TUSIIACHIE JAMII ITULELEE WATOTO
Dunia kwa sasa inashuhudia maeneo mbalimbali yakikabiliwa na
maovu, ambayo licha ya kwenda kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu, pia
yanaviumiza viumbe vyake alivyoviumba.
Wakati wa uumbaji, Mwenyezi Mungu alikusudia dunia iwe
sehemu nzuri na ya raha kwa kila kiumbe chake. Binadamu, wanyama, wadudu na
mimea tofauti na makusudio ya muumba, vinaendelea kuteseka na mahangaiko ya
kila kukicha.
Uharibifu wa mazingira, vita, ujambazi, utekaji nyara,
ulawiti, ubakaji na maovu mengi yameendelea kuigubika dunia giza, tofauti na
kusudio la muumba.
Yote haya kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mwanadamu.
Kiumbe ambacho Mwenyezi Mungu alikiumba kwa mfano wake. Swali la kujiuliza kama
binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu maovu yanatoka wapi?
Wazazi tumejisahau kwa kiasi kikubwa. Mtaa hauzai mtoto,
magereza hayazai mtoto, bunduki hazizai mtoto, majangwa na ukame havizai mtoto,
mtoto anazaliwa na mwanadamu tena mwenye mfano wa Mungu. La kujiuliza hapa ni
je, imefika wakati tumeviachia vitu hivyo vituzalie na kutulelea watoto?
Kisingizio kikubwa kwa sasa kimekuwa “ubize”. Kweli,
kulingana na hali ya maisha ambayo hairuhusu jinsia moja tu ndio itafute, wote
baba na mama wanatafuta ili kuwajengea watoto maisha mema ya baadaye. Pamoja na
utafutaji huo, bado hatutakiwi kujisahau katika utafutaji huku tukiwaachia
watumishi wa ndani, walimu, majeshi, magereza, NGO’s na taasisi za kidini
zitufundishie watoto wetu tabia.
Wazazi lazima tutambue kuwa jukumu la kuijenga kesho ya
mtoto linaanza na sisi. Tusikwepe majukumu eti kwa kuwapeleka watoto mbali na
sisi ili tupate nafasi ya kutimiza mahitaji yetu ya kimaisha hasa utafutaji wa
pesa. Inasikitisha kukuta mzazi anampeleka mtoto mdogo ambaye hata kuongea
vizuri hajaweza akasome shule ya bweni. Hapo unatarajia nini? Hiyo pesa
unayotafuta itaziba matokeo ya mwanao kukengeuka kitabia?
Tukae nao, tusali nao, tuwasimulie hadithi, tuwape mifano ya
mafanikio, mifano mizuri inayowajenga katika misingi ya upole, huruma,
kusamehe, nidhamu, upendo na uvumilivu. Tusiwakwepe au kuwaweka mbali nasi.
Tujitahidi sana kuziba mianya ya wao kukaa mbali nasi na hatimaye kupata nafasi
ya kusomba tabia za ajabuajabu ambazo mwisho wa siku zinarudi kwetu.
Majambazi, wauaji, vibaka, wabakaji, walawiti, waharibifu wa
mazingira, watekaji hawajatumwa na Mungu kuja kufanya hayo. Ni matokeo ya sisi
wazazi kuwaweka mbali na hatimaye wakapata “walimu” mitaani au magheto hadi
kufikia hapo. Humwoneshi upendo mwanao kila siku vipigo, matusi, kebehi,kashfa
na kumdhalilisha, huchezi naye, unamtenga, humtimizii mahitaji yake, humpi
mafunzo ya kiimani, humpi nafasi ya kufurahia uwepo wako duniani, hapo
unatarajia nini?
Mwenyezi Mungu wabariki watoto wetu.
Bernard James
Comments
Post a Comment