SIKU YA CHAKULA DUNIANI: PAPA FRANSISKO ATOA MBINU ZA KUPAMBANA NA NJAA
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Oktoba 2017 katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2017 yanayoongozwa na kauli mbiu “Badili mwelekeo wa uhamiaji; Wekeza katika usalama wa chakula na maendeleo Vijijini” ametembelea Makao Makuu ya Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO na kuzungumza na viongozi wakuu pamoja na wajumbe maalum na baadaye kutoa hotuba yake katika maadhimisho haya, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 72 tangu FAO ilipoanzishwa na Miaka 36 tangu Jumuiya ya Kimataifa ianze kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani. Amegusia uhusiano uliopo kati ya baa la njaa na uhamiaji; umuhimu wa kubadili mwelekeo kwa kusikiliza kilio cha watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekumbusha kwamba, ilikuwa ni tarehe 16 Oktoba 1945 viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa walipoanzisha Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO ili kupambana na baa la njaa duniani lililokuwa limesababishwa na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. FAO ikaanzishwa ili kusaidia kuweka usawa katika mgawanyo wa chakula duniani sanjari na kuhakikisha kwamba, haki ya chakula inalindwa kwa wote. Baa la njaa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu kiasi kwamba, hata ule umoja na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa unakwamishwa kiasi hata cha watu kushindwa kupata msaada wa chakula cha dharura na matokeo yake, watu wanakufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.
Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kupambana na baa la njaa duniani linalotokana na vita pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi; ukosefu wa fursa za ajira na uhamiaji, kwa kuwekeza katika maendeleo ya teknolojia rafiki itakayosaidia kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu kwa kudhibiti kiwango cha watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani au watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Haki ya Kimataifa inaonesha njia ambazo zinapaswa kufuatwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kutatua kinzani, migogoro na vita mambo yanayochangia ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Wimbi kubwa la wahamiaji linapaswa pia kudhibtiwa kwa kudhibiti biashara haramu ya silaha duniani ambayo inaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Amani na utulivu ni nguzo msingi katika mapambano ya baa la njaa duniani. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni chanzo kingine kinachopelekea watu kuendelea kutumbukia katika baa la njaa duniani.
Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao sasa kuna baadhi ya nchi zinajitoa ni muhimu sana katika kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali kwa ajili ya faida kubwa kwa gharama ya maskini ambao wanateseka sana. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kubadili mtindo wa maisha, matumizi ya rasilimali ya dunia, vigezo vya uzalishaji na tabia ya ulaji, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kutunza chakula. Dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha watu wote, tatizo ni ubinafsi na uchoyo unaofumbatwa katika faida kubwa na matokeo yake ni kinzani na ongezeko la watu maskini wanaotafuta msaada wa chakula duniani.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapa kuna haja ya kubadili mwelekeo kwa kujenga utamaduni wa kuhifadhi chakula, jambo linalohitaji wongofu wa ndani; umoja na ushirikiano wa kimataifa kwa kujikita katika utu, heshima ya binadamu na usalama wake; mambo yanayofumbatwa katika upendo na haki; ili kubainisha: sera na mifumo mipya ya maendeleo na ulaji sanjari na kuwajengea watu uwezo wa kuzalisha chakula chao wenyewe badala ya kuwa tegemezi wa msaada wa chakula kutoka nje pamoja na kujenga utamaduni wa watu wa Mungu kushirikishana kile walicho nacho!
Juhudi hizi ziende sanjari na udhibiti wa matumizi ya silaha ambazo zinasababisha vita na hatimaye, kuwatumbukiza watu katika baa la umaskini. Utu wa binadamu ni kanuni msingi inayopaswa kutekelezwa na wote. Udhibiti wa wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi linahitaji ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuzingatia sheria, kanuni na itifaki za Jumuiya ya Kimataifa. Hapa, anasema Baba Mtakatifu, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwajibika bara bara kwa kuzingatia diplomasia inayobainishwa kwenye Mkataba wa Kimataifa kuhusu usalama wa wahamiaji na wenye mpangilio thabiti.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kilio cha maskini kinaweza kufupishwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, hali inayohitaji kupata majibu muafaka, uwajibikaji, mshikamano na umoja unaofumbatwa katika udugu. Jumuiya ya Kimataifa iwajengee watu uwezo wa kiuchumi katika nchi zao, ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kukimbia makwao kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, umaskini na magonjwa mambo yanayo kwamisha matumaini ya maisha ya watu wengi duniani.
Kuna haja ya kuwekeza katika miundo mbinu na rasilimali fedha ili kupambana na baa la njaa na umaskini sanjari na udhibiti wa wimbi la wakulima wakubwa wakubwa kutaka kupora maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya mafao ya watu wachache. Sera na mwelekeo mpya ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuondokana na kishawishi cha rushwa na ufisadi; kwa kujikita katika utawala bora unaoheshimu pia utawala wa sheria. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake zote litaendelea kujielekeza zaidi katika kuwahudumia wote pasi na ubaguzi kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na wito wake, hii pia ni changamoto kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wajumbe wataweza kuchangia kwa hali na mali, ili kuiwezesha FAO kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili mafao, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment