STENDI KUU WAANZISHA JUMUIYA, WAWA MFANO KWA WENGINE
WAKRISTO
wanaofanya kazi katika maeneo ya stendi kubwa nchini wameshauriwa
kuanzisha umoja wa jumuiya ndogondogo katika maeneo yao ya kazi ili kushiriki
masuala ya ibada na taratibu za Kanisa kwakuwa wengi wao hawashiriki kusali
jumuiya katika makazi yao kwani muda mwingi wanautumia katika mazingira yao ya
kazi.
Wito huu
umetolewa na wanajumuiya ya “watakatifu wote” wafanyao kazi katika
maeneo ya Stendi Kuu jimboni Sumbawanga hivi karibuni wakati wa maandamano ya
matembezi ya msalaba wa Jubilei ya miaka 50 ya parokia ya Kanisa Kuu jimboni
humo ambapo maandamano hayo ya kutembeza msalaba yaliuteka mji wa
Sumbawanga kuanzia maeneo ya stendi kubwa ya mabasi iliyopo Sokomatola na
kuhitimishwa katika parokia ya Kanisa Kuu na kupokelewa na Askofu wa Jimbo
Katoliki Sumbawanga Mhashamu Damian Kyaruzi.
Akizungumza kwa
niaba ya wanajumuiya ya Watakatifu Wote, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Ernesti
Kasanka amesema kuwa tangu alfajiri hadi jioni wanashinda stendi, kwa maana
hiyo wengi wao hawashiriki ibada za jumuiya majumbani na hivyo kusababisha
kukosa huduma za kiroho pale inapotokea matatizo kwa wenzao au uhitaji wa
sakramenti za Kanisa kwani wanakuwa na vipingamizi vya kutoshiriki ibada hivyo
kuomba kuanzisha jumuiya katika maeneo yao ya kazi.
“Kwa kiasi
kikubwa sana tunaofanya kazi katika mazingira ya stendi hatushiriki ibada,
tunaonekana ni kama wahuni, watu wa fujo na kwakuwa mazingira ya kazi zetu toka
alfajiri mpaka jioni tunakuwa stendi hivyo tuliamua kuomba kuanzisha jumuiya
kwa kufuata taratibu na miongozo ya Kanisa na kuchagua viongozi
tulikubaliwa na mpaka sasa kila siku za jumamosi saa kumi jioni tunakutana
katika moja ya ofisi na kusali, na kwa mantiki hii tunashauri pia wakristo wakatoliki
wenzetu wanaofanya kazi katika mazingira ya stendi kama sisi katika mikoa yote
ya Tanzania waungane waanzishe jumuiya, na viongozi wa Kanisa watusaidie kwa
hili maana itasaidia kuimarisha na kuongoa watu, kupunguza maovu na hata
itasaidia kuondoa dhana potofu ya kuwa watu wanaofanya kazi stendi ni
wahuni, hawafai wasiomcha Mungu wala kuwa na hofu ya Mungu kitu ambacho si
kweli, tunajua umuhimu wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya kila mwanadamu,
ingawa mazingira yetu ya kazi yanakua ni changamoto kushiriki jumuiya
nyumbani,” amesema Ernest Kasanka.
Naye Filbert
Lwela maarufu kwa jina la Sumbuko, mmoja wa wanajumuiya ya Watakatifu Wote
amesema kuwa ni manufaa mengi ambayo wameyapata tangu kuanzishwa kwa jumuiya
hiyo kwani vijana wengi wameweza kujitambua na kuanza kufunga ndoa hata
kushiriki sakramenti za Kanisa lakini pia imesaidia kupunguza vurugu na tabia
zisizofaa kwa baadhi ya vijana.
“Tumeiita
jumuiya ya Watakatifu Wote kwakuwa ni mkusanyiko wa watu wengi na wanatoka
katika vigango na parokia mbalimbali na imetusaidia kama mimi na wenzangu
tumeshaandikisha ndoa na sasa tumejitambua, tabia ya ulevi asubuhi, wizi,
udokozi, uhuni na kila aina ya tabia mbaya huonekana katika maeneo ya stendi, lakini kwa sasa unashangaa
kuona vijana wa stendi kuwa na hofu ya Mungu kiasi kikubwa, na baadhi yao
waliasi dini sasa wanarudi na wengine kubadili dini na kuja katika Kanisa
Katoliki kwani tunashirikiana katika shida na raha kama zilivyo jumuiya
zingine,” amesema Sumbuko
Jumuiya ya
watakatifu wote jimboni Sumbawanga imeanzishwa mwezi wa pili mwaka huu na
imekuwa mfano pekee wa kusaidia kubadilisha imani na kuleta utulivu na jitoleo
kwa Mungu ambapo jumuiya hii itazinduliwa tarehe 29 Novemba na
inaongozwa na Mwenyekiti Ernest Gervansi Kasanka, Makamu Mwenyekiti ni Paskali
Chakupewa, Katibu Mkuu Nuru Abdul, Katibu Msaidizi Ladislaus Wasoka na mweka
hazina Ernest Boazi (Shamba boy).
Comments
Post a Comment