"TUSIPOFUNDISHA DINI SHULENI MAOVU HAYATAKOMA"
PADRI Gaitan Maswenya, Paroko wa
Parokia ya Makole Jimbo Kuu Katoliki Dodoma amesisitiza umuhimu wa watoto wa
shule za msingi na sekondari kufundishwa somo la dini shuleni kwao ili
kuwajenga kiroho na kiutu.
Padri Maswenya amesema hayo hivi
karibuni alipokuwa akizungumza na KIONGOZI katika mahojiano maalumu.
Amesema kuwa somo la dini shuleni
linasaidia kuwajenga watoto kumjua Mungu na kuwafanya wawe wanyenyekevu, hivyo
kuwaepusha na majaribu mbalimbali ya shetani ikiwemo vitendo vya wizi, ujambazi
na maovu mengine.
“Watoto hawa wanafundishwa masomo ya
kawaida na walimu wao, lakini bila ya kuwafundisha somo la dini tutegemee
kuvuna mabua,” amesema padri Maswenya.
Ameongeza kuwa Serikali imeandaa
mazingira mazuri ambapo imeruhusu viongozi wa madhehebu ya dini kufika katika
shule za msingi na Sekondari kufundisha, hivyo hakuna kisingizio chochote cha
kukosa kwenda kuwafundisha somo hilo.
“Watoto hawa wengine hawana fursa ya
kupata neno la Mungu kwa sababu miongoni mwao hawaendi kanisani kwa sababu moja
ama nyingine, kumbe somo la dini litasaidia kuwainjilisha na hivyo kumjua
Kristo mkombozi wa dunia.”
Padri Maswenya amefafanua kuwa ili
Kanisa liweze kumtangaza Kristo ni lazima lianzie chini kwa watoto wakiwemo
wale walioko shuleni.
Amewaasa wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari kuwasikiliza kwa umakini mapadri na viongozi wengine wa
dini wanapofika shuleni kuwafundisha somo la dini ili waweze kulifahamu neno la
Mungu ambalo litawasaidia kujenga urafiki na Mwenyezi Mungu.
Katika hatua nyingine Parokia hiyo
imefanya sherehe ya kumkumbuka somo wake Mtakatifu Gaspal del Buffalo Alhamisi
hii ambapo Ibada ya misa takatifu na mashangilio mbalimbali pamoja na chakula
cha pamoja yamefanyika.
Padri Maswenya amewashukuru
waamini wote wa Parokia hiyo kwa majitoleo yao ambayo yamekuwa yakifanikisha
shughuli mbalimbali parokiani hapo.
Comments
Post a Comment