PAPA FRANSISKO ATOA KAULI MBIU SIKU YA UPASHANAJI HABARI DUNIANI 2018


Kauli mbiu ya Siku ya Upashanaji Habari Duniani kwa  mwaka 2018 ni “Kweli itawaweka huru" Yoh. 8:32. Habari potofu na uandishi  wa amani". Ndiyo iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ambayo huadhimishwa kila mwaka wakati wa Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni na mwaka 2018 itakuwa ni tarehe 13 Mei. Habari potofu zimekuwa na athari kubwa sana katika maisha ya watu! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waandishi wa habari kujikita katika uandishi unaopania kujenga na kudumisha amani duniani.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu utachapishwa rasmi tarehe 24 Januari 2018 wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Francis wa Sales, msimamizi wa waandishi wa habari! "Fake news" Habari potofu" ni mada inayochangamkiwa sana na vyombo pamoja na taasisi mbalimbali kutokana na unyeti na utata wake katika maisha ya watu na taasisi husika. Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican inataka kuchangia katika mchakato wa kukuza na kudumisha ukweli katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kwa kujikita katika sababu zinazopelekea watu kuandika habari potofu, mantiki iliyo nyuma yake na "uchafuzi wa hali ya hewa" katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kunakofanywa kwa makusudi na baadhi ya waandishi wa habari kinyume kabisa cha kanuni maadili, weledi, uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza haki ya watu kupata habari za kweli na za uhakika, muhimu katika ujenzi na udumishaji wa wa Injili ya amani duniani!
Habari za kughushi zimeleta madhara makubwa sana katika maisha ya watu binafsi, serikali na jamii katika ujumla wake! Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican inataka kukazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa uandishi wa habari unaojikita katika weledi, daima ukitafuta ukweli katika maisha na ukweli huu, uweze kuwaweka watu huru! Uandishi wa habari unaosimikwa katika ukweli unapania kuleta umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii kati ya watu!
Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya kiswahili ya Radio Vatican

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI