TEMEKE YAUNDA KAMATI YA MAHUSIANO BAINA YA DINI MBALIMBALI
Wajumbe wa Kamati ya Mahusiano baina ya Watu wa Dini
Mbalimbali wilayani Temeke wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya
kuchaguliwa (Picha na Dalphina Rubyema)
ILI kusimamia shughuli za ustawi wa mwanadamu pasipo kufungamana na
upande wowote wa kidini, Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam imefanikiwa kuunda
Kamati ya Mahusiano ya Dini mbalimbali (Interfaith) itakayodumu kwa kipindi cha
miaka mitatu.
Kamati hiyo yenye wajumbe kutoka
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), imeundwa hivi karibuni wakati wa
kikao cha siku mbili kilichoratibiwa na ofisi ya Mradi wa Uendelezaji wa Utu wa
Mwanadamu (IHDP) unaotekelezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
kupitia Idara yake ya Haki, Amani na Uadilifu katika Uumbaji (JPIC) na kufadhiliwa
na Shirika la Misaada kwa Makanisa la Norway (NCA).
Viongozi hao waliochaguliwa na
nafasi zao zikiwa kwenye mabano ni pamoja na Sheikh Zailaih B. Mkoyogope kutoka
BAKWATA (Mwenyekiti), Padri Andrew Mtweve toka CCT (Makamu Mwenyekiti),
Mchungaji Manase Mwakalile toka CCT (Katibu), Sheikh Ali Mohamed Ali toka
BAKWATA (Katibu Msaidizi) na Padri
William Sindano toka TEC (Mhasibu).
Akizungumza kabla ya kuundwa kwa
Kamati hiyo, Mkurugenzi wa Mahusiano baina ya Dini Mbalimbali , Jimbo Kuu
Katoliki Dar es Salaam, Padri Christian Likoko ambaye pia ni Mshauri wa Kamati
hiyo amewaambia washiriki wa kikao hicho kuwa pamoja na mambo mengine, kuundwa
kwa kamati hiyo kutawezesha wanaTemeke kujumuika kwa pamoja kujadili mambo ya amani na maendeleo kwa jamii kwa ufanisi zaidi
bila kuathiri imani ya mtu.
“Uhusiano huu si kwa ajili ya kuingilia
au kuathiri imani…kila imani itaendelea kusimama na misingi yake iwe ni kiibada
na kuongoza bila kuingiliwa,” amesema Padri Likoko ambaye pia ni Paroko wa
Parokia ya Kanisa la Mashahidi wa Uganda, Magomeni Jimbo Kuu Katoliki Dar es
Salaam na Mshauri wa Kamati hiyo.
Amesema kamati hiyo pia itakuwa
na jukumu la kujadili kwa kina vyanzo mbalimbali vinavyoweza kuchochea vurugu
na uvunjifu wa amani hivyo kujadili njia bora ya utatuzi.
“Pia kamati itashauri ama kupanga
na kutekeleza programu mbalimbali za pamoja zenye lengo la kuleta maendeleo na
uwajibikaji kwa jamii katika maeneo ya wilaya ya Temeke,” amesisitiza.
Kwa sasa shughuli za maendeleo
zinazosimamiwa chini ya Mahusiano baina ya Dini mbalimbali wilayani Temeke ni
zile zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Utu wa Mwanadamu (IHDP)
TEC kupitia Idara ya Haki, Amani na Uadilifu katika Uumbaji (JPIC) kwa
kufadhiliwa na Shirika la Misaada kwa Makanisa la Norway (NCA).
Awali akitoa utambulisho kwa
washiriki wa kikao hicho na shughuli zinazofanyika chini ya IHDP, Mratibu wa
Taifa wa Mradi huo Joyce Lusatila, amesema shughuli zimejikita katika maeneo
makuu mawili ambayo ni pamoja na Uwezeshaji wa Kiuchumi (Economic Empowerment)
na Ulinzi wa Rasilimali (Resource Governance).
Amesema chini ya uwezeshaji wa
kiuchumi shughuli zinazofanyika ni pamoja na zile za Benki za Kijamii Vijiji za
Watu wa Dini Mbalimbali (IR-VICOBA) wakati ulinzi wa rasilimali unahusisha
masuala ya kuwezesha jamii katika ngazi za msingi kufuatilia Rasilimali za Umma
zinazotolewa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Maendeleo katika maeneo yao
(PETS). Hata hivyo amesema kuna masuala mtambuka yanayofanyika chini ya mradi
huo ambayo aliyataja kuwa ni jinsia na usaidizi wa kisheria.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa,
Mwenyekiti Sheikh Zailaih Mkoyogope, amesema kamati hiyo itafanya kazi kwa
kujituma kwa maslahi ya wananchi wa Temeke bila kujali itikadi za kisiasa, dini,
kabila na rangi.
“Tunachoomba ni kupewa ushirikiano
unaostahili kutoka TEC kwani kama tulivyoambiwa awali kwamba shughuli hizi
upande wa Temeke zinasimamiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kazi
kubwa iliyopo mbele yetu ni kwenda kujitambulisha kama Kamati kwa Mkuu wa
Wilaya pamoja na kuunganishwa na wawezeshaji hasa IR-VICOBA na kamati za PETS
ili tuweze kuwafikia walengwa wengine,” amesema.
Shughuli za Usimamizi wa Mradi wa
Uendelezaji wa Utu wa Mwanadamu wilayani Temeke chini ya TEC zilianza mwaka
2008.
Comments
Post a Comment