 1997 mwezi wa sita alipohitimu kwa kutunukiwa shahada ya pili.

Mara baada ya kumaliza masomo yake alirudi mara moja jimboni kwake Njombe na kupangiwa kuwa mwalimu wa kuwaandaa vijana wanaokwenda kujiunga na Seminari kuu Peramiho. Alifanya huduma hiyo katika Parokia ya Kifanya.

Mwaka 1998 mwezi Oktoba alihamishwa kutoka Kifanya na kuwa mlezi wa kiroho na Mwalimu katika nyumba ya Masista Imiliwaha, Jimboni Njombe. Alikuwepo pale takribani muda wa miaka saba hadi mwaka 2004.

Akiwa Imiliwaha alifanya kazi zilizohusiana na nyumba  ya Masista, miradi mingi ya watawa ilishauriwa naye hususani ujenzi  wa shule ya sekondari ya kwanza ya Masista. Vile vile alijishughulisha na miradi ya maji shirikani na vijiji vinavyoizunguka Imiliwaha.

Tarehe 08/12/2004 Baba Mtakatifu, Yohane Paulo II alimteua kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo Katoliki TUNDURU- Masasi na tarehe 30/01/2005 aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki TUNDURU – Masasi katika Kanisa kuu la Mtakatifu Fransisco Xavery.
Amekuwa Askofu Mwandamizi (Askofu mwenye haki ya kurithi Jimbo). Kwa muda wa miezi saba hadi tarehe 25/08/2005 alipochukua Jimbo na kuwa Askofu rasmi wa Jimbo.

Toka hapo amekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki TUNDURU-Masasi akijishughulisha katika mambo mengi ya kiroho na kimwili.

Katika kukabiliana na uhaba wa miito aliamua kujenga seminari ndogo ya Jimbo katika Parokia ya Muhuwesi. Pamoja na seminari hiyo amejenga nyumba ya mapadri iliyopo nyuma ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Francisco Xavery.
Katika ngazi ya kitaifa amekuwa akijishughulisha na Uhusiano wa dini mbalimbali chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Afya yake ilianza kuzorota tangu mwaka jana mwezi wa pili. Alipatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili Dar es salaam. Kutoka Muhimbili alikwenda Chenai, India katika Hospitali ya Apolo.
Mhashamu Baba Askofu amefariki mjini Muscat Oman akiwa tena safarini kuelekea India kwa matibabu.


SHUKRANI
Wana taifa la Mungu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Jimbo Katoliki TUNDURU- Masasi tunatoa shukrani kwa madaktari wa Hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa jitihada zao za kuokoa  maisha ya baba yetu mpendwa. Tunawashukuru Madaktari wa hospitali ya Apolo huko Chennai India kwa kumpatia matibabu marehemu.

Shukrani za pekee zimwendee Sr. Beatrice Kayombo OSB wa shirika la Wabenediktini wa Mt. Agnes nyumba ya Immiliwaha Njombe kwa  kumtunza baba yetu. Yeye kama mtawa na daktari amekuwa msaada mkubwa kwa baba Askofu wakati wote wa ugonjwa wake.

Tunatoa shukrani zetu kwa ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa ushirikiano waliotupatia tangu tulipopatwa na msiba hadi kurejesha mwili wa baba yetu mpendwa hapa Tanzania.


Shukrani zetu za pekee kwa Padri Jacob Mchopa ambaye amekuwa akimtunza  marehemu baba Askofu wakati wa ugonjwa wake.  Tutakuwa watovu wa shukrani tusipomtaja Mhashamu Baba Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe ambaye alijitoa kwa hali na mali katika matibabu ya marehemu baba Askofu.

Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake na libarikiwe!

RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA…..! NA MWANGA WA MILELE UMWANGAZIE! APUMZIKE KWA AMANI … AMINA!



Imeandaliwa na
Kurugenzi ya Mawasiliano TEC na Padri Martin Amlima
Katibu wa Jimbo – Tunduru Masasi

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI