BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI KENYA LASISITIZA AMANI
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linaialika familia ya Mungu nchini Kenya, kujenga na kudumisha amani na utulivu, tayari kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kufikia muafaka kuhusu mabadiliko ya Katiba yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa wananchi wote wa Kenya! Raia wanataka nchi ambayo inasimamia: ukweli; inatetea haki na kukemea maovu. Ikiwa kama Serikali na taasisi zake hazitekelezi kwa dhati vipaumbele hivi basi lengo lake ni kuendelea kufaidika na jasho la wananchi pasi na maboresho ya dhati katika huduma!
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavitaka vyama vya kisiasa nchini Kenya pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kukaa na kujadiliana kwa pamoja, ili kuibua mwongozo utakaowezesha uchaguzi wa marudio hapo tarehe 26 Oktoba 2017 kuwa: huru, wa haki na unaoaminika walau na wananchi wote. Maaskofu wanavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba, vinatekeleza dhamana na wajibu wao barabara, ili: utawala wa sheria, haki na usawa viweze kutawala tena.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, mazingira ya sasa ya “vuta nikuvute” yanayoundwa na wanasiasa, yanaweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa! Ndiyo maana kuna haja ya kujikita katika mchakato wa majadiliano, kwa kuongozwa na dhamiri nyofu; ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Kenya ili kuimarisha utawala bora unaokumbatia utu wa binadamu na haki zake msingi. Machafuko hayana budi kuepukwa kwa gharama yoyote ile kwani madhara yake ni makubwa kwa maisha ya wananchi wote wa Kenya katika medani mbali mbali za maisha!
Maaskofu kwa kutumia maneno ya Nabii Ezekieli 3:17-19 wanapenda kuwaonya watu wenye nia mbaya, kuachana na mwenendo huo, kwa kuokoa roho zao na kuanza kutenda mema. Maaskofu wanamshauri Rais Uhuru Kenyatta kuwa ni alama ya umoja wa kitaifa kwa kuonesha ujasiri na moyo mkuu katika kipindi hiki cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi mkuu na baada ya matokeo. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ndiyo yenye dhamana ya kusimamia uchaguzi mkuu nchini Kenya na kwamba, wanaipongeza kwa sera na mikakati inayochukuliwa kwa wakati huu ili uchaguzi ujao wa Rais uweze kuwa huru, wa haki, amani na wenye kuaminika.
Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, changamoto zilizotolewa na viongozi wa vyama vya kisiasa nchini Kenya zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya majadiliano katika ukweli, uwazi, daima kwa kuzingatia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika tamko lake linakaza kusema, linaguswa sana na kilio na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Kenya hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marudio! Wanataka kuona wote wanakuwa washindi kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; badala ya maandamano, vurugu na ghasia ambazo hazina mvuto wala mashiko kwa ustawi wa maendeleo na demokrasia ya kweli nchini Kenya. Hotuba za chuki na uchochezi, hazina nafasi tena, bali wanasiasa wajikite katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika majadiliano, umoja, upendo na mshikamano wa kidugu! Uchaguzi unakuja na kupita, lakini umoja na udugu ni mambo ya kudumu! Tamko hili limetiwa mkwaju na Askofu Philip Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.
Comments
Post a Comment