UNAFIKI NI SUMU KALI SANA
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 17 Oktoba, anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Antiokia, Askofu na mfiadini, aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican amekazia umuhimu wa waamini kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu ili liweze kuwa ni dira na mwongozo katika maisha yao. Yesu anasikitika sana pale wafuasi wake wanapotumbukia katika unafiki kwa kuzingatia maisha ya nje na kusahau kujikita katika mchakato wa maboresho ya maisha ya kiroho.
Baba Mtakatifu alikuwa anafanya rejea juu ya lawama ambayo Yesu aliwatolea Mafarisayo na waalimu wa Sheria, walioacha mambo ya adili pamoja na kufanya mapenzi ya Mungu wakajikuta wakipotea njia na kutumbukia katika rushwa na mmong’onyoko wa maadili. Waalimu wa sheria walifananishwa na Yesu kuwa kama makaburi yaliyopakwa rangi yakang’aa kwa nje, lakini ndani mwake, kulijaa mifupa tupu! Ni watu waliopenda kuonekana kwa nje, lakini kutoka katika undani wa maisha yao, ni watu waliokuwa wanatembea gizani; walisimamia haki na uzuri wa mambo ya nje, lakini wakashindwa kushughulikia maisha yao.
Ni watu ambao walikuwa na ufahamu mkubwa ambao ungewasaidia kumtambua Mwenyezi Mungu, lakini wakamezwa zaidi na malimwengu! Wapagani wanashutumiwa kwa sababu ya kupenda mno malimwengu kwa kuchanganya utukufu wa Mungu na mambo ya kidunia. Makundi yote haya matatu anasema Baba Mtakatifu, yameshindwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Ukristo, kwa kuwa na “kichwa maji” kiasi hata cha kushindwa kusikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yao.
Ni watu ambao, uhuru wa kweli, upendo na huruma ya Mungu haina nafasi tena mioyoni mwao na matokeo yake wamekuwa ni watumwa wa mawazo na matendo yao, kiasi cha kuabudu viumbe badala ya kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana! Waamini wanaposhindwa kusikiliza, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wanageuka kuwa watumwa. Neno la Mungu ni sawa na upanga wenye makali kuwili.
Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuwa makini katika maisha yao, kwani wanaweza kuwa ni kikwazo kikubwa kwa waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kristo Yesu, daima yuko malangoni pa maisha ya waja wake, anabisha hodi, mtu akimfungulia, ataingia na kukaa pamoja naye, ili kumwonjesha upendo wake usiokuwa na kifani! Yesu anasikitika sana anapowaona wafuasi wake wakimezwa na malimwengu ndio maana aliulilia mji wa Yerusalemu, ambao ulishindwa kuonesha upendo wa dhati baada ya kuteuliwa na Mwenyezi Mungu, kwa kukazia mambo ya nje badala ya kujikita katika maboresho ya maisha ya kiroho na kiutu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment