"HAKUNA TALAKA KANISA KATOLIKI"
KANISA Katoliki linaamini kwamba ndoa ni makubaliano ya mke mmoja
na mume mmoja ambapo baada ya makubaliano hayo yaliyofanyika kihalali, hakuna mahakama
yeyote inayoweza kutoa talaka kuwatenganisha wanandoa hao vinginevyo mpaka kifo
kitakapowatenganisha kadiri ya mpango wa Mwenyezi Mungu.
Ndoa katika Kanisa Katoliki ni miongoni mwa Sakramenti saba,
tena ni tendo la kudumu ambalo linafanyika kwa uhalali katika vigezo vyote kwa lengo
la kuwapatanisha na kuwaunganisha watu hao wawili kuwa mwili mmoja ili kuunda familia
takatifu hatimaye kujenga Kanisa dogo la nyumbani.
Moja ya majukumu yanayopaswa
kutekelezwa na wanandoa mara baada ya kufunga ndoa ni kujihusisha na shughuli za
Kanisa mojawapo ikiwa ni kulipa zaka na michango mingine ya Kanisa, japokuwa kumekuwepo dhana potofu miongoni mwa waamini hasa
wanandoa mara baada ya kupata sakramenti hiyo kushindwa kushiriki tena shughuli
za Kanisa mfano ibada za jumuiya na ulipaji wa zaka huku wakidhani kwamba si jukumu
lao.
Hayo yameelezwa na padri
Abdon Nzegesera wa parokia ya Ilonga jimboni
Morogoro katika adhimisho la ndoa takatifu lililofanyika hivi karibuni ambapo
jumla ya ndoa saba zimefungwa kwa pamoja katika Kigango cha Mtakatifu
Maria mama wa Rozali Takatifu kilichopo Msowero jimboni humo ambayo ni miongoni
mwa juhudi za kutokomeza kabisa uchumba sugu.
Padri Abdon amesema kuwa ndoa ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
hakuna mwanadamu mwenye mamlaka ya kuitenganisha kutokana na sababu yoyote itakayoweza
kujitokeza ambapo ni wajibu wa kila mmoja kujitafakari kwa kina kabla ya kuingia
katika agano hilo hali ambayo wakati mwingine wengi wao hutamani kudai talaka mara
baada ya kutawala magomvi na mifarakano katika familia hatimaye kutengana kabisa
kinyume na sheria za Kanisa.
“Mtambue kwamba chochote kinachounganishwa na Mwenyezi Mungu
hakuna mwanadamu mwenye mamlaka ya kutenganisha, ndoa ikishafungwa kanisani kwa
utaratibu wa Kanisa kwa uhalali na vigezo vyote, asitokee mtu akaenda kwenye
mahakama fulani ya kijiji au serikali kuomba talaka kwa sababu zozote, hakuna atakayeweza kutoa maamuzi kinyume
na sheria za Kanisa Katoliki kwa sababu linapinga uwepo wa talaka na kuwatenganisha
mke na mume zaidi ya Mungu mwenyewe kupitia
fumbo la kifo, ukikubali kuingia humu ni afadhali uchukue maamuzi kabla hujasema
ndiyo, siyo kama nawatisha ili muogope bali
nawaimarisha mpendane kimamilifu,” amesema padri Nzegesera.
Mbali na hayo padri Nzegesera amesisitiza kuwa changamoto katika
maisha ya ndoa zipo, na isiwe chanzo kimojawapo cha kushindwa kuvumiliana, huku
akiwahimiza zaidi kudumu katika sala wasisubiri tu kumwomba Mungu na kusali baada
ya misukosuko, bali nyumba zao ziwe Kanisa dogo la nyumbani kupata amani,
uvumilivu na upendo.
Kwa hiyo na ninyi msisubiri mpaka misukosuko itokee ndio mkumbuke kwamba kuna Kanisa, msisubiri mpaka mpate shida
ndipo mkumbuke kwamba Mungu yupo, msisubiri mpaka migogoro iwazidi ndio muanze kusali,
daima muwe watu wa sala muwaalike watakatifu wa mbinguni waweze kuwaombea katika
nyumba zenu, majaribu yatakuwepo lakini mkidumu katika sala nyumba zenu zitakuwa
Kanisa dogo la nyumbani, si ajabu hawa hawa
wanaoshuhudia ndoa hizi wakawa wa kwanza
kuleta majaribu katika ndoa zenu, vumilieni yote Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja nanyi,” amesema padre Nzegesera.
Naye Nicholaus Mbota mmoja wa waliofunga ndoa, awali akizungumza
kwa niaba ya wanandoa wenza amesema kuwa
waamini walio wengi wanaishi nje ya ukatoliki bila ndoa takatifu kwa kulenga ubinadamu
zaidi hasa kuogopa gharama za sherehe, inafika wakati kunajengeka mazoea ya kuzoeana
mke na mume na kuweka mbali baraka ya ndoa takatifu kwa misingi ya Kanisa kuishi
nje ya masakramenti ya Kanisa, kumbe jambo
la msingi ni kutimiza sheria za Kanisa bila kujali kula na kunywa kuliko kuishi nje ya baraka.
“Kikubwa tuombeane na
kupendana, suala la ndoa ni kuvumiliana, kupendana, kuchukuliana,
kusameheana na kubebeana mizigo, nadhani neno samahani linaweza
kuokoa ndoa ambayo wakati mwingine ilikuwa katika hatari ya kufa, mara nyingine kujishusha na kumjua mwenzi wako ni dawa tosha inayoweza kutusaidia kuishi
maisha ya amani bila kukengeuka kwa sababu
hata kutoka nje ya ndoa inatokana na mmojawapo kutomthamini mwenzi wake, tukiyaishi hayo kila mmoja atakuwa na hofu ya Mungu ndoa zetu zitakuwa imara zaidi,”
amesema Mbota.
Maadhimisho ya ndoa
hizo ni miongoni mwa juhudi zinazofanywa na viongozi wa kiroho hasa paroko Abdon
Nzegesera kushirikiana na makatekista wa vigango vinavyozunguka parokia hiyo,
ili kuhakikisha kwamba uchumba sugu unapotea miongoni mwa waamini katika Kanisa
ili kila muamini awe huru kushiriki masakramenti ya Kanisa hasa Komunio
Takatifu.
Parokia ya Ilonga imekuwa na mwendelezo wa kuwakomboa
waamini waishio katika uchumba sugu kwa kuwahimiza waamini hao kupitia paroko
wao padri Abdon Nzegesera pamoja na makatekista wa vigango hivyo kuepuka
uchumba sugu kuishi na familia bila kufunga ndoa takatifu ambapo kuna jumla ya
ndoa 18 za waamini waliokuwa wanaishi maisha ya uchumba sugu zimekombolewa,
ndoa 11 kutoka kigango cha Gongoni B ndani ya kipindi cha miezi miwili
iliyopita na ndoa 7 kutoka kigango cha Msowero parokiani hapo.
Comments
Post a Comment